‘TASAF ni malaika aliyetumwa na Mungu’

MLELE

Na Walter Mguluchuma

Ruzuku inayotolewa na serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imewawezesha wanakaya maskini katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlele mkoani Katavi kujikwamua kimaisha kwa kuanzisha shughuli za kiuchumi.

Kwa miaka saba sasa TASAF imekuwa mstari wa mbele katika kuboresha maisha ya wananchi maskini na kuwawezesha kushiriki katika ujenzi wa taifa.

JAMHURI limezungumza na baadhi ya wanufaika wa awamu ya pili ya mpango wa kuzinusuru kaya maskini (PSSN) unaoendelea ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mlele.

Mmoja wa wanufaika wa mpango huo, Stephano Abel, mkazi wa Inyonga wilayani humo, anakumbuka maisha magumu ambayo amewahi kuyapitia akisema: “Hata kupata mlo mmoja tu kwa siku ilikuwa ni bahati kubwa.

“Sasa hapo sijazungumzia mzigo mkubwa niliokuwa nao wa kuwalea watoto wangu wawili. Kwa kweli nimewalea kwa shida sana na kwa miaka mingi.”

Anasema kabla ya kujiunga na TASAF jamii inayomzunguka haikuwa tayari hata kumkopesha chumvi kwa kufahamu kwamba isingekuwa rahisi kwake kulipa kutokana na umaskini uliokuwa umeing’ang’ania familia yake.

“Nikaanza kujishughulisha na ufugaji na kilimo ili kuhakikisha walau watoto wanapata mahitaji  muhimu ikiwamo kwenda shule.

“Hali ilikuwa ni ngumu sana hata kuifikiria au kuikumbuka kunanitia uchungu. Mungu si Athumani, mwaka 2015 nikabahatika kuorodheshwa katika mpango wa Tasaf,” anasema Abel.

Naam! Nuru na matumaini mapya yakawasili  katika kaya ya Mtanzania huyu kwani kwa mara ya kwanza maishani mwake akaweka mfukoni mwake Sh 32,000 kama ruzuku kutoka TASAF!

Ruzuku hiyo ya kila mwezi ilikuwa ni nyota ya jaha kwa kaya hii na kwa hakika ndicho kiini cha kumkwamua Abel na familia yake kimaisha.

“Nilipopata fedha hizo nikaanza kufanya biashara ndogondogo kwa juhudi kubwa, usiku na mchana. Kipato kikawa kinaongezeka siku hadi siku. Ninamshukuru Mungu kwa kuwa sasa ninaaminika na kukopesheka,” anasema kwa furaha inayoonekana dhahiri.

Anasema sasa hata waliokuwa wakimnyoshea kidole kumnanga kutokana na umaskini wake, wanamuiga kwa jinsi anavyojituma.

Katika kiwango cha fedha alichokuwa akikipokea, Abel alikuwa akitenga kiasi fulani cha fedha kwa matumizi ya shule kwa watoto wake; yaani madaftari, kalamu na sare za shule.

Mmoja kati ya watoto wake hao sasa ni mwanafunzi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii huko Sumbawanga mkoani Rukwa huku mwingine akiwa darasa la saba.

Mbali ya kusomesha watoto, sasa amejenga kibanda (nyumba) cha  kuishi akikiezeka kwa bati.

Abel anawataka wananchi wa Mlele na Watanzania wote kuwatafuta na kuwaorodhesha wenye sifa ya kujiunga na mfuko huo, wajiunge kwa kuwa una manufaa makubwa.

“Kwangu mimi TASAF ni sawa na malaika aliyetumwa na Mungu kuiletea familia yangu habari njema na maisha mapya. Walau sasa tunaishi kama binadamu wengine,” anasema. 

Magreth Kaswiza ni mnufaika mwingine wa TASAF aliyezungumza na JAMHURI.

Mama huyu amekuwa akipokea ruzuku ya Sh 40,000 kwa mwezi anazozielekeza katika shughuli za kilimo cha mahindi na karanga, ufugaji wa kuku na ushonaji.

“Mpango huu umebadilisha kabisa maisha yangu na kurejesha furaha ndani ya nyumba yetu. Awali hali haikuwa nzuri hata kidogo,” anasema.

Magreth amebainisha kuwa mmoja kati ya watoto wake aliowasomesha kutokana na ruzuku ya TASAF sasa yupo chuo kikuu, huku mwenyewe akiwa na uwezo wa kulima au kulimisha ekari nne za mahindi na karanga kwa ajili ya chakula na biashara.

“Kama hujawahi kupitia maisha kama niliyopitia mimi hauwezi kufahamu nini kinachofanywa na serikali kupitia TASAF. 

“Kwa kweli tumesaidiwa sana sisi tuliokuwa tukikabiliwa na umaskini wa kipato, tukikosa mahitaji muhimu na ya msingi,” anasema akitoa ombi kwa serikali kuzitoa fedha hizo kwa wakati kwa walengwa.

Akizungumzia utendaji wa Mfuko, Mratibu wa TASAF wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele, Graceanna Msemakweli, anasema maofisa huwatembelea walengwa kuona shughuli za uzalishaji mali wanazofanya na kuwashauri jinsi ya kutumia ruzuku kwa tija.

“Walengwa wetu hujishughulisha na kilimo, ufugaji na wengine hufanya biashara ndogondogo,” anasema Graceanna.

Mpango wa TASAF Mlele ulizinduliwa mwaka 2014 katika Halmashauri ya Mlele na Mpimbwe, kwa pamoja zikiwa na walengwa 2,629.

Baada ya halmashauri kugawanyika, Mlele ilibaki na vijiji vinne kati ya 28 vya awali, vilivyokuwa na walengwa 343.

Baada ya uhakiki, mpango huo sasa umesalia na walengwa 283 ambao kati ya Januari na Oktoba mwaka huu, wamelipwa ruzuku ya Sh 65,000,804.  

“Siku zote sisi huwahimiza walengwa kujiwekea akiba kwa ajili ya kuwasaidia kuwa na makazi bora na ya kudumu, na watoto wao waendelee kupata elimu hadi elimu ya juu,” anasema Graceanna.

Anasema mifano ipo, tena mingine ni ya kujivunia, kwa kuwa kuna watoto wanaosoma vyuo vikuu.

TASAF wamekuwa wakiwasaidia walengwa kwa kuwapatia elimu juu ya matumizi ya fedha ziweze kuwasaidia.

Maofisa wa taasisi hii ya serikali huwafuatilia walengwa kuona wanavyotumia fedha za ruzuku kuhakikisha zinatumika kama serikali ilivyolenga.

“Kwa kiasi kikubwa walengwa wamekuwa wakitumia fedha vizuri kwa kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi,” anasema.

Graceanna anaonyesha kusikitishwa kwake na walengwa wachache wanaodhani fedha wanazopewa ni kwa ajili ya kunywea pombe.

Hata hivyo, elimu ya matumizi bora ya ruzuku inaendelea kutolewa.