*Asema CCM ikifanya makosa, nchi itayumba

Na Angela Kiwia, Dodoma

 

Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee wa Kasi na Viwango, na Waziri wa sasa wa Uchukuzi, Samuel Sitta, ameta ja sifa nne za mtu anayefaa kuwa rais wa nchi, huku akidai yeye anazo na za ziada zinazomfanya ajione anatosha kuwa Rais wa Tanzania wa Awamu ya Tano.
  Katika mahojiano na Gazeti JAMHURI yaliyofanyika mjini hapa wiki iliyopita, Sitta anataja sifa hizo kuwa ni pamoja na uadilifu, uaminifu, uwezo wa kuamua mambo na ujasiri wa kutenda.
  “Namuomba Mwenyezi Mungu atuepushe na mgombea urais anayekwenda kujitafutia utajiri binafsi Ikulu,” anasema Sitta kwa kuchagua maneno katika mahojiano hayo.
  Anasema; “Iwapo chama changu CCM kitateua mgombea ambaye hana sifa hizo, kitakuwa kimefanya kosa kubwa. Na kuanzia hapo tutarajie maandamano yasiyokoma nchi nzima. Na mtu huyo hatamaliza muda wake madarakani."
  Kutokana na hali hiyo, Sitta anasema ni imani yake kuwa CCM haitafanya kosa hilo.


“Mimi ninazo sifa hizo na za ziada, nimefanya kazi kwa uaminifu mkubwa awamu zote nne, sifa ambayo ni adhimu kwa baadhi ya watu,” anasema Sitta na kuongeza; “Hebu tusubiri muda ufike.”
  Akichambua sifa moja baada ya nyingine, Sitta anasema kwamba umefika wakati nchi kuwa na viongozi waadilifu hasa Rais ambaye hatakuwa tayari kuhujumu nchi huku akitumia kundi la watu aweze kuingia madarakani.
  Sitta anasema haiwezekani mtu akawatumia watu kwa kuanza kuwahonga na wakati huo huo ni mwanasiasa ambaye anamiliki ukwasi mkubwa huku akitajwa kuwa bilionea.
  “Hii inadhihirisha wazi kuwa alitumia nafasi yake aliyopatiwa na wananchi kuunda vijikampuni vya siri ili kuweza kujiongezea kipato, jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa Taifa na watu wake,” anasema.
  Kuhusu uaminifu, Sitta anasema kwamba nchi inahitaji Rais atakayeweza kuwaunganisha Watanzania kutokana na kuwapo kwa matukio mengi ambayo yamesababisha kupunguza imani kwa Serikali iliyopo madarakani.
  “Rais huyo atapaswa kuwa tayari kuusema ukweli, ikiwa ni pamoja na kukiri mapungufu (upungufu) pale yanapojitokeza ambapo atatakiwa kutatua matatizo yaliyopo bila hofu,” anasema Sitta.


  Anasema Serikali imekuwa na watu ambao wana tabia ya kuwachukulia wananchi juu juu kwa kudhani hakuna jambo lolote wanalolijua huku wakiwalaghai, jambo ambalo si sahihi katika karne ya sasa.  
  Anaeleza kuwa ni lazima Rais awe na uaminifu wa kiwango cha kurejesha imani ya Watanzania.
  “Awe Rais ambaye anafahamu mfumo wa Serikali na nchi na jamii kwa ujumla. Rais atakayeingilia kati mambo mbalimbali katika kutibu madhaifu yaliyojitokeza,” anasema Sitta na kuongeza: “Ni vyema akawa na uzoefu katika mfumo wa uongozi ili uweze kumsaidia katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku na kutokana na uzoefu huo ataweza kukabiliana na jambo lolote linaloweza kujitokeza.”
  Kuhusu uwezo wa kuamua; Sitta anasema ni muhumu zaidi kuwa na kiongozi mwenye uwezo mkubwa wa kufanya uamuzi wenye kuhimili joto la siasa litakalojitokeza wakati huo na kutenda kazi ipasavyo.


