Tuchukue tahadhari za mvua zinazoendelea kunyesha

Jumamosi ya wiki iliyopita Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa tahadhari ya matarajio ya hali mbaya ya hewa kwa siku tano.

TMA ilitoa tahadhari ya mvua kubwa kwa siku tano mfululizo kuanzia Jumamosi hadi kesho kwa maeneo machache ya mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Iringa, Tanga, Dodoma, Songwe, Mbeya, Ruvuma, Mtwara, Njombe, Lindi pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba na upo uwezekano wa kunyesha ikiwa ni ya wastani au kubwa, na athari zinazoweza kujitokeza ni baadhi ya makazi kuzungukwa na maji na kusimama kwa shughuli za kiuchumi.

Pia TMA ikatoa angalizo la upepo mkali unaofikia kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa  yanayofikia mita 2.0 katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi (mikoa ya Lindi, Mtwara, Tanga, Dar es Salaam na Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia) pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba. 

Angalizo hilo pia likataja athari zinazoweza kujitokeza kuwa ni baadhi ya makazi kuzungukwa  na maji pamoja na kusimama kwa shughuli za kiuchumi na kuathirika kwa baadhi ya shughuli za uvuvi na usafirishaji. 

Sisi Gazeti la JAMHURI pia tunawasihi wote wanaoishi katika maeneo hayo kujiandaa na kuendelea kuzingatia kuchukua tahadhari kwa sababu mvua na upepo huo ambao kimsingi ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi unaweza kusababisha vifo na athari nyingine.

Mathalani, tumepata taarifa kwamba katika siku za hivi karibuni baadhi ya wakazi wa Kata ya Kalengakelu, Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro wamekosa sehemu ya kuishi baada ya nyumba 21 na madarasa matatu ya Shule ya Msingi Kalengakule kuezuliwa na upepo na hakuna mtu aliyepoteza maisha.

Pia wakazi wa Mlimba mkoani Morogoro nao wamekutwa na athari kama hizo baada ya nyumba zaidi ya 230 kuezuliwa na upepo mkali ulioambatana na mvua na kusababisha baadhi yao kupoteza baadhi ya vitu vyao.

Huku nyumba nyingine 27 nazo zimeezuliwa na mvua iliyoambatana na upepo mkali na watu wawili wakijeruhiwa, akiwamo mtoto kujeruhiwa katika Kijiji cha Banawanu, Kata ya Udonja, Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe na kwa wakazi wa Dar es Salaam usiku wa Januari 20, mwaka huu walishuhudia mvua kubwa iliyoambatana na upepo na mingurumo ya radi ikinyesha na kusababisha umeme kukatika kwa muda mrefu katika baadhi ya maeneo.

Pamoja na mambo mengine, tunawasihi madereva wa vyombo vya moto nao kuendelea kuchukua tahadhari pindi wanapokuwa barabarani kwa sababu mvua zinazoendelea kunyesha pia zimeleta athari za kubomoa madaraja, vivuko na miundombinu mingine na wale wanaotembea kwa miguu nao pia tunawaomba wasivuke maeneo yenye maji mengi yanayopita kwa kasi kubwa.

Pia tunawaomba wananchi wote kuripoti kwa mamlaka husika matukio hatarishi yanayotokea katika maeneo yao baada ya kusababishwa na mvua kubwa au upepo mkali ili hatua stahiki ikiwamo uokoaji ziweze kuchukuliwa.