Wiki iliyopita baadhi ya wamiliki wa viwanda vya kuzalisha saruji wamekaririwa na vyombo vya habari wakidai kuwa wanataka saruji kutoka nje ya nchi izuiliwe kuingia hapa nchini. Wanajenga hoja kuwa saruji kutoka nje itaua viwanda vya ndani.

Wanasema gharama za uzalishaji ni kubwa, na wanaajiri watu wengi hivyo uingizaji wa saruji kutoka nje ya nchi utawaharibia soko na hivyo kupunguza uzalishaji na hatimaye kiwe kifo cha viwanda vya ndani.

 

Taarifa tulizonazo zinaeleza kuwa wenye viwanda hawa wameanza uzengezi. Wanapitapita kwa wabunge. Wanawashawishi waanzishe hoja ya kuzuia saruji ya kutoka nje ya nchi isiruhusiwe kuingia nchini. Hoja hii imetufanya tuchunguze mambo mengi.

 

Wakati wazalishaji wa saruji wakilalamika, katika mwaka wa fedha uliopita wamepata faida ya wastani wa Sh bilioni 62 kwa mwaka. Fedha hizi ni nyingi. Shilingi bilioni 62 ni sawa na bajeti ya wizara mbili kwa wizara ambazo si kubwa.

 

Kama hiyo haitoshi, tumekumbuka maneno ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa, aliyesema katika nchi hii mfuko wa saruji unaweza kuuzwa kwa wastani wa Sh 5,000. Tumejaribu kufuatilia kwa kina tukaona inawezekana.

 

Kwa saruji inayozalishwa hapa nchini, tumebaini kuwa gharama ya kuzalisha mfuko mmoja ni karibu Sh 6,400. Kiasi hiki kinajumuisha gharama zote ikiwamo kodi. Kwa bahati mbaya, wenye viwanda wamekuwa wakiidanganya Serikali kuwa gharama ya kuzalisha mfuko mmoja wa saruji ni karibu Sh 12,000.

 

Kabla ya Serikali kuruhusu uuzaji wa Saruji kutoka nje ya nchi, mfuko mmoja wa saruji ulipanda bei hadi Sh 18,000 katika jiji la Dar es Salaam, mikoani uliuzwa hadi Sh 25,000. Baada ya saruji kutoka nje ya nchi kuruhusiwa, bei imeshuka hadi Sh 14,000.

 

Tumechunguza gharama za saruji kutoka nje ya nchi kuwa mfuko mmoja wa saruji hadi unafika katika bandari ya Dar es Salaam unakuwa sawa na dola 3 au Sh 4,800. Kodi ndizo zinazopandisha bei ya saruji kutoka nje kufikia Sh 11,000.

 

Kwa maana nyingine, kodi zikiwa za kiungwana wafanyabiashara bado wanaweza kupata faida. Hiyo faida ya Sh bilioni 62 waliyopata, inadhirisha kuwa pamoja na saruji kutoka nje ya nchi kuwapo nchini hawapati hasara, isipokuwa wana uchu wa faida ya kutisha.

 

Tunasema, kwa nia ya kuwatia adabu wafanyabiashara wachumia tumbo, utaratibu wa saruji kutoka nje ya nchi uendelee sambamba na uzalishaji wa ndani. Pia Serikali iangalie uwezekeno wa kupunguza kodi watu wajenge nyumba za maana. Tunasema tusiruhusu mtego wa kuzuia saruji ya nje kunufaisha wachumia tumbo wa hapa ndani.

 

1529 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!