Katika toleo la leo tumechapisha habari za mgogoro unaoendelea kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba. Mgogoro huu ni mkubwa kwa kiwango ambacho wananchi, watendaji, viongozi, wafanyabiashara na hata wanasiasa wamefika mahala hawaaminiani. Kila kona ya Bukoba kuna mazungumzo kwenye makundi.

Uchunguzi wa Gazeti JAMHURI uliowezeshwa na Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), umebaini kuwapo kwa hofu kubwa juu ya hatima ya mgogoro katika Manispaa ya Bukoba. Wakati Mkurugenzi mpya wa Manispaa, Limbakisye Shimwela, akisema wananchi wasiwe na hofu nyaraka ziko salama, baadhi ya madiwani akiwamo Samuel Luhangisa wanasema nyaraka zimeibwa.

 

Nyaraka zinazodaiwa kuibwa ni stakabadhi na vitabu mbalimbali vinavyohusu mradi wa viwanja 5,000 katika Manispaa ya Bukoba, mikataba ya mikopo kutoka UTT na Benki ya Rasilimali inayodaiwa kukopwa kufanyia upembuzi yakinifu wa kujenga soko na fidia ya viwanja, ubinafsishaji wa eneo la kuoshea magari na mengine mengi. Hofu hii imelazimisha wananchi kugeuka walinzi wa ofisi za halmashauri kuangalia nani anaingia na nani anatoka humo muda wote.

 

Shimwela amesema kuwa tayari anayo barua ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ikimtaarifu juu ya ukaguzi wa dharura utakaofanyika wakati wowote kuanzia sasa, na kumpa maelekezo kuwa matokeo ya ukaguzi yawasilishwe kwenye Baraza la Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba. Ina maana taarifa hii ikiwasilishwa itajadiliwa.

 

Mjadala sisi hatujui utachukua mkondo upi. Hata hivyo, ukichukulia kauli ya Diwani wa Kahororo kuwa madiwani wanane wanaompinga Meya Anatory Amani wanaweza kupiga kura katika kikao hicho na kwamba baada ya ukaguzi CAG apeleke taarifa yake kwa Waziri Mkuu, vinginevyo fimbo zitatembea, basi tunasema aina ya mgogoro uliopo Bukoba ni ya hatari.

 

Tunasema hadi sasa, sisi kama Gazeti JAMHURI hatuna uhakika nani ana makosa. Hatujui kama mbunge anayetuhumiwa kuhonga madiwani na watendaji ndiye mwenye makosa, na wala hatujui meya anayetuhumiwa kumhonga Mkuu wa Mkoa, Kanali Fabian Massawe, Katibu wa CCM Mkoa, Everin Mushi na baadhi ya madiwani iwapo ndiye mwenye makosa na iwapo wamehonga kweli.

 

Ukaguzi wa CAG utasaidia kukata mzizi wa fitina. Zitajulikana mbichi na mbivu. Ikiwa Kagasheki ndiye mwenye makosa, taarifa ya uchunguzi ikibainisha hivyo basi aadhibiwe bila huruma. Ikithibitika ni Meya Amani naye aadhibiwe pia. Kubwa tunalosema sisi ni hii hali ya sintofahamu. Vikao vya halmashauri kwa sasa havifanyiki.

 

Tangu Mei 2013, hakuna kikao kilichofanyika kufanya uamuzi katika Manispaa ya Bukoba. Huu si mkondo sahihi. Tunasema CAG afike Bukoba haraka, akague na kutoa taarifa haraka kisha mgogoro upatiwe ufumbuzi. Tunawaasa pia wakazi wa Bukoba kuwa mgogoro huu hauna tija. Uamuzi utakaotolewa, basi ukubaliwe na kuhitimisha mgogoro huu kisha shughuli za maendeleo zianze upya.

 

Kuiruhusu Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kuendelea na mgogoro huu bila ukomo, ni kujenga mazingira ya kudidimiza maendeleo si ya Bukoba tu, bali Mkoa wote wa Kagera, kwani Bukoba ndiyo makao makuu ya mkoa.

 

Katika hili, tunaamini busara itachukua mkondo wake na viongozi wanaopingana ndani ya nafsi zao wapime uzito na wako sahihi kwa kiwango gani kwa msimamo walionao, ili tunasema kwa maslahi ya umma viongozi wawe nguzo ya kumaliza mgogoro huu.

1400 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!