DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Vijana wanaotaka kujiunga na Jeshi la Polisi wamelalamika majina yao kuondolewa katika orodha kwa kile wanachokitaja kuwa ni baada ya kufaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza na la pili katika mitihani yao ya kidato cha sita.

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, vijana hao kutoka mikoa ya Mara, Lindi na Mtwara (majina yanahifadhiwa) wanasema licha ya kuwa na sifa nyingine zinazostahili lakini wanashangaa wao kuondolewa katika orodha hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita huku wahitimu wa kidato cha nne wakiwa na ufaulu wa kiwango cha daraja la nne wakipata nafasi.

“Nina miaka 22, nimehitimu kidato cha sita mwaka jana, matokeo yangu ya kumaliza elimu ya kidato cha sita nimepata ufaulu wa daraja la pili.

“Lakini jina langu limeondolewa katika orodha ya wanaotakiwa katika usaili wakati vigezo vyote vinavyotakiwa katika nafasi za ajira hizo ninazo,” anasema kijana mmoja ambaye ni mkazi wa Mara.

Nao vijana wengine wa Lindi na Mtwara ambao ni wahitimu wa kidato cha sita wanasema hawajui kwanini wao wanaondolewa kisa wana ufaulu wa kiwango cha madaraja hayo.

‘‘Hatujui katika mikoa mingine hali ikoje, lakini baadhi yetu wenye ufaulu wa daraja la kwanza na la pili katika matokeo yetu ya kidato cha sita tumeachwa na hatujachukuliwa. Ila waliomaliza kidato cha nne na wenye ufaulu wa daraja la nne wameitwa kwa wingi,” anasema kijana mmoja wa mkoani Lindi.

‘‘Inavyoonekana wanaotakiwa kujiunga na Jeshi la Polisi ni wale ambao hawakufanya vizuri katika mitihani yao ya kidato cha nne au kidato cha sita. Waliopata daraja la nne ndio wamechukuliwa lakini wenye daraja la kwanza na pili tumeachwa,” anasema kijana mmoja wa mkoani Lindi.

Kutokana na malalamiko hayo, JAMHURI limemtafuta Msemaji wa jeshi hilo, David Misime, zaidi ya mara 10 kupitia simu yake ya mkononi lakini hakupokea na alipoandikiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) ulioomba ufafanuzi kuhusu namna usaili wa ajira hizo unavyoendeshwa, nao hakuujibu licha ya kuonyesha umemfikia. 

Malalamiko ya vijana hao yanakuja baada ya hivi karibuni jeshi hilo kutangaza nafasi mbalimbali za ajira kwa vijana wanaotaka kujiunga nalo.

Pia kupitia tangazo la jeshi hilo lililotolewa Septemba 24, mwaka huu na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro, linasema usaili wa vijana wenye elimu ya shahada, stashahada na astashahada walioomba kujiunga kupitia Makao Makuu ya Polisi Dodoma kuwa usaili wao utafanyika kuanzia Septemba 27 hadi 30, mwaka huu jijini Dar es Salaam, eneo la Polisi (Barracks) Barabara ya Kilwa karibu na Hospitali Kuu ya Polisi Kilwa Road, kuanzia saa mbili asubuhi.

Pia tangazo hilo linasema kuwa kwa wale wenye elimu ya kidato cha nne na sita waliowasilisha maombi yao kwa makamanda wa polisi wa mikoa watafanya usaili kwenye mikoa yao.

Aidha, tangazo hilo limeorodhesha vijana 1,475 wenye elimu ya shahada, stashahada na astashahada waliochaguliwa kufanya usaili huo.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ajira mpya za askari 2,300 kwa vyombo vyote vya usalama vilivyopo chini yake.

Akizungumza mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita katika kikao chake na viongozi wakuu wa utawala wa vyombo hivyo, anasema wamepokea barua kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuhusu ajira mpya.

“Rais Samia ametoa ajira mpya kwa vyombo vya usalama vilivyo chini ya  Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ametupatia Jeshi la Uhamiaji nafasi 350 kwa kada ya konstebo, lakini pia ametupatia nafasi 700 kwa Jeshi la Magereza kwa nafasi za warder na wardress, pia ametupatia nafasi 250 kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kada ya konstebo na ametupatia nafasi 1,000 kwa Jeshi la Polisi kwa kada ya konstebo,” anasema Simbachawene.

Anasema kwa niaba yake na vyombo anavyoviongoza anamshukuru Rais Samia kwa kutoa nafasi hizo zitakazopunguza kwa kiasi kikubwa ukosefu wa askari.

“Napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya wizara na vyombo hivi ambavyo wizara yetu inavisimamia kumshukuru Rais Samia kwa kutupatia nafasi hizi, pamoja na changamoto tulizokuwa nazo.

“Suala la upungufu wa askari lilikuwa jambo linalotupa changamoto, na uzuri ni kwamba kibali kilichokