Uchaguzi Tanzania tutavuna tunachopanda

Balile
Kwa siku za karibuni nimejipa jukumu la kusoma vitabu vitakafitu. Nasoma Biblia na Korani Tukufu. Nasoma maandiko matakatifu. Katika safu hii sitarejea Biblia wala Korani Tukufu, bali ujumbe mmoja tu kutoka vitabu hivi – MAONYO YA MAKUHANI na wengine wanaoitwa manabii kwa njia ya nyaraka.
Kila walichokiona walikiandika. Ndiyo maana leo tunasoma Biblia au Korani Tukufu na kupata historia na utabiri. Ni ujumbe huo ninaotaka kuufikisha leo. Siku za kuishi hapa duniani zinazidi kupungua. Nakaribia nusu karine nikiwa hai hapa duniani, hivyo najua hata kama si kwa mapenzi yangu, bali kwa mapenzi yake aliye juu ipo siku nitaelekelea waliko babu, bibi na baba yangu. Kwenye nyumba ya milele!
Sitanii, nikiwa na uelewa katika maisha yangu nimeshuhudia uchaguzi wa mwaka 1980, mwaka 1985, mwaka 1990, mwaka 1995, mwaka 2000, mwaka 2005, mwaka 2010 na mwaka 2015. Ule wa mwaka 1975 nilikuwa bado mdogo sikushiriki kampeni kwa njia yoyote. Mwaka 1980 ndipo nimeshiriki kampeni chini ya alama ya jembe na nyumba vikiwakilisha wagombea.
Nimepata fursa ya kushuhudia uchaguzi wa mfumo wa chama kimoja na uchaguzi wa mfumo wa vyama vingi. Nikiri kwamba uchaguzi hadi mwaka 1990 ulikuwa sawa na utani wa jadi wa mpira wa Simba na Yanga. Sina uhakika sana kwa nini, ila nadhani ni uwapo wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyetaka kujenga Tanzania ya mfano.
Ikumbukwe mwaka 1963 Chama cha TANU kilipitisha Azimio la Tanganyika kuwa nchi ya Chama kimoja. Azimio hili lilitekelezwa rasmi mwaka 1965. Chama cha TANU kilishika hatamu rasmi na mwaka 1967 kilitangaza Azimio la Arusha, ambapo moja ya mambo liliyotaka ni viongozi kutenganisha siasa na biashara.
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi, Oscar Kambona alipinga Azimio hili. Kambona alitajwa kuwa na mali nyingine zikiwamo nyumba za kupangisha na kwamba alikuwa anapata mshahara zaidi ya mmoja ikiwamo kupokea fedha kutoka nje ya nchi.
TANU ilipoona ukakasi mwaka 1968 ikamfukuza uanachama Kambona pamoja na wabunge wengine akiwamo Dk. Fortunatus Lwantyantika Masha (Jimbo la Geita Mashariki wakati huo), Joseph Kaselabantu (Nzega Mashariki), Wilfred Mwakitwange (Taifa), Stephen Kibuga (Mufindi), Modestus Chogga (Iringa Kusini), Eli Anangisye (Rungwe Kaskazini), Gervas Kaneno (Karagwe) na Jeremiah Bakampenja (Ihangiro, Bukoba).
Sitanii, historia zilizoandikwa zinanionyesha kuwa mwaka mmoja kabla ya Uhuru, mwaka 1960 uliitishwa uchaguzi wa vyama vingi. TANU kilimuengua Herman Elias Sarwatt wa Mbulu akaamua kuwa mgombea binafsi, akashinda. TANU mwaka 1965 kilimteua tena Sarwatt agombee kwa tiketi ya TANU na akashinda.
Nimejaribu kurejea hizo historia, nikiamini zitanileta hadi mwaka 1995, ambapo Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi, alijaribu kwa kutumia polisi katika uchaguzi kuchokoza Watanzania waliokuwa wamehamasishwa na vuguvugu la NCCR-Mageuzi kwa kuwapiga mabomu wakati wanambeba aliyekuwa mgombea, Agustino Lyatonga Mrema.
Hali ilikuwa inaanza kuwa mbaya, hadi Mwalimu Nyerere aliposimama na kusema: “Kama anataka kubebwa kama jeneza, mwache abebwe.” Baada ya kauli hii ya Nyerere Mrema hakukubali kubebwa tena. Uchaguzi huo uliodhaniwa kuwa ungekuwa wa kwanza kuitia doa Tanzania ukapita salama salmini.
Tanzania tumekuwa na uchaguzi wa ushindani. Tangu mwaka 1992, ambapo Mwalimu Nyerere aliishawishi Serikali ya Rais Mwinyi kukubali mfumo wa vyama vingi kwa hoja kwamba kama “wengi washinde, na wachache wasikilizwe” tumekuwa na uchaguzi wa ushindani wa hoja.
