Na Deodatus Balile, Dar es Salaam

Mwezi huu aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, amejiuzulu. Ndugai ambaye ni Mbunge wa Kongwa, amejiuzulu kutokana na maneno makali aliyoyatoa Desemba 28, 2021 akiishambulia serikali kwa kuchukua mikopo kutoka nje ya nchi. Kilicholeta shida si mikopo, ila watu walijiuliza, kwa nini mikopo ihojiwe sasa wakati awamu zote zilikuwa zinakopa?

Sitanii, Oktoba 26, 2021 niliandika makala ndefu nikieleza jinsi Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ilivyokopa fedha nyingi, wastani wa Sh trilioni 29 katika kipindi cha miaka mitano tu. 

Kwa bahati mbaya, muda wote serikali ya Rais Magufuli ilikuwa ikitwambia Watanzania kuwa inanunua ndege, inajenga reli, Bwawa la Mwalimu Nyerere la Umeme na miradi mingine mingi kwa fedha zetu; haikopi.

Katika makala hiyo nilihoji, hivi kama tungeambiwa kuwa serikali ilikuwa inakopa kungepunguza nini? Nilihoji kulikuwapo sababu gani ya kutudanganya kuwa hatukopi? Nilipongeza utaratibu uliotumiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekopa Sh trilioni 1.3 tu kutoka IMF, lakini zimejenga madarasa 15,000, zimejenga vituo vya afya 237 na miradi mingine mingi ikiwamo ya maji.

Kwa bahati mbaya mkopo alioukopa Rais Samia, na hadharani, kipo kikundi ambacho kiliona ndio mlango wa kujengea hoja zao za kuelekea mwaka 2025. Kuna watu wanasema Watanzania ni wapole, ila binafsi naomba tusiendelee kuamini hivyo. Maneno yaliyotolewa na Watanzania dhidi ya Ndugai, tena wanachama wenzake, yalinidhihirishia kuwa watu wana uchungu na nchi yao.

Sitanii, leo siandiki kwa kuzama katika mgogoro wa mkopo, bali nazungumzia Uspika. Nafahamu kuna watu wamechomeka jina langu kwenye orodha iliyokuwa inatembea mtandaoni ikionyesha kuwa ni ya watu waliochukua fomu za kugombea Uspika. Binafsi nimetamka mara kadhaa kuwa mimi msimamo wangu uko wazi, siwezi kuchanganya siasa na uandishi wa habari.

Nimesema mara kadhaa kuwa ikitokea nikafanya kazi nje ya uandishi wa habari, sitarudi kwenye chumba cha habari kuwasimamia waandishi au kuhariri kazi za uandishi wa habari, bali nitabaki kuwa mchambuzi wa masuala yanavyoendelea kwa kutoa maoni yangu, badala ya kufanya kazi ya uandishi ambayo ni ya kukusanya, kuchakata na kuchapisha.

Ni katika muktadha huo nawaangalia wagombea Uspika waliojitokeza. Wengi waliojitokeza kuwania nafasi ya kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) nawafahamu vizuri, nao wananifahamu. Niseme tu kuwa miongoni mwa watia nia hao, wagombea halisi ni wawili tu. Nafahamu kuwa wawili hawa wamelitumikia Bunge kwa muda mrefu na wanazifahamu kanuni za mchezo. Wengine wanatangaza majina yao tu.

Sitanii, ukiacha suala la kufahamu sheria zinazoendesha Bunge, lipo suala jingine. Bunge la sasa linakuwa na changamoto za aina yake. Utafiti umeonyesha kuwa wananchi wamepungukiwa imani kuhusu Bunge baada ya matangazo kuzuiwa kurushwa ‘live’. 

Hiyo ni moja ya changamoto atakazokutana nazo Spika ajaye. Bunge hili lina vijana, ingawa mvutano wa vyama vingi kwa sasa uko likizo kutokana na idadi ya wabunge wa upinzani bungeni.

Kwa vyovyote iwavyo, Bunge la 12 limepata changamoto. Amefariki dunia Rais wa Awamu ya Tano, Dk. Magufuli na Spika Ndugai amejiuzulu. Katika mihimili mitatu, wakuu wa mihimili miwili watakuwa ni wapya kabisa baada ya uchaguzi wa Spika. Wawili hawa wanashika hatamu katika kipindi ambacho kuna changamoto katika mfumo na utaratibu wa kufanya siasa nchini.

Bunge hili linatarajiwa kushirikiana na Rais Samia kuponya vidonda vya kisiasa. Kwa upande wa wafanyabiashara, Rais Samia amekwisha kufanikiwa kuponya vidonda kwa asilimia kubwa. 

Wafanyabiashara sasa wanapewa marejesho ya VAT, suala ambalo walikwishalisahau, akaunti zao hazikamatwi na makusanyo ya serikali yamevunja rekodi kwa kukusanya Sh trilioni 2.51 kwa mwezi Desemba, 2021.

Sitanii, tusifanye majaribio ya kupima kina cha maji kwa kutumbukiza miguu yote miwili katika uchaguzi wa Spika. Uspika si cheo cha kujifunzia siasa. Tunahitaji Spika mwenye utulivu kichwani. Umri nao usindikize utulivu huo. 

Awe na uzoefu wa sheria na kanuni, lakini asiwe mtu mwenye mihemko. Tukiamua kuchagua mtu mwenye mihemko kuwa Spika, tufahamu kuwa tutakuwa tumeamua kupanda mtumbwi wa mabarafu kuelekea bahari kuu. Mungu ibariki Tanzania.

684 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons