Sababu mazungumzo ya Marekani, Iran kusuasua

Na Nizar K Visram

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres alitangaza hivi karibuni kuwa Iran imechelewa kulipa mchango wake, kwa hiyo haki yake ya kupiga kura inasimamishwa. 

Mwakilishi wa Iran katika UN alieleza kuwa uchelewashaji huo umetokana na vikwazo vya Marekani. Akaongeza kuwa Iran ina akiba tosha katika benki za kigeni lakini akaunti zake zimezuiliwa na Marekani.  

Kwa mujibu wa kanuni za UN, nchi wanachama wanaochelewa kulipa mchango zaidi ya miaka miwili wanazuiliwa kupiga kura. Deni la Iran kwa UN limefikia dola za Marekani milioni 18. 

Katika akaunti yake iliyopo Korea Kusini kuna dola bilioni 7, lakini fedha hizo zinakaliwa na Marekani.

Hatua hii ya Marekani ilianza mwaka 2018 wakati aliyekuwa rais wakati huo, Donald Trump, alipojitoa kutoka mkataba wa nyuklia uliosainiwa mwaka 2015 na Marekani, Iran na mataifa makubwa ulimwenguni. 

Trump akaiwekea Iran vikwazo vya kimataifa, kitu ambacho kinaendelea kutekelezwa leo na Rais Joe Biden. 

Ikumbukwe kuwa mkataba huo (Joint Comprehensive Plan of Action – JCPOA) ulisainiwa wakati wa utawala wa rais Barrack Obama na Joe Biden akiwa makamu wake.

Hata hivyo tangu Aprili mwaka jana mazungumzo yamekuwa yakiendelea mjini Vienna (Austria) kutafuta njia ya kuufufua mkataba. 

Marekani kwa upande mmoja na Iran kwa upande wa pili zimekuwa zikilumbana, na matokeo yake mazungumzo yamekuwa yakijikokota. Baada ya kila mkutano wajumbe wamekuwa wakirudi nyumbani ili kushauriana na serikali zao. Kisha wanarudi tena na kuendelea na duru mpya. 

Kwa njia hii mpaka sasa zimefanyika duru nane za mazungumzo. Duru ya nane imeanza Januari 16, mwaka huu. Marekani inaitaka Iran ikomeshe urutubishaji wa madini ya urani kwa matumizi ya nguvu za nyuklia na Iran inaitaka Marekani itekeleze mkataba wa 2015 na ikomeshe vikwazo. 

Mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 (JCPOA) ulisainiwa na mataifa ya Marekani, Iran, Ufaransa, Urusi, Uingereza, China na Ujerumani. 

Mazungumzo yalichukua miaka mitano hadi mataifa haya kufikia maridhiano. 

Mkataba wa JCPOA ulisainiwa na Serikali ya Marekani chini ya aliyekuwa rais Obama na Biden akiwa makamu wa rais. Baada ya uchaguzi urais ukashikwa na Donald Trump. 

Mei 2018 Trump akaukana mkataba kwa kusema unaipendelea Iran, akarudisha vikwazo dhidi ya Iran, tena vigumu zaidi.

Chini ya Trump kila nchi au kampuni au benki iliyoshirikiana na Iran iliadhibiwa. Yaani nchi za Kiafrika hazikuruhusiwa kufanya biashara au hata kupokea misaada kutoka Iran. 

Kwa mujibu wa JCPOA, shirika la kimatifa linalosimamia nishati ya nyuklia (International Atomic Energy Agency – IAEA) limekuwa likiikagua Iran ili isirutubishe urani. Ripoti zinasema Iran imekuwa ikitii. Sasa baada ya Marekani kujitoa Iran ikakataa kukaguliwa vituo vyake vya nishati ya nyuklia. 

Iran ikaanza kurutubisha urani hadi kiwango cha asilimia 60. Hata hivyo hii haina maana nchi hiyo inatengeneza silaha ya nyuklia kwa sababu ili kufanya hivyo itabidi irutubishe asilimia 90.

Rais Biden alipokuwa akifanya kampeni ya urais aliahidi kuwa akichaguliwa ataufufua mkataba wa JCPOA. Ndipo Iran nayo ikakubali kufanya mazungumzo ili Marekani iondoe vikwazo. 

Sasa lugha ya Biden imebadilika. Waziri wake wa mambo ya nje alisema kurudia JCPOA ni kwa masilahi ya Marekani. Akaongeza: “Iwapo hilo halitawezekana basi itabidi tutafute njia mbadala. Tuko tayari kwa lolote.”

