Tanzania ni nchi tajiri kwa rasilimali, na licha ya pato lake kukua mwaka hadi mwaka, wananchi wake ni maskini.

Hiyo inatokana na sekta za ajira kuwa chini kiuzalishaji. Watanzania wengi wako katika sekta isiyo rasmi ambako uzalishaji na kipato uko chini.

 

Akizungumza wiki iliyopita katika warsha iliyoandaliwa kuwajengea wanahabari uwezo wa kuripoti habari za Umoja wa Mataifa (UN) jijini Dar es Salaam, Ofisa Mawasiliano wa Umoja huo, Hoyce Temu, amesema uwiano kati ya nafasi za kazi haulingani na idadi ya watu kwa asilimia 80.

 

Anasema wastani huo ni wa juu ikilinganishwa na viwango vya kimataifa na vya kanda.

Hata hivyo, anasema asilimia 36 ya watu hao walioajiriwa wanaishi kwa kipato cha chini ya mstari wa umaskini, jambo linaloashiria kuna uzalishaji duni na ukosefu wa kazi.


“Licha ya kukosekana kwa ajira, soko la ajira Tanzania lina ubaguzi wa jinsia – wanawake wanalipwa ujira mdogo zaidi ikilinganishwa na wanaume.


“Wastani wa vipato vya mwezi miongoni mwa waajiriwa wa kiume ni mara mbili ya vile vya wafanyakazi wanawake. Vile vile kiwango cha kutoajiriwa kipo juu zaidi,” anasema.

 

Anasema kilimo kinachangia robo ya pato la taifa kwa asilimia 85 ya bidhaa zinazopelekwa nje, na kinatoa ajira kwa karibu asilimia 80 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi, na katika hao, asilimia 90 ni wanawake.

 

Hata hivyo, mapato katika sekta ya kilimo ambacho ni uti wa mgongo wa Taifa letu, ni ya chini kutokana na kiwango duni cha uzalishaji wa kilimo unaotokana na uwekezaji duni katika sekta ya miundombinu.

 

Ofisa huyo anasema ukosefu wa pembejeo, huduma za ugani, mikopo, matumizi ya teknolojia ya kisasa, biashara na masoko ya uhakika, ni miongoni mwa sababu za uzalishaji duni wa mazao.

 

Pia uendeshaji wa kilimo kinachotegemea mvua pekee na matumizi yasiyo endelevu, pia huchangia katika kupunguza uzalishaji.

 

“Yote haya kwa pamoja ni mambo yaliyosababisha kuwapo kwa nguvu kazi nyingi kwenye kilimo, lakini ambayo hailingani na kinachozalishwa kwenye ardhi mtaji,” anasema.

 

Anasema UN inatoa misaada ya kiufundi na kiujuzi kuziwezesha wizara, idara, wakala na mamlaka za Serikali za Mitaa na wadau wengine kuendesha uchumi. Pia kuendeleza upatikanaji wa fursa sawa za kiuchumi, kukuza biashara na kuwa na matumizi sahihi ya rasilimali ili kuongeza uzalishaji na utengenezaji nafasi za ajira.

 

Temu anasema UN pia inaipatia Serikali misaada ya kuandaa mkakati wa ukuaji, kwa kumsaidia kila Mtanzania kupata fursa za kukua kiuchumi na hasa makundi ya wanyonge watu wanyonge.

 

“Hii ni pamoja na kutoa nyenzo za kimkakati za kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi, yanayolenga kufanya mazingira yawe endelevu yasiyombana maskini na hasa kwa njia ya utetezi wa sera na kuendeleza uwezo na kushirikisha maarifa,” anasema.

Elimu

Anasema kwamba elimu ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha elimu ya msingi inawafikia wote, ikiwa ni lengo la pili la Maendeleo ya Milenia.

 

Anasema tangu kufutwa kwa ada katika elimu ya msingi mwaka 2001, uandikishwaji shule umepanda ambapo kuanzia mwaka huo asilimia 59 ya watoto walikuwa na umri wa kwenda shule waliandikishwa.

 

Mwaka 2010 idadi hiyo iliongezeka na kufikia asilimia 95, na kumekuwapo na ongezeko la kuridhisha katika ngazi za elimu ya awali na sekondari.


Licha ya maendeleo haya, changamoto iliyopo ni kuhakikisha watoto wanapata elimu bora, kwa kuwa viwango vimekuwa vikishuka katika ngazi zote.

 

“Sababu ya ongezeko kubwa la uandikishaji kwa ufupi halikuendana na upatikanaji wa ubora katika mahitaji ya elimu kama vile walimu wenye sifa, vifaa vya elimu na mazingira yenye hadhi ya kujifunzia.

 

“Kwa mfano, ni asilimia 53 tu ya watoto wenye umri wa miaka 13 waliokamilisha mzunguko mzima wa elimu ya msingi mwaka 2010, na watoto wachache tu waliofaulu mitihani ya cheti cha elimu ya msingi,” anasema.

 

Anasema kumekuwa na tofauti kubwa kati ya mkoa mmoja na mwingine katika suala la kupata elimu, uwiano wa watoto wenye umri wa kwenda shule walioandikishwa elimu ya msingi unaanzia asilimia 88.7 kwa Mkoa wa Tabora na asilimia 99.8 kwa mkoa wa Tanga.

 

Anasema UN imesaidia Serikili kutoa fursa katika upatikanaji wa elimu bora kwa wote katika ngazi zote.

 

“Mkakati huu wa UN unalenga kuongeza ubora wa elimu na harakati, zinazolenga kumsaidia mwanafunzi kuongeza ubora wa ufundishaji na kutoa fursa kwa makundi yaliyotengwa kiuchumi na kijamii.

 

“Katika kuandaa mfumo wa elimu wenye ufanisi na wenye kuleta tija, Umoja wa Mataifa unasaidia uanzishwaji wa programu ya utoaji wa chakula shuleni,” anasema Temu.

UN pia inasaidia harakati za kuimarisha mfumo wa mafunzo ya ualimu kabla na wakati wakiwa kazini, kuimarisha viwango vya ufundishaji katika ngazi ya sekondari na elimu ya juu katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.


1284 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!