Ufuatao ni mchango wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba, alioutoa hivi karibuni bungeni wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Fedha.

“Mheshimiwa mwenyekiti, mimi nashukuru umenipa nafasi nichangie mpango huu. Mheshimiwa mwenyekiti, nimekuja na mipango mitatu. Nimekuja na mpango wa 2016/17, 2017/18 na 2018/19.

Mheshimiwa mwenyekiti, naanza na deni la taifa, kwenye mpango wa 2016/17 tuliambiwa ilipofika Oktoba 2015 deni la taifa lilikuwa dola (za Marekani) bilioni 19. Ikilinganishwa na dola bilioni 18 za mwezi Oktoba mwaka 2014.

Lakini tulipokuja … mpango wa mwaka 2017/18, tukaambiwa deni la taifa limekuwa dola bilioni 18, ongezeko la asilimia 9.76.  Sasa mwaka uliopita ilikuwa 19, mwaka unaofuata tunaambiwa ni 18, lakini kuna ongezeko.

Hawakuishia hapo mheshimiwa Spika, wanasema ongezeko hili wanalinganisha na dola bilioni 16 za kipindi cha 2015. Kwenye mpango huu wa mwanzo wanasema Oktoba ilikuwa 19, kwenye mpango huu wa pili wanasema Oktoba ilikuwa bilioni 16.

Lakini sasa kwenye mpango huu mpya wanasema deni la taifa linafika dola bilioni 26 ukilinganisha na dola bilioni 22 za mwaka 2016 Juni, lakini kwenye ripoti ya Juni tunaambiwa dola bilioni 19.

Kwa hiyo mheshimiwa mwenyekiti moja ya tatizo tulilonalo hapa ni data hizi zinazoletwa hapa na Wizara ya Fedha. Data ni za kwao, haiwezekani kuwa na ‘mistake’ (makosa) ya zaidi ya dola bilioni 3.

Jamani hatusomi ‘ma-document’ haya! Maana yake nini ninachotaka kusema; Ukiangalia mipango yote mitatu kwa kweli ni copy and paste (kunakili moja kwa moja).

Ukipitia yote wamebadilisha language (lugha) ya kinachosemwa ni kile kile, kwa hiyo mheshimiwa mwenyekiti hapa tunapanga lakini ni kwa sababu ni katiba lazima tupange. Yanayokwenda kufanyika wao wanajua… Bunge lako halijui.

Mheshimiwa mwenyekiti nasema, deni la taifa linapanda na sasa hivi linapanda kwa trilioni 4 kwa mwaka kulingana na ripoti za BoT (Benki Kuu). Maana yake ni nini; maana yake tumeamua kama serikali kwamba kila kitu kinafanywa na serikali.

Mheshimiwa mwenyekiti, hatuwezi kuendelea, halipo taifa duniani ambalo kila kitu linajenga kwa fedha zao. Maana kwangu mimi hata ukikopa ni fedha zako ina shida, ukikopa bado ni fedha zako.

Lakini mwenyekiti wewe ni shahidi, tumekwenda Moscow, Uwanja wa Moscow International unajengwa na mtu. Hivi sisi humu ndani tunasema tutafanya PPP, ukitafuta miradi ya PPP haipo.

Serikali hii haiamini katika private sector, tunataka Bunge hili tukubaliane Waziri wa Fedha atuambie serikali hii haikubaliani na private sector. Kwa sababu mipango yako mwanzo mpaka mwisho huongelei private sector, kama tumerudi kwenye ujamaa tuambiane wote tujue.

Lakini haiwezekani tunaimba ujamaa halafu tunataka matokeo ya kibepari, haiwezekani, hakuna katikati, na mwenyekiti soma mpango huu, hakuna production (uzalishaji). Hatuongelei kukuza tija, angalia kwenye kilimo, angalia mazao yote ya kilimo, hakuna anayeongelea kukuza tija.

Maana nilitarajia wangesema mwaka huu tumezalisha tani fulani za mahindi, mwaka kesho ni tani fulani za mahindi – hakuna; pamba hakuna, kahawa hakuna, tumbaku hakuna, korosho hakuna, hakuna mwenyekiti. Sasa tunapanga nini?

