Manungu Complex panafaa kwa ligi Morogoro

Na Mwandishi Wetu 

Baada ya miaka 23 kupita, juzi Jumamosi tuliwaona Simba wakiwa katikati ya mashamba ya miwa yaliyopo Turiani, wakimenyana na ‘wakata miwa’ Mtibwa Sugar katika dimba la Manungu Complex, kisha kutoka sare ya bila kufungana. 

Mchezo huo ulikuwa moja kati ya ile michezo migumu lakini hasa ni kutokana na hali ya uwanja wenyewe ilivyo. Lakini kwetu sisi mashabiki burudani ya soka imepatikana. Kila timu imepata ilichostahili.

Mechi kama hiyo ya Mtibwa Sugar na Simba ya Dar es Salaam iliwahi kuchezwa uwanjani hapo miaka 23 iliyopita na haikumalizika. Ikavunjika kutokana na vurugu zilizotokea siku hiyo.

Miaka 23 kwa hakika ni muda mrefu sana. Ni sawa na umri wa kijana ambaye anamaliza chuo kikuu sasa. Kwamba anazaliwa, anasoma shule ya msingi, sekondari na hatimaye chuo kikuu, Simba hawajakanyaga tena Manungu japokuwa timu inayomiliki uwanja huo ipo Ligi Kuu kwa miaka yote hiyo.

Tangu hapo maofisa waliokuwa madarakani katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zamani likijulikana kama Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) wakapiga marufuku wenye uwanja huo, Mtibwa Sugar, kuutumia kwenye mechi kubwa kama kati yao dhidi ya Simba na Yanga.

Ule mchezo uliosababisha kupigwa marufuku matumizi ya uwanja wa Manungu ulichezwa katika msimu wa 1998/99. 

Enzi hizo Mtibwa Sugar ilikuwa moto kweli kweli! Wakati huo timu ilikuwa chini ya makocha John Simkoko na msaidizi wake, Ahmed Mumba.

Wachezaji wao walikuwa ni akina Peter Manyika, Mecky Maxime, Peter Nkwera, Mao Mkami, Alphonce Modest, Simon Mhesa, Aboubakary Mkangwa, Twaha Omary, Ramadhan Ngubiagai, Shaaban Chumu, Godfrey Kalumbeta na wengineo. Kwa hakika kikosi kilisheheni mafundi.

Kinachotajwa kusababisha vurugu zile ni mashabiki wa Mtibwa Sugar kuwamwagia upupu wachezaji wa Simba. 

Baada ya hali kuwa hivyo ikatajwa kuwa kipa wa Simba, Mohamed Mwameja, ndiye aliyekuwa kinara kuhakikisha mwamuzi anamaliza mchezo huo ambao Simba tayari walishakuwa nyuma kwa mabao 3-0.

Hiki kilikuwa moja ya vituko vikubwa vya kukumbukwa. Watu walianza kulikumbuka tukio hili ilipotangazwa tu mechi ya Mtibwa Sugar na Simba kuchezewa Manungu. 

Zama hizo Mtibwa Sugar walienea sana uwanjani. Utawaambia nini wakazi wa Lukenge, Gezaulole, Stafu kubwa na mdogo, Madizini, Kidudwe, Kukwe, Kisala, Manyinga, Turiani na Morogoro na maeneo mengine mengi ya karibu?

Inatajwa kuwa hata wanafunzi wa shule zote za msingi kama Kiwandani ambayo ipo karibu na uwanja huo, kesi kwa walimu wao zilikuwa haziishi kwa sababu mtoto alikuwa yuko tayari kutoroka ili tu akaitazame Mtibwa Sugar uwanjani na akache masomo darasani.

Si kiwandani tu, bali hata wakazi wa Kidudwe, Kisala, Lusanga, Manyinga, Kilimanjaro na Kichangani walikuwa wanafika uwanjani hapo.

Mapenzi na timu yao yalikuwa ya kweli. Usishangae ukakutana na kijana wa sasa wa Mtibwa akakwambia anaipenda Mtibwa Sugar na hana ushabiki wa Simba wala Yanga.

Wakata miwa hao walishibishwa kuipenda timu yao. Hata katika pambano lao hili la Simba watu walijaa kushuhudia timu yao ikimenyana na Simba.

Baada ya Manungu Complex kuwashuhudia Simba, pia watawaalika Yanga katika uwanja huo. Hii itakuwa fursa nyingine ya mashabiki wa Mtibwa Sugar kuiona Yanga katika uwanja wao.

Hiyo ni fursa waliyoipata, kubwa wawe na nidhamu, washabikie lakini kwa utulivu ili burudani kama hizo wasizikose tena na ziwe katika kila msimu. Si leo hivi, kesho vile.

461 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons