TEF kuwakusanya wahariri Afrika

Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

Wahariri wa vyombo vya habari kutoka nchi mbalimbali barani Afrika wanatarajiwa kukutana mara mbili nchini Tanzania, ndani ya miezi miwili, JAMHURI limeelezwa.

Katika matukio hayo ya kihistoria, wahariri kutoka zaidi ya mataifa 10 ya Afrika watakutana kwa mara ya kwanza Machi mwaka huu huko Zanzibar, kabla ya kukutana tena Mei 3, mwaka huu jijini Arusha.

Akizungumza katika kikao kazi cha Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kilichofanyika kwenye Hoteli ya Sapphire jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, amesema mikutano hiyo itatumika kuimarisha uhuru wa habari nchini na maendeleo ya kiuchumi kwa Afrika.

“Mikutano hii miwili ya kitaaluma ni muhimu kwani itaimarisha uhusiano wa kitaaluma kwa wanahabari wa Afrika Mashariki na nchi zinazotuzunguka.

“Wahariri (wanahabari) kutoka nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa Machi huko Zanzibar, pamoja na mataifa jirani,” amesema Balile.

Mgeni rasmi katika mkutano wa Arusha utakaofanyika wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, Mei 3, anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan; wakati Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi akitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa Machi mwaka huu huko Zanzibar.

Mbali na mataifa ya Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, DRC na Sudan Kusini, wageni kutoka Zambia na Malawi wanatazamiwa kuwapo Zanzibar; huku wahariri kutoka Afrika Kusini, Ghana na Nigeria wakialikwa kwenye mkutano wa Arusha.

Balile amesema kukutana kwa wanahabari kutoka mataifa mbalimbali hasa ya Afrika Mashariki kutawezesha vyombo vya habari kuwa na ajenda moja katika kuchangia kukua kwa uchumi, amani na usalama katika ukanda huu.

 “Maandalizi yanakwenda vizuri yakiongozwa na kamati mbalimbali zilizoundwa kwa ajili ya kuandaa mikutano hii miwili muhimu,” anasema Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TEF (KUT), Salim Said Salim.

Mbali mikutano hiyo, kikao hicho kilizungumzia pia masuala ya kimaadili, kitaaluma na uwajibikaji wa wahariri na waandishi wa habari nchini pamoja na mabadiliko katika Wizara ya Habari na mchakato wa mabadiliko ya sheria.