Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limekamilisha mkutano wake wa bajeti wiki iliyopita. Ukiondoa mjadala wa bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, masuala mengine kadhaa yalijitokeza bungeni.

Mojawapo ya mambo hayo ni serikali kuwasilisha mabadiliko ya sheria ya takwimu, marekebisho yaliyolenga vifungu vya sheria hiyo kuhusu haki ya kuchapisha au kutoa taarifa za takwimu kwa umma.

Mabadiliko hayo yalifanywa kupitia Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, Namba 3 wa Mwaka 2019, uliowasilishwa kwa hati ya dharura.

Katika uwasilishaji wa marekebisho hayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi, alisema pamoja na mambo mengine, mapendekezo husika yamekusudia kuanzisha kamati ya kitaalamu (Technical Committee) ambayo jukumu lake litakuwa kupokea na kujadili malalamiko yanayotokana na wadau kuhusu usahihi wa takwimu zilizotolewa kwa umma.

AG katika ufafanuzi wake wa marekebisho hayo alisema imependekezwa kufutwa kwa vifungu vya 24A na 24B na kuviandika upya, pia kuongeza vifungu vipya vya 24C, 24D, 24E na 24F kwa lengo la kuweka utaratibu wa kutoa matokeo ya takwimu zinazotofautiana na takwimu rasmi zilizotolewa na serikali.

Kwa mujibu wa AG, marekebisho hayo yanatoa fursa kwa mtu yeyote kutoa takwimu zinazotofautiana na zilizotolewa na serikali iwapo atakuwa amezingatia misingi ya kitakwimu iliyowekwa katika miongozo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa inayosimamia utoaji wa takwimu.

Lakini jambo jingine kubwa kwenye suala hilo ni marekebisho ya kufutwa kwa kifungu cha 37 (4) kilichokuwa kinatoa adhabu kwa mtu anayetoa taarifa za takwimu bila kupata kibali cha Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

JAMHURI tumeyapokea kwa mikono miwili marekebisho haya. Hata hivyo, ni busara zaidi tukakumbushana masuala kadhaa muhimu juu ya namna baadhi ya maoni yenye mantiki, kwa nyakati fulani, yanavyopuuzwa.

Itakumbukwa kuwa wadau mbalimbali walipata kuwasilisha maoni yao kuhusu muswada wa sheria hii ya takwimu ulipokuwa ukiwasilishwa bungeni kwa ajili ya mjadala. Kati ya maoni yao, wadau hao hasa kutoka katika taasisi binafsi, yakiwamo baadhi ya mashirika yasiyo ya serikali (NGOs) waliweka bayana matundu katika mapendekezo yaliyokuwa yamekusudiwa kutoka serikalini, lakini hata hivyo walipuuzwa.

Matokeo yake, leo hii serikali inarejea maoni yale yale iliyoyapuuza. Je, awali maoni yale yangesikilizwa na kufanyiwa kazi kungekuwa na madhara gani kwa taifa? Ni wakati muafaka sasa kujifunza namna ya kusikiliza maoni ya watu mbalimbali kwa kigezo cha ubora na si vinginevyo, halafu fursa za kuwasilisha muswada kwa hati ya dharura zitumike katika mantiki halisi ya dharura. Tujisahihishe.

3200 Total Views 21 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!