Serikali ikate mzizi wa fitna Loliondo

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuendelea na ziara yake mkoani Arusha, baada ya kuikatiza kutokana na majukumu mengine ya kitaifa.

Mkoa wa Arusha, kama ilivyo mikoa mingine nchini, ina rasilimali muhimu kwa ajili ya uchumi wa Taifa letu. Ukiacha kilimo, Mkoa wa Arusha unaiingizia Serikali mapato mengi ya fedha za kigeni kutokana na utalii.

Tunampongeza Waziri Mkuu kwa kuchukua hatua muhimu ya kupiga marufuku uingizaji mifugo ndani ya Kreta. Hapa ikumbukwe kuwa idadi ya watalii wanaozuru eneo hilo imepungua, baada ya kubaini raha inayopatikana Ngorongoro ambayo ni ya wanyama na mandhari nzuri inatoweka kwa kasi kutokana na uharibifu wa mazingira na wingi wa mifugo.

Tunaamini Waziri Mkuu Majaliwa hataishia hapo, bali atafukunyua na kupata ukweli kuhusu Baraza la Wafugaji ambalo linatuhumiwa kufuja mabilioni kwa mabilioni ya shilingi zinazotengwa kwa ajili ya kuwasaidia wana-Ngorongoro.

Pia, tunatumaini Waziri Mkuu atatumia fursa hii kutoa tiba mujarabu ya utitiri wa NGOs zilizoko Ngorongoro kwa maslahi ya wachache badala ya kuwakomboa wananchi kimaisha.

Katika ziara hii, Waziri Mkuu, akiwa mtendaji mkuu wa shughuli za Serikali, atoe msimamo madhubuti utakaosaidia kuliokoa Pori Tengefu la Loliondo na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA). Njia sahihi ni kuhakikisha kunatengwa eneo la uhifadhi na eneo kwa ajili ya shughuli za wananchi.

Tunatambua kuwa uamuzi huo ni mgumu kutokana na kujipanga kwa wanasiasa, NGOs, wawekezaji wenye kujinufaisha na Loliondo pamoja na watu ambao maisha yao yanastawi kutokana na kudumu kwa mgogoro wa Loliondo.

Waziri Mkuu atoe uamuzi wenye kulinda maslahi mapana ya nchi, kwani rasilimali zilizoko Loliondo, Ngorongoro na Serengeti ni za Watanzania wote. Zinapaswa kuwanufaisha Watanzania wote kama ilivyo kwa gesi, samaki, almasi, dhahabu, misitu na rasilimali nyingine. 

Tunatambua kuwapo nguvu kubwa za ushawishi zenye mlengo wa kumfanya Waziri Mkuu asiweze kuchukua uamuzi wenye manufaa kwa nchi. Tunaamini vyombo vinavyohusika vitampa taarifa zenye kumwezesha kutoa uamuzi sahihi.

Ahakikishe nguvu za watu wa ndani wanaoshirikiana na vibaraka wa nje kuiyumbisha Loliondo isitawalike zinafikia tamati. Wananchi wanahitaji amani ili waweze kushiriki kuboresha maisha yao na ya nchi kwa jumla. 

Tunakutakia kila la heri katika ‘mtihani’ huu wa Loliondo. Wakati umefika sasa wa kuona suluhu ya kudumu inapatikana katika eneo hili.

1142 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!

Comments

comments

Show Buttons
Hide Buttons