Kuna wamachinga wanaovuna mamilioni, walipe kodi stahiki

Hakuna binadamu anayependa kulipa kodi. Lakini Serikali haiwezi kujiendesha bila kodi, hivyo ni wajibu wa kila mtu mwenye sifa za kulipa kodi, kufanya hivyo.

Hata hivyo, mara nyingi katika mataifa yaliyoendelea, wananchi wamekuwa wepesi wa kulipa kodi tofati kabisa na nchi kama Tanzania.

 

Yapo mambo mengi yanayosababisha hali hiyo. Mosi, ni ukweli kuwa wananchi wengi huwa hawana elimu ya kutosha juu ya faida za ulipaji kodi.

 

Pili, ni ukweli ulio wazi kuwa wananchi wengi wanakatishwa tamaa na matumizi mabaya ya kodi wanazolipa. Wamekuwa hawafurahishwi na matumizi ya kodi wanayolipa katika kuwaletea maendeleo.

 

Serikali yetu imekuwa butu kwenye ubunifu wa kodi. Badala yake imejiegemeza kwa watumishi wa sekta rasmi, hasa serikalini na katika mashirika ya umma na kuacha maeneo muhimu ambayo yangeweza kuongeza mapato.

 

Matokeo ya uamuzi huo ndiyo haya tunayoshuhudia kila mwaka kodi zikipandishwa kwenye vinywaji, sigara, mafuta, huduma za simu na kadhalika.

 

Masikini wenye kipato kidogo ambao hawana namna ya kukwepa kodi, wanakamuliwa kweli kweli. Wabunge wamekuwa wakiishauri Serikali ipunguze misamaha ya kodi, lakini hawasikilizwi. Misamaha ya kodi ni mingi mno.

 

Hivi sasa mfanyakazi anayelipwa mshahara wa Sh 200,000 anakatwa kodi kubwa, lakini mfanyabiashara wa Kariakoo anayeingiza mamilioni ya shilingi kila siku, halipi kwa kigezo kuwa ni mmachinga!

 

Kichekesho kingine cha wachumi wetu ni kile cha kufuta kodi zote kwenye bajaji na pikipiki za kawaida, kwa kigezo kuwa uamuzi huo umelenga kuwasaidia vijana waliojiajiri! Huko ni kujidanganya kwa sababu wenye vyombo hivyo wengi ni matajiri wakubwa.

 

Tunaishauri Serikali iache kujiendesha kwa mazoea. Igeukie upande wa pili huu wa wanaojiita wafanyabiashara wadogo iweze kukusanya kodi. Wamachinga wengi walioko Kariakoo na maeneo kama hayo, wanauza bidhaa za matajiri. Wamachinga wanatumiwa kama mwanya wa kukwepa kodi.

 

Endapo wananchi wengi watalipa kodi, ni wazi kuwa hata kiwango cha kodi kitakachotozwa kitapungua sana, na hivyo wananchi wengi watakuwa na ari ya kujitokeza kulipa. Kwa mwenendo huu wa kukamua watu wachache na kuwaacha wengi wakitamba bila kulipa kodi, ni wazi kwamba Serikali itaendelea kuhemea.

 

Mfumo wa kutumia mashine za malipo za kielektroniki unapaswa kutekelezwa kisheria. Mwananchi asidai risiti, bali anapokutwa hana risiti, akamatwe na ikiwezekana mali yake itaifishwe. Kwa kufanya hivyo kila mwananchi atadai risiti na kupewa.

 

Mashine ya kielektroniki zitumike hadi kwenye baa na migahawa ambako kwa sasa mapato yake hayajulikani, vizuri licha ya ukweli kwamba pombe na sigara vinaongoza katika kuiingizia fedha nyingi Serikali.

 

Tunatoa wito kwa Serikali kupanua wigo wa kodi – watu wengi zaidi walipe – badala ya utaratibu wa sasa wa watu wachache kulipa ziadi.