Mheshimiwa mwenyekiti, tunapanga vizuri sana lakini mwisho wa siku ukiangalia mpango uliopita yale yale yamesemwa huku mipango yote wanasema wataweka fedha TIB. Fedha hizo zisaidie ku-leverage (kujiinua) kwenye miradi, toka wameanza kusema hawajaweka senti tano TIB.

Sasa mimi naomba mtusaidie, mambo ambayo mnajua hamuwezi kuyafanya msiyaandike, unless (vinginevyo) mnaamini Bunge lako (spika) halisomi ‘ma-document’ haya.

Mheshimiwa mwenyekiti, ukienda humu ndani utaona kabisa kwa mfano leo tunaongelea bei ya mahindi, naomba nikwambie mheshimiwa mwenyekiti, bei ya mahindi kinachofanya bei imeshuka watu hawataki kusema; Zambia wameanzisha commercial farming (kilimo cha kibiashara), wamelima mahindi mengi sana sasa yanauzwa mpaka Somalia.

Kwa vyovyote hatuwezi ku-compete (kushindana) kwa sababu wao wameongeza production (uzalishaji), sisi hatuongelei production. Sisi tunahangaika kubana, kubana sasa mmegeuza ni uchumi wa kubana tu, leo tumeleta sheria hapa ya kubana.

Hakuna anayeongelea kupanua mwenyekiti, hakuna. Mwenyekiti unaweza ukaanzisha kiwanda cha pamba una marobota 240,000 kwa mwaka? Bangladesh kiwanda kimoja kinatumia marobota milioni 5, leo sisi tunaongelea viwanda vya pamba kwa marobota 240,000. Tunamdanganya nani hapa?

Mimi namuonea huruma sana Mheshimiwa Rais, anahangaika wenzake hawamwambii ukweli, mtanisamehe.  Leo rais anakwenda kuwaambia viwanda ndivyo vizalishe sukari lakini tumesema hapa siku zote hakuna aliyetuelewa hili Bunge.

Lakini kwa vile rais amesema viwanda vitazalisha sasa, lakini wabunge nenda kwenye records, tumesema waongezeeni maeneo walime. Ilovo waliomba maeneo wakanyimwa, Ilovo wamekwenda Zambia, leo ni namba two kwa sugar Afrika.

Sisi ardhi tunayo ni over regulations, over regulations na humu ndani waziri angalia anaongelea kodi tu, haongelei kukuza biashara. Anaongelea kukusanya kodi peke yake, tunakusanya kodi kwa nani?

Na leo mheshimiwa mwenyekiti mabenki yanakufa, mabenki yote yana rekodi less profit hata mabenki makubwa. Uchumi unaofanya vizuri mheshimiwa mwenyekiti unaangalia mambo haya mawili; performance ya bank industry na performance ya stock exchange.

Go to Dar es Salaam, turn over exchange, turn over ya stock exchange imeshuka kutoka bilioni 20 mpaka bilioni 2. Na no one is talking about 85%, Waziri wa Fedha hasemi, wala sidhani kama ana interest na sioni mwenye interest na hili jambo.

Ni nini hii! Jamani hii nchi ni yetu wote, na naombeni haiwezekani viwanja vya ndege tujenge kwa pesa zetu, reli kwa pesa zetu, umeme kwa pesa zetu, barabara kwa pesa zetu, hivi sisi ni nani?

Dunia yote imekwenda kwenye private sector, the whole world, China, China kuna barabara … road tall, Malaysia kuna barabara za tall road, kokote tunakoenda. Mheshimiwa mwenyekiti, la mwisho ni mambo mawili:

Moja, tunaleta hapa sheria ambayo humu ndani hawajasema ya kuleta NASACO, mnajua kwa sababu gani mwenyekiti; tunaongelea Tanzania tuna-manage makontena 600,000, Singapore wana-manage makontena milioni 34.

Badala ya kuongelea kuongeza mzigo, tuongeze makontena yatoke 600,000 mpaka milioni 4, milioni 5 tunafikiria ku-regulate hayo hayo, kulinda hizo 600,000 zetu.

