Na Charles Ndagulla,Moshi

Hatua ya kutofungwa pingu kwa mmoja wa Wakurugenzi wa Shule ya Sekondari ya Scolastica, Edward Shayo (63), anayetuhumiwa kwa mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa shule hiyo, Humphrey Makundi imezua utata na kuhojiwa na baadhi ya mahabusu wa gereza la Karanga mjini Moshi.

Shayo alikuwa miongoni mwa watuhumiwa 11 waliokamatwa kufuatia mauaji ya mwanafunzi huyo aliyetoweka shuleni hapo Novemba 6, na mwili wake kuokotwa Novemba 10, mwaka jana ukielea kwenye mto Wona uliopo takribani mita 300 kutoka shuleni hapo.

Hata hivyo, watuhumiwa nane katika shauri la mauaji hayo wameachiwa huru katika mazingira ambayo baadhi ya wakazi wa mjini Moshi walianza kuhisi kwamba ‘wameyeyuka’ pasipo kujulikana walipo.

Hadi sasa ni watuhumiwa watatu pekee  waliofikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkaazi Moshi  na kusomewa shitaka moja la mauaji ya kukusudia.

Watuhumiwa hao ni Shayo, mlinzi wa shule, Hamis Chacha (28) na Makamu Mkuu wa shule hiyo, Labani Nabiswa(37).

Shauri hilo lililo mbele ya Hakimu Mkaazi, Julieth Mawole, lilitajwa kwa mara ya kwanza Novemba 11 mwaka jana.

Baadhi ya mahabusu na washitakiwa wa shauri hilo wameelezea kushtushwa na mwenendo wa Shayo kutofungwa pingu kama ilivyo kwao, kila wanapoingizwa na kutoka mahakamani hapo.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Koka Moita amesema uamuzi wa kumfunga pingu mtuhumiwa unatokana na sababu tofauti na kwamba si kosa anapotokea asiyefungwa pingu.

Amesema miongoni mwa sababu inayotumiwa na polisi kumfunga pingu mtuhumiwa ni ikiwa anathibitika kuwa ni mkorofi.

“Kama mtuhumiwa ni mkorofi na unaona kabisa kuna dalili za kutoroka, hapo ndipo tunachukua hatua za kumfunga pingu, lakini si kila mtuhumiwa anaweza akafungwa pingu,”amesema.

Pia Koka amesema kuna watuhumiwa ama washitakiwa ambao hawapaswi kufungwa pingu, wakiwamo watoto wadogo na wenye umri mkubwa au wazee.

Kwa hali, amesema mshitakiwa Shayo yupo kwenye kundi la wazee akiwa na umri wa miaka 63, hivyo anastahili ‘msamaha’ wa kutofungwa pingu.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa Novemba 11 mwaka jana alipofikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo, Shayo alikuwa  amefungwa pingu kama ilivyokuwa kwa washitakiwa wenzake.

Pia hatua hiyo (kumfunga pingu) ilijirudia mara kwa mara walipofikishwa mahakamani hapo, lakini alianza kuonekana pasipo kufungwa pingu kuanzia Januari 19, mwaka huu.

KUACHIWA WATUHUMIWA NANE

Kutoonekana kwa watuhumiwa nane wa mauaji hayo, ulizua minong’ono kwa baadhi ya wakazi wa mjini Moshi, ikidaiwa miongoni mwao walitoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Lakini Kaimu Kamanda Koka amekanusha madai ya kutoweka kwa watuhumiwa hao na kusema waliachwa huru baada ya kukosekana ushahidi wa kuwafikisha mahakamani.

Tangu kuanza kwa upepelezi wa tukio hilo, polisi haijawahi kuyataja majina ya watuhumiwa nane walioachiwa huru baada ya kukosekana kwa ushahidi.

Wakati akitangazwa kukamatwa kwao, Kaimu Kamanda Koka aliwataja miongoni mwao kwa nafasi (nyadhifa) zao kuwa ni daktari wa Mawezi, polisi wa Himo, Mama lishe wa Himo na mlinzi wa kimasai wa Himo,

Washitakiwa watatu wanaoendelea na shauri hilo mahakamani, walisomewa shitaka lao na mawakili wa Serikali, Kassim Nassir akisaidiana na Faygrace Sadallah huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Elikunda Kipoko.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao wanadaiwa kuwa  Novemba 6 mwaka jana, kwa pamoja  walimuua Humprey Makundi kwa kukusudia.

Hata hivyo washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Kaimu Kamanda Koka ameliambia JAMHURI kuwa, baada ya uchunguzi wa kina kuhusiana na mauaji hayo, hapakuwa na ushahidi dhidi ya watuhumiwa nane kati ya 11, hivyo jeshi hilo halikuwa na sababu ya kuendelea kuwashikilia.

ILIVYOKUWA

Novemba 12, mwili wa marehemu ulizikwa na manispaa ya Moshi kwenye makaburi ya Karanga bila kutolewa kwa muda wa watu ama ndugu kwenda  kuutambua.

Ndugu  wa marehemu wakiongozwa na baba mzazi, Jackson Makundi waligundua kuwa mwili uliozikwa katika makaburi hayo ulikuwa wa mwanaye, hivyo kuomba kibali cha mahakama kuufukua kwa uchunguzi.

Novemba 17 mwaka jana , Mahakama ya Hakimu Mkaazi ya Moshi ilitoa  kibali cha kuufukua mwili huo.

Mwili huo  ulifanyiwa uchunguzi wa kitabibu  na madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC na kushuhudiwa na baba wa marehemu.

Ikabainika kuwa marehemu alikatwa na kitu chenye ncha kali kiunoni,mgongoni,kwenye mapaja na mbavu mbili zilivunjika.

Baba mzazi huyo akasema kutokana na majibu ya uchunguzi, mwanaye aliuawa na akaviomba vyombo vya dola kuchunguzi na kuwasaka wahusika wa mauaji hayo.

Mwili wa marehemu Humphrey  ulizikwa Desemba 2 mwaka jana nyumbani kwao katika kijiji cha Komakundi,Moshi Vijijini.

 MWISHO.

5224 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!