NA MICHAEL SARUNGI

Jacob Zuma, Rais mstaafu wa Afrika Kusini ameondoka madarakani baada ya kuwapo shinikizo kutoka ndani ya chama chake cha African National Union (ANC).

Zuma amejizulu wadhifa huo Februari 14, mwaka huu, huku akikana kuhusika katika tuhuma mbalimbali za ufisadi zilizoibua shinikizo la kuondolewa Ikulu, likitokea kwenye chama chake cha ANC.

Zuma aliingia madarakani kwa mara ya kwanza Mei 9, 2009, kisha akashinda tena kiti hicho katika Uchaguzi Mkuu wa  2014.

Tayari aliyekuwa Makamu wa Rais wakati wa utawala wake, Cyril Ramaphosa ameshaapishwa kuchukua nafasi hiyo. Alikula kiapo kwenye kikao cha Bunge Februari 15, mwaka huu ikiwa ni siku moja baada ya kujiuzulu kwa Zuma.

Kujiuzulu kwa Zuma kunaingizwa katika historia ya matukio ya kisiasa yanayowagusa marais wa nchi za Afrika, ikiwamo kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn.

Hailemariam alijiuzulu akisema tukio hilo ni muhimu ili kuleta mageuzi yatakayochochea amani na demokrasia endelevu nchini humo.

Hailemariam, aliyeiongoza Ethiopia tangu mwaka 2012, alijiuzulu pia nafasi yake ya kuuongoza umoja wa vyama unaojulikana kama Ethiopian People’s Revolutionary Democratic Front (EPRDF).

Maelfu ya raia wa Ethiopia wamekufa katika harakati za miaka mitatu ya kupinga utawala wa Hailemariam

Lakini pia kuna kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe aliyefukuzwa Ikulu kwa nguvu za jeshi la nchi hiyo.

Kwa namna hiyo, matukio hayo na mengine kama ya machafuko ya kisiasa na ‘nguvu za umma’ yaliyoziangusha tawala za Libya, Misri na Tunisia yanatoa taswira na mwonekano wa sasa na baadaye narani humo.

Wasomi wachambua

Wanazuoni kadhaa nchini wamesema kuongezeka kwa viongozi wa kiafrika wanaojiuzulu, ni matokeo ya wengi wao kuiacha misingi ya kiutawala ndani ya nchi zao.

Miongoni mwa hayo ni kushiriki ama kushirikiana na watu wasiokuwa wema, kutumia vibaya madaraka yao na kujihusisha na rushwa au vitendo vingine vya kifisadi.

Wamesema viongozi wa Afrika wanapaswa kuwa na macho mapana yenye uwezo wa kusoma alama za nyakati, kisha kuchukua tahadhari.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dk Benson Bana, amesema  tawala nyingi za kiafrika zinakosa mifumo imara ya kitaasisi, badala yake zinakuwa na watu imara ambao wanapoondoka madarakani,  nchi husika zinakuwa matatani.

Dk Bana amesema yanayotokea Afrika Kusini, Ethiopia, Zimbabwe na kwingineko Afrika ni matokeo ya viongozi kujiona ‘miungu watu’ na mwisho wake kujikuta wakiingia katika matatizo makubwa na wananchi waliowaingiza madarakani.

“Haya yaliyotokea (Zimbabwe, Ethiopia na Afrika Kusini) yanapaswa kusambaa katika bara zima la Afrika, ili kuwaondoa viongozi wote waliozigeuza ofisi za umma kama mali zao binafsi wao na ndugu na jamaa zao,” amesema Bana.

Ametoa mfano wa Mugabe, kufuata matakwa ya mkewe (Grace) na kujikuta akiwasahau wananchi wa Zimbabwe, matokeo yake ikawa kuondolewa madarakani kwa nguvu za jeshi la nchi hiyo lililokuwa linamtii.

Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Azavel Lwaitama amesema tatizo linalozikumba nchi nyingi za kiafrika na kujikuta baadhi ya viongozi wake kujiuzulu ama kuondolewa madarakani kabla ya muda wao kumalizika ni usaliti wao viapo vyao.

Amesema usaliti huo ni sehemu ya viashiria vya kutenda na kuongoza mataifa yao kinyume cha kusudio na azma ya mawazo ya waasisi wa mataifa  wanayoyaongoza.

Dk Lwaitama amesema yanayotokea katika bara la Afrika yanachangiwa pia na ubinafsi uliotawala kwa viongozi wengi walioamua `kuzikanyaga’ Katiba za nchi zao na kujali maslahi yao binafsi nay a washirika wao.

“Hata tuliyoyashuhudia Zimbabwe, Ethiopia , Afrika Kusini na kwingine ni ishara  kuwa  watawala wengi ndani ya bara hili wanapaswa kujitathmini kama kweli bado wanaendelea kuwatumikia wananchi waliowaingiza madarakani,” amesema Dk Lwaitama.

Ametoa mfano kuwa nia ya kuanzishwa kwa vyama vya ukombozi katika nchi nyingi za kiafrika ilikuwa ni kuzikomboa nchi hizo na wananchi wake kutoka mikononi mwa wakoloni, waliokuwa wakizitawala  kwa mabavu.

Amesema historia ya utu wa Mwafrika inaanzia tangu Mwafrika alipokataa kuvunjiwa utu wake na kujenga harakati za kudai uhuru na ukombozi,  kutokana na kuonewa, kudhalilishwa na kunyonywa na wakoloni.

Dk Lwaitama amesema kuanzishwa kwa vyama vya ukombozi katika nchi mbalimbali Afrika, Umoja wa Vyama vya Ukombozi vya Afrika Mashariki na Kati PAFMECA) zililenga kuukataa unyonyaji wa kikoloni.

