Na Pd. Tunda la Kanisa (M.afr)
 
Wiki iliyopita mwandishi alizungumzia dhana ya kumtegemea Mungu katika kila uamuzi uufanyao kama binadamu. Je, leo unafahamu anazungumzia nini? Endelea…
Katika somo la pili mtume Paulo anatuasa kuwa kila mtu afuate wito wake kikamilifu na kutimiza mapenzi ya mwenyezi Mungu. Kama wewe ni padre, sheikh, mchungaji, mwinjilisti, mwanasiasa, mtumishi wa umma, waziri, polisi, mwalimu, mkulima, basi timiza wajibu wako kwa uhuru wote.
Timiza wajibu wako kwa furaha, amani na bila kunyanyaswa wala kunyanyasa mtu yeyote. Hii ndiyo tiketi yako ya kwenda mbinguni huku ndiko kusoma alama ya nyakati vizuri.
Tukimtazama Yesu Kristo mwenyewe kama kiongozi, mwalimu na mchungaji mwema kwa kila mtu anajikita katika kutimiza wajibu wake wa kuhubiri habari njema ya ufalme wa upendo, amani, furaha, na umoja.
Siyo hilo tu, lakini habari anayoihubiri Yesu Kristo ni ya kuponya maradhi, majeraha, shida, matatizo, kuliponya taifa la wana wa Israeli. Tukiileta injili katika nchi yetu je, hatuoni alama ya nyakati kwetu kwamba taifa letu linaugua na linahitaji uponyaji?
Je, tunakubali au hatutaki kusikia kamba tunaumwa?  Dawa ya kwanza ya ugonjwa ni “kukubali” kwamba unaumwa, ndipo itakapoanza kufanya kazi, lakini ukikataa basi ndipo kifo nacho kitakapoanza kuingia katika maisha yako.
Ukiitazama nchi yetu kwa jicho la injili unaona wazi kwamba kwamba kama nyakati za Waisraeli, inaugua maradhi ya unyanyapaa, ubaguzi, ukandamizaji, rushwa, kukosa haki, haki kisiasa, uhuru katika maeneo kadhaa, ukosefu wa demokrasia ya kweli, kuzorota kwa usalama wa raia, watu kupotea ( Mwandishi wa habari huko Kibiti, akina Ben Sanane na kadhalika).
 
Yapo mauaji wa polisi huko kibiti, wabunge kuvamiwa na kujeruhiwa kwa risasi (Tundu Lissu), hofu na woga wa kusema ukweli, siasa za uadui, chuki na uhasama, madawa ya kulevya, ulevi wa pombe, vurugu katika uchaguzi na kuzuka kwa madhehebu ya upotoshaji.
Tunasumbuliwa na mmomonyoko wa maadili kwa baadhi ya viongozi wa dini, mmomonyoko wa maadili katika jamii, uvunjifu wa ndoa, ukosefu wa ajira, utoaji mimba, madhara ya vithibiti mimba kwa akina mama, ongezeko la kansa, uhalalishaji wa ndoa za jinsia moja, migogoro ya viongozi wa serikali barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Aasa za kupindukia, ujambazi, maisha magumu kwa walio wengi, na kadhalika. Je, ni kweli nchi yetu haihitaji uponyaji? Je, tukisoma alama za nyakati zinatuambia nini? Je, ni busara kukaa kimya tuu au bora kutamani kusikia sauti ya manabii inasema nini?
Ushauri wangu kwa serikali ya awamu ya tano ni kutengeneza mazingira rafiki ili sauti ya Mungu iweze kusikika kwa uhuru zaidi katika jamii ya Watanzania badala ya kutaka kuelekea kupangiwa mahubiri.
Kwa kweli nikiwa msema kweli niseme wazi kwamba nilikwazwa sana na kauli ya Katibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani iliyosema kwamba serikali itafungia taasisi za dini ambazo zitakiuka malengo yake.
Lakini nilipotafakari niliona kauli hiyo ilitokana na makemeo yaliyotolewa na baadhi ya viongozi wa dini kipindi cha Krismasi juu ya matukio yasiyoashiria amani, utu, usalama wa raia, haki na demokrasia komavu katika nchi yetu.
Tunu inayoitwa amani ni zawadi kutoka kwa Mungu. Mwanadamu amepewa wajibu wa kuitunza tu, basi. Nilipata bahati ya kumwuliza kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa kanisa (Askofu/Mchungaji, jina ni siri yangu kwa sababu za kiusalama). Swali langu lilikuwa hivi “ Ni kwa nini kama Tanzania tunasema tuna amani, lakini wakati huohuo kila mahali kuna walinzi na polisi wanazunguka na bunduki kwenye magari? Je, hii ni alama gani ya nyakati?”
Jibu nililopewa lilikuwa hili, “Ukiona kitu kinaongelewa sana ujue hakipo.” Kwa mfano tunapoongelea pesa na umasikini ujue kuna shida. Watu wakizungumzia mno sukari, ujue kuna upungufu. Rai yangu kwetu sote watawala na wataliwa tusome alama za Nyakati badala ya kupinga kila kisemwacho na watu tofauti, ili tujue kinachoendelea katika taifa letu la Tanzania lenye kila aina ya utajiri.
Nabaki kuendelea kuamini kwamba, “Ukitaka amani ya kweli basi jitahidi kutenda Haki.” Yesu anatukumbusha kuwa, “Heri wapatanishi kwa maana wataitwa wana wa Mungu.”  Sasa ni wakati wa kuitafuta amani ya kweli kwa kusikiliza sauti ya Mungu, sauti ya kinabii. Mungu ibariki Tanzania na watu wake!
Mwandishi wa makala hii, ni msomaji mzuri wa Gazeti la JAMHURI na anapatikana kwa barua pepe, frmapunda91@gmail.com
4910 Total Views 6 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!