Hii ni nini hii, hakuna anayewaza kuongeza biashara, kuongeza production hakuna. Soma mwanzo mpaka mwisho, hatuongelei kukuza biashara.

Mheshimiwa mwenyekiti, leo hii ukienda kwenye mabenki kila kitu kimeshuka, everything mwenyekiti. Naomba nikupe data mbili, tatu; personal landing 2015 ilikuwa asilimia 25.5, leo ni asilimia 8.

Trade 2015 ilifika asilimia 24.6, leo ni asilimia 9, manufacture ilikuwa 30%, leo ni asilimia 3 na hakuna anayesema. Tunaona mambo ni mazuri, ukisema tutaanza kupewa majina.

Mwenyekiti mambo hayako sahihi kwa sababu moja tu; ukiangalia mwenyekiti sababu yetu yote ni moja tu, mpango wetu wa mwaka huu ndio wa mwaka jana, ndio wa mwaka juzi na ndio wa mwaka unaokuja.

Mwenyekiti naomba sana Bunge lako tuamue tuiombe serikali iseme sasa inataka ujamaa, twende kwenye ujamaa moja kwa moja, kama ni ubepari au uchumi wa soko twende kwenye uchumi wa soko.

Short of that tukivichanganya mwenyekiti hatuwezi kwenda kama taifa.

Nakushukuru mheshimiwa mwenyekiti. Mwenyekiti la mwisho nilitaka kusemea suala la Kigoma REA, alisema jana Obama kinachoendelea REA leo ni dhambi.

Kigoma tumepata mkandarasi amepewa kazi, ni Kigoma na Katavi, anataka kuanza CRB inakuja inasema huyu hafai! Hivi CRB mikoa yote hamkuona umuhimu wa kuangalia procurement mnaangalia mkoa mmoja?

Na kwenye sheria ya procurement CRB inakujaje? Lakini sababu tunazijua, aliyekuwa anataka kazi ya Kigoma na Katavi ndiye mwenyekiti wa CRB, ndiye mwenyekiti wa CRB.

Kwa hiyo ni conflict of interest na mawaziri leo; Waziri Kalemani hawezi kuamua, ana kigugumizi, Waziri Mbalawa hawezi kuamua, ana kigugumizi, kwa sababu wote tunazijua.

Watu wa Kigoma mnatuweka wapi? Kwani sisi si Watanzani? But unfortunate hivi sisi ni nani? Nataka kusema mheshimiwa suala la REA na suala la Kigoma kwenye REA Three naombeni mfanye uamuzi kama suala labda mumpe huyo ambaye najua ni mpendwa ambaye yuko CRB, mpeni tufanye kazi.

Yule maskini mwenzetu ambaye alifanya REA Two, ambaye leo hamumuoni wa maana mnyang’anyeni basi, mpeni mnayemtaka.

Nataka kumalizia mheshimiwa mwenyekiti, nakushukuru lakini mwenyekiti mipango yetu kwa kweli ni ya mwaka jana, mwaka juzi. Sielewi maana yake ni nini. Nakushukuru mheshimiwa mwenyekiti.

Spika: Asante sana Mheshimiwa Peter Serukamba, tunaendelea na uchangiaji lakini kabla hatujaendelea waheshimiwa wabunge nikwambieni, Katiba iliweka utaratibu kwamba mipango ya nchi itapita hapa kwanza ninyi muijadili kwanza.  Hilo halikuwekwa hivyo kwa bahati mbaya, iliwekwa hivyo ili nyinyi mseme kwa niaba ya wananchi.

Kwa hiyo katika mambo ya msingi kama haya fungukeni ili wasikie. Usijifunge funge hapo, ooh! Mimi CCM, CCM ndiyo inataka mipango mibovu kabisaa!

Kwa hiyo ni wakati wenu wa kusema tumsaidie waziri, tuisaidie serikali tusonge mbele. Kwa hiyo unapoomba nafasi ya kusema hapa uwe umejiandaa, si ile tu unaunga mkono na kukaa chini.

1450 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!