Amesema tofauti na matarajio ya wananchi wengi barani Afrika ya kuona nchi zao zikipiga hatua za kimaendeleo baada ya kupata uhuru, hali imekuwa ni tofauti matokeo yake ni ukoloni kurudi kwa njia ya nyuma ya uwekezaji.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Bashiru Ally amesema viongozi wa Afrika wanapaswa kurudi nyuma na kujiuliza, nini yalikuwa malengo ya waasisi wa nchi hizo wakati wa kupigania uhuru.

Amesema magwiji wa siasa za kiafrika kama Hayati Nkwame Nkrumah, Mwalimu Nyerere, Gamal Abdel Nasser  na wenzao  waliokuwepo  wakati  Umoja wa nchi Huru za Afrika (OAU), ukianzishwa Mei 25, 1963, ikitokea wakafufuka wanaweza wasiamini yanayotokea barani humo.

Dk Bashiru amesema baadhi ya viongozi wa Afrika wameshindwa kuzifikisha nchi zao katika maendeleo yaliyokuwa shabaha ya uhuru na ukombozi kutoka kwa wakoloni.

“Hebu tujiulize shabaha ya uhuru na ukombozi wa mwafrika tangu uhuru wa nchi ya Gold Coast (Ghana) mwaka 1957 hadi Afrika Kusini (1994), ikiwa ni nchi ya mwisho kujikomboa barani Afrika, je Afrika imejikomboa, jibu ni hapana,” amesema.

Amesema Afrika haitajikomboa endapo watawala hawatabadili misimamo yao na kuzirudia fikra za waasisi wa mataifa hayo.

Dk Bashiru amesema, tathmini ya kiuchumi barani Afrika inapaswa kuelekezwa kwa nchi za bara hilo kupima ukuaji wa uchumi wake kutoka katika lindi la umaskini na matumizi ya rasilimali kama ardhi, misitu, madini na nguvukazi watu.

Amesema hakuna kitu kitakachorudisha heshima ya viongozi wa Afrika zaidi ya kuungana na kuwa kitu kimoja na kushirikiana katika nyanja pana ya kiuchumi na kuacha kuwa tegemezi wa nchi za Ulaya na Marekani.

Amesema haya yanayoshuhudiwa kutokea katika nchi za Afrika Kusini, Ethiopia na Zimbabwe ni matokeo ya viongozi hao kusahau misingi ya awali ya kuwa watumishi wa wananchi, badala yake kutumikia nafsi zao.

Ametoa mfano kuondolewa madarakani kwa Mugabe kumedhihirisha kwamba `alicheza karata’ zake vibaya kwa kuiacha misingi ya awali ya kuleta ukombozi wa kiuchumi kwa Wazimbabwe.

Kwa mujibu wa Dk Bashiru, kuondolewa kwa Mugabe kulichochewa na tofauti za kisiasa kati ya makundi mawili makubwa ndani ya chama tawala cha ZANU-PF.

Makundi hayo yalikuwa yaliyokuwa yanamuunga mkono mke wa Mugabe, Grace Mugabe na aliyekuwa Makamu wa Rais na sasa Rais wa nchi hiyo, Emmerson Mnangagwa, wawili hao wakitaka kumrithi Mugabe.

Amesema hiyo yote ilitokea kwa sababu ya Mugabe kusahau misingi aliyowaahidi Wazimbabwe wakati anaomba uungwaji mkono kutoka kwa raia wan chi hiyo alipokuwa akiomba ridhaa ya kuwaongoza.

“Hili la Zimbabwe halina tofauti kubwa na yaliyomkuta Zuma japo tuhuma zake kubwa ni ufisadi na kutumia madaraka vibaya, kote huko ni kukiuka miiko ya uongozi na kutanguliza ubinafsi,” amesema.

Ametoa mfano kuwa ukosefu wa uongozi imara nchini Ethiopia umesababisha nchi hiyo kuwa dhaifu, inayokumbwa na misukosuko jambo ambalo ni hatari  kwa usalama  katika  eneo zima la pembezoni mwa Afrika.

WASIFU MFUPI WA ZUMA

2005: Alituhumiwa kwa rushwa ya mabilioni ya dola kwenye mkataba wa silaha wa mwaka 1999 madai ambayo yalitupiliwa mbali kabla hajawa Rais kwa mara ya kwanza mwaka 2009

2016: Mahakama iliamuru ashitakiwe kwa makosa 18 ya rushwa dhidi ya mkataba wa silaha ambao alikatia rufaa akashinda.

2005: Alishitakiwa kwa kumbaka rafiki wa familia na kufutiwa mashitaka mwaka 2006

2016: Mahakama iliamuru kuwa amekiuka kiapo chake kama Rais na kutumia fedha za Serikali kuboresha makazi yake binafsi, fedha ambazo alizilipa baadaye

2017: Wakili wa Serikali alisema ateua Jaji Kiongozi wa kamati ya kuchunguza iwapo ana uhusiano na familia tajiri ya Gupta madai ambayo ameyakanusha

2018: Zuma alikubali maombi hayo

Akiwa na miaka 17 Zuma alijiunga na ANC na kuwa mwanacha hodari katika tawi lake la Jeshini Umkhonto We Sizwe, in 1962.

Kuzaliwa

Alizaliwa tarehe 12 Aprili 1942. Nkandla, Afrika Kusini. Alikuwa  Rais wa Afrika Kusini tangu mwaka 2009 hadi 2018, alipojiuzulu kwa kashfa mbalimbali za rushwa.

By Jamhuri