Ndiyo maana mwaka 1995 Dk. Wilbrod Slaa alipomshinda Patrick Qorro katika kura za maoni kwa Jimbo la Mbulu, na CCM ikamuengua akahamia CHADEMA, ambako alimshinda Qorro na kuwa mbunge hadi mwaka 2015 alipojivua uanachama. Tulishuhudia siasa za ushindani bila kumwaga damu. Mwaka 1992 mfumo wa vyama vinge ulirejeshwa. Sina uhakika kama bado tunauhitaji.
Sitanii, naandika makala hii kwa kurejea matukio ya uchaguzi mdogo uliofanyika Novemba, mwaka jana kwa kata 43 za udiwani, uchaguzi wa majimbo matatu ya ubunge ambayo upinzani wa kweli haukusimamisha wagombea na matokeo ya uchaguzi wa Februari 17, ambapo hadi tunakwenda mitamboni zilikuwapo taarifa kuwa wagombea waliotoka upinzani wakajiunga CCM na wakateuliwa tena kugombea kupitia CCM wameshinda.
Hawa si wengine, bali ni Maulid Mtulia (Kinondoni) na Godwin Mollel (Siha). Yamekuwapo matukio ya vifo viwili vinavyohusishwa na uchaguzi, moja likiwa la polisi kumpiga risasi mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliyekuwa kwenye daladala.
Yametajwa matukio ya sanduku la kura kutolewa kituoni likarejeshwa. Yametajwa matukio ya askari polisi kughasi wapigakura. Yametajwa matukio ya wapigakura kujitokeza wachache kuliko maelezo. Imetajwa mwandishi wa habari kukamatwa. Tumeshuhudia picha katika mitandao watu wakipigwa. Tumeona uchaguzi ukisusiwa na  vyama vikiondoa mawakala wake.
Sitanii, kwa tafsiri ya kawaida wanaofanya haya yote wanaweza kutumia maneno ya mitaani kwa kusema “wapinzani tumewanyoosha”, ikiwa wananufaika na matokeo hayo. Hata hivyo, nasema na naomba ibaki katika kumbukumbu kuwa tunapanda mbegu.
Inawezekana mbegu inayopandwa sasa isiote mwaka huu, miaka minne au mitano ijayo, ila tukiendelea hivi miaka 15 ijayo naomba kutabiri kuwa Tanzania itakuwa na sura tofauti kisiasa. Wimbo wa utulivu na amani huenda tusiusikie tena.
Naangalia nchi zote zinazoishi kwa tabu kama Somalia, Ethiopia ambako Waziri Mkuu wake amejiuzulu, Sierra Leon, Nigeria, Yugoslavia, Iraq na nyingine walianza kidogo kidogo kama tunavyofanya sisi kwa sasa.
Tunapanda mbegu ya chuki. Familia zinazoumizwa, familia zinazopoteza wapendwa wao kwa sababu ya siasa tujaribu kuvaa viatu vyao. Tujiulize kama ipo siku zitawasamehe wenye kuua wapendwa wao.
Na hapa ninapoandika hivi, naomba nieleweke. Sitaki kuamini kuwa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imekaa ikaamua kuchukua mkondo huu wa kisiasa. Nazungumza na wanasiasa wengi ndani ya CCM wanaoushangaa mfumo huu mpya.
Wengi wanadhani kuna kundi dogo ndani ya chama ambalo linapeleka chaka mfumo wa siasa nchini. CCM imepata kuwa na Mtandao ulioelekea kukimega chama, lakini sasa hili kundi lisilojulikana kama lipo ndani ya CCM na likatenda matukio haya basi tujue linavunja misingi ya umoja, amani na utulivu.
Sitanii, nimesema nimeamua kuweka kumbukumbu. Nikasema niseme kuwa aina ya siasa tulizozishuhudia katika uchaguzi mdogo nilioutaja ikiwa zitaendelea, basi tujue kuwa tunaimwagia nchi petrol. Siku mtu akiwasha kiberiti hatutakuwa na pa kujificha moto ukiwaka. Tupige moyo konde. Tufahamu kuwa maisha bila siasa yanawezekana.
Kila nikisoma maandiko matakatifu sijaona mahala ambapo Yesu au Mtume Mohamed alilazimika kutumia jeshi kulazimisha atakalo lifanyike. Haya majeshi nayo waliomo wajue Mungu anamlipa mtu kadri ya matendo yake. Yote tunayoyafanya kwa kivuli cha taasisi tunazozitumikia siku ya hukumu tutatoa hesabu binafsi. Mungu iepushe Tanzania kikombe hiki.