Wachambuzi wanasema hiyo “njia mbadala” inamaanisha utumiaji wa silaha za kivita. 

Iran inataka JCPOA iwe na kifungu cha kisheria kitakachohakikisha kuwa hakuna nchi itakayojitoa siku zijazo kama alivyofanya Trump. 

Pia inataka vikwazo viondolewe kabla ya Iran kuacha kurutubisha urani au kabla ya kuruhusu IAEA kukagua vituo vya Iran. Marekani itapaswa kuachia akaunti za Iran ilizozishika, na itapaswa kuiruhusu Iran iuze mafuta yake katika soko la kimatifa na kutumia fedha zake za kigeni bila vizuizi

Tatizo moja ni kuwa ingawa mazungumzo ya Vienna yanashirikisha nchi zilizosaini JCPOA, lakini nyuma ya pazia kuna Israel ambayo ‘inashiriki’ bila kuwamo katika mazungumzo. Hivyo, siku zote Israel imekuwa ikiihimiza Marekani ichukue msimamo mkali  dhidi ya Iran.

Televisheni ya Channel 12 nchini Israel imeripoti kuwa wakuu wa Israel wamekuwa wakiitaka Marekani iishambulie Iran. Wakati huohuo Israel yenyewe imesema iko tayari kuishambulia Iran.

Haya si maneno matupu, kwani kati ya 2010 na 2012 wanasayansi wanne wa Iran wameuawa. Julai 2020 kituo cha nyuklia cha Natanz nchini Iran kilichomwa moto. Novemba 2020 mara baada ya Biden kushinda urais wa Marekani, mwanasayansi mbobezi wa Iran aliuawa. 

Wakati mazungumzo ya Vienna yanaendelea, waziri wa mambo ya nje wa Israel alifika London na Paris akizishawishi serikali za huko zisikubali kufikia makubaliano. 

Pia waziri wa mambo ya kijeshi wa Israel pamoja na mkuu wake wa ujasusi (Mossad) walifika Washington ambako walionana na waziri wa mambo ya kijeshi na waziri wa mambo ya nje wa Marekani pamoja  na maofisa wa Shirika la ujasusi la CIA.

Kwa mujibu wa Gazeti la Yedioth Ahronoth nchini Israel, wageni hao walifika Marekani na ‘ushahidi’ ukionyesha jinsi Iran inavyounda silaha za nyuklia. 

Pamoja na yote haya Israel imepanga kutumia dola bilioni 1.5 ili kuishambulia Iran. Oktoba na Novemba mwaka jana waliendesha mazoezi makubwa ya kivita na Aprili mwaka huu wanakusudia kurudia mazoezi wakitumia ndege za kivita aina ya Lockheed Martin’s F-35.

Marekani nayo inajitayarisha kwa utumiaji wa silaha. Wiki moja kabla ya duru ya nane ya mazungumzo kuanza mjini Vienna, Kamanda Mwandamizi wa Marekani katika Mashariki ya Kati, Jenerali Kenneth McKenzie, ametangaza kuwa majeshi yake yako tayari kuingia kazini iwapo mazungumzo yatashindwa.

Ripoti moja inasema kuwa mawaziri wa majeshi wa Israel na Marekani wamezungumzia uwezekano wa majeshi yao kushambulia vituo vya nyuklia nchini Iran.

Wachambuzi wanasema maelewano yanahitaji Marekani ikubali kuwa lilikuwa kosa kujitoa kutoka JCPOA. Huo ulikuwa mkataba. Marekani ilitakiwa iondoe vikwazo. Iran imetekeleza mkataba kwa mujibu wa ripoti za wachunguzi wa  IAEA miaka ya 2016, 2017 na 2018. 

Marekani imeiwekea Iran vikwazo visivyokuwamo katika JCPOA. Imeiadhibu hata Korea Kusini na Japan kwa kufanya biashara na Iran. Na Iran imewekewa vikwazo hata vya kununua dawa za Uviko-19, saratani na kifafa. Ripoti ya UN ya Januari 2021 inasema vikwazo vya Marekani vimechangia kuongezeka kwa Uviko-19 nchini Iran hadi kufikia vifo zaidi ya 130,000.

Hili ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Swali kubwa linaloulizwa ni je, iwapo mazungumzo ya Vienna yakifanikiwa, na Iran ikafikia makubaliano na Rais Biden, itakuwaje iwapo yeye atashindwa uchaguzi wa 2024 na iwapo Trump atarudi Ikulu ya White House?

 nizar1941@gmail.com

0693 555373

673 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons