DODOMA

Na Mwandishi Wetu

Aliyewahi kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Michezo kwenye Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Leonard Thadeo na Hakimu Mfawidhi (mstaafu) wa Mahakama ya Utete, Rufiji, Ally Katembo ni miongoni mwa wajumbe watano walioteuliwa kuunda kamati ya kusimamia uchaguzi wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali nchini (SHIMIWI), unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu kwenye mkoa utakaotangazwa baadaye.

Wanakamati hao wamepitishwa mwishoni mwa wiki kwenye mkutano mkuu wa dharura wa SHIMIWI uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma, ambapo wanakamati wengine waliopitishwa kwa kura za ndiyo za wajumbe wote 98 walioshiriki ni Joyce Benjamin (mstaafu) aliyekuwa mtumishi wa umma kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, huku Mohamed Ally aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Uchukuzi na sasa ni Mkurugenzi wa Utawala kwenye Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula nchini (NFRA) na Thadeo Almas ambaye ni Mwanasheria wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Mohamed ndiye katibu wa kamati hiyo, ambapo mwenyekiti ni mwanasheria.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu (mstaafu) wa SHIMIWI, Moshi Makuka, amesema kwa mujibu wa katiba ya shirikisho hilo Ibara ya 21 inataka mwenyekiti wa kamati lazima awe na taaluma ya sheria; ambapo kwa ujumla aliyataja majukumu ya kamati hiyo kuwa ni pamoja na kushughulikia masuala yote yanayohusu uchaguzi wa shirikisho; kuandaa kanuni za uchaguzi na kuziwasilisha kwa Kamati ya Utendaji ili zipitishwe na Mkutano Mkuu; na kutoa fomu za kugombea nafasi mbalimbali.

Majukumu mengine ni kufanya usaili wa wagombea; kutangaza majina ya wagombea; kupanga tarehe ya uchaguzi kwa wakishirikiana na Kamati ya Utendaji iliyopo madarakani; kusimamia uchaguzi na kutangaza matokeo ya uchaguzi.

Mbali na uteuzi huo wa wajumbe, pia wajumbe hao wamepitia na kuboresha kanuni za uchaguzi, ambazo zinaonyesha taratibu za uchaguzi huo; kuchambua, kutangaza majina ya wangombea; wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi na wenye haki ya kupiga kura; wagombea kujieleza; wajumbe wenye haki; kupiga kura; mpangilio wa uchaguzi; kuhesabu kura; mshindi; na matokeo ya uchaguzi.

Hata hivyo, Makuka amezitaka klabu zote ambazo bado kufanya uchaguzi zihakikishe zinakamilisha zoezi hilo, ili waweze kupata nafasi ya kuingia kwenye mkutano wa uchaguzi mkuu kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi; pia wahakikishe wanachagua viongozi makini, wenye weledi, busara na ushawishi kwa viongozi mbalimbali wa ngazi za juu.

“Pia mkahikishe mnatengeneza bajeti halisia kwa ajili ya mabonanza na mashindano zikiwa na tija kwa wizara na idara za serikali, kwani itasaidia kufanya uongozi ujipange kwa ufanisi na kuweza kushiriki kila wakati bila kukosa fedha za ushiriki,” amesema Makuka.   

Naye mwenyekiti wa mkutano huo wa dharura, Ally Katembo, amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

By Jamhuri