  “Ukiangalia kwa umakini na uzoefu, utaweza kuona ya kuwa Rais ajaye atakumbana na wakati mgumu zaidi kuliko wale wote waliomtangulia. Hii yote ni kutokana na nchi mahali ilipo na changamoto zilizopo kwa Watanzania. Ipo chuki kubwa na ya waziwazi kati ya walio nacho na wasio nacho, hili ni jambo la hatari kwa nchi,” anasema.
  Anasema kwamba Rais kama kiongozi wa nchi, hana budi kuwa na uwezo wa kuamua na mwepesi kufanya uamuzi huo kuweka mambo sawa huku akisisitiza kuwa Watanzania wa sasa ni waelewa na hawako tayari kuona wakiongozwa na mtu ambaye hatakuwa tayari kutimiza wajibu wake ipasavyo.
  Kuhusu ujasiri; Sitta anasema kwamba kila binadamu ana ujasiri, lakini ule wa urais ni wa kuongoza na kusimamia nchi kama kiongozi mkuu wa nchi.
  “Kusigana kunakotokea kwa jamii iliyopo sasa ni mfano mzuri katika uongozi tunaouhitaji kipindi kijacho. Tunahitaji kiongozi jasiri na mwenye maamuzi (uamuzi),” anasema Sitta.
  Anasema kwamba katika kipindi kifupi, Taifa limeshuhudia matamko ya mara kwa mara ya viongozi wa dini, jambo ambalo si la kupuuzwa kukabiliana nayo katika kulinda amani ya nchi na hali hiyo huwa ni changamoto kwa Rais.
  “Rais jasiri ataweza kuonesha msimamo wa nchi katika masuala ya kisiasa. Ni lazima iwepo sheria ya kutenganisha siasa na biashara, maana jambo hili limepigiwa kelele kwa muda mrefu sasa, lakini halijaweza kutafutiwa ufumbuzi,” anasema.
  “Vita ya rushwa haiwezi katu kuwa na mafanikio kama hakuna sheria ya kutenganisha biashara na uongozi. Kumekuwapo na juhudi za kuhakikisha sheria hii inatungwa ila hakuna lolote lililotokea. Wapo walioleta hoja, lakini zimeishia hewani. Iwapo mfanyabiashara ataamua kuingia katika siasa atatakiwa kuweka wazi mali zake, madeni na kadhalika,” anasema.
  Anaeleza kuwa yeye binafsi anatambua kwa hali ilivyo wapo watu wenye vigezo hivyo alivyovitaja na CCM haina upungufu wa watu ambao baadhi yao tayari wametangaza nia ya kugombea nafasi ya urais na wengine bado.
  Anasema yeye binafsi anaowafahamu kuwa wanafaa kuwania nafasi hiyo na wenye vigezo hivyo ni watu watano ambao hakuwa tayari kutaja majina yao kwa wakati huu.
Anabainisha kuwa kupitia mikakati yake anaamini CCM itadhibiti vitendo vya rushwa maana tayari baadhi ya watu wameweza kutumia kiasi kikubwa cha fedha kuwania madaraka hayo makubwa na kwamba jambo hilo halikubaliki na watu hao tayari wamepoteza sifa ya kuwania nafasi hiyo.
  “Naamini Kamati Kuu itatupa watu watatu bora, hivyo tutajitahidi tupate mtu ambaye atafanana na Katiba yetu ya Chama Cha Mapinduzi, ambaye hatumii na hatotumia nafasi yake kujinufaisha.


  “Uongozi ni dhamana, ataitumikia kama ambavyo kiapo chetu cha CCM kinavyosema. Lakini iwapo Mkutano Mkuu utaweza kumpitisha mtu ambaye ni kinyume na hapo nataraji kuona nchi yangu ikikumbwa na maandamano yasiyokwisha, hivyo kumuondoa Rais madarakani”.
  Kuhusu Tume ya Uchunguzi aliyoiunda kufuatia kumsimamisha Kaimu Mkurugenzi wa Bandari, Mhandisi Madeni Kipande, Sitta anasema Kamati hiyo iliomba kuongeweza muda wa wiki moja ya ziada kuweza kukamilisha kazi hiyo na muda huo ulimalizika Machi 20, 2015 na baada ya kukabidhiwa ripoti anatarajia kukutana na wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Bandari kujadili Ripoti ya Kamati.


  “Taarifa italetwa hapa Dodoma, Ijumaa (iliyopita) na nitakutana nao waweze kunikabidhi. Inawezekana tayari wamefika, ila hatujawasiliana. Nikishapata ripoti hiyo nitasubiri Bunge limalizike ndipo nitarudi Dar es Salaam na kufanya mchakato wa kukutana na Bodi ili tuweze kuangalia kwa pamoja yaliyoletwa na Kamati tuwe na msimamo mmoja,” anasema.
 Kadhalika, kwa upande wa uamuzi wake wa kuweka zuio la mabehewa ya TRL ikiwa ni pamoja na Ripoti ya Tume ya Uchunguzi aliyoiunda kutokana na kudaiwa kuwapo kwa ufisadi katika ununuzi wa mabehewa hayo, Sitta anasema angali anafuatilia.
  “Mimi nilichokifanya ni kusimamisha uletwaji wa mabehewa hayo kutokana na mtindo wa kuyaleta kwa mafungu mafungu, kwa mtazamo wa juju juu yanaonekana kuwa na kasoro. Kwa muda wa miezi miwili mabehewa 30 tayari yamepata ajali hilo si suala la kupuuza,” anasema Sitta, akisubiri Ripoti ya Kamati iliyoundwa na mtangulizi wake, Dk. Harrison Mwakyembe.


  Amesema tayari Bodi ya TRL imeshakutana na Kamati ya Uchunguzi na ametaarifiwa kuwa ripoti hiyo ipo tayari na ni ndefu.
  “Nayo nasubiri kukabidhiwa ripoti hizo ili niweze kuona yaliyobainika ikiwa ni pamoja na kukutana na Bodi husika na kuweka msimamo na kauli moja thabiti,” anasema.

By Jamhuri