Mwishoni mwa wiki zimetokea habari za kusikitisha. Mmiliki wa Kampuni ya Home Shopping Centre, Said Mohamed Saad, amemwagiwa tindikali usoni na sasa amepelekwa kwenye matibabu nchini Afrika Kusini.

Saad alikumbwa na mkasa huo saa 2:00 usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita katika eneo la Msasani City Mall, jirani na ofisi za Ubalozi wa Marekani na Kituo cha Polisi Oysterbay, jijini Dar es Salaam. Chanzo hakijaelezwa, lakini kwa vurugu zilizokuwapo kuna kila dalili kuwa hali hii inahusiana na biashara.

 

Wapo wafanyabiashara waliokuwa wakilalamika kuwa Kampuni ya Home Shopping Centre imeua kampuni nyingine katika biashara ya uwakala wa kusafirisha mizigo ndani na nje ya nchi. Malalamiko yamekuwa makubwa mno.

 

Ukiachana na hilo, sisi tunauona huu ni mwendelezo wa Taifa letu pendwa la Tanzania kupotea njia. Tunakumbuka Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Absalom Kibanda, alivyovamiwa na watu wasiofahamika, akapigwa, akatobolewa jicho, akakatwa kidole na kila aina ya unyama.

 

Mwaka uliopita yalitokea mauaji kadhaa kwenye mikutano ya kisiasa yakiwamo ya mwandishi Daudi Mwangosi, huko Nyololo, Iringa. Padre ameuawa huko Zanzibar na mwingine amepigwa risasi akaponea chupuchupu.

 

Katika Kanisa la Olesiti, Arusha, bomu limelipuliwa, mkutano wa Chadema Arusha nako limerushwa bomu, Dk. Stephen Ulimboka alitekwa akateswa kinyama kabisa na matukio mengi ya ajabu. Ukiangalia mwelekeo kuna kila dalili kuwa Taifa letu linapotea njia.

 

Wakati Rais Jakaya Kikwete anaingia madarakani, tatizo kubwa la nchi hii lilikuwa ni ujambazi. Moja ya ahadi zake ilikuwa ni kukomesha ujambazi na wizi katika mabenki. Hakika tunasema kwa kiwango kikubwa Rais Kikwete amefanikiwa katika hili.

 

Hata hivyo, kwa bahati mbaya katika miaka hii miwili tuliyomo, umeibuka uhalifu wa ajabu. Watu hawataki tena kutii sheria. Watu wamepoteza utu. Wananchi hawana tena woga, wanaamua kutenda wanaloona linawafaa. Wanaumizana.

 

Sisi tunasema hali ilipofikia ni mbaya. Tulidhani mambo haya yapo kwenye siasa. Tumeshuhudia hujuma katika dini, siasa, uandishi wa habari na sasa kwenye biashara. Hakika hakuna aliye salama. Nchi yetu imepoteza mwelekeo kwa kiwango cha kutisha.

 

Tunaitaka Serikali iwasake wote wanaoendesha uharamia huu na kuwafikisha mbele ya sheria. Kama iliweza kudhibiti majambazi, tunaamini haishindwi kudhibiti matukio haya ya kinyama yanayofanywa na kundi dogo, lakini lenye madhara makubwa kwenye amani ya nchi yetu.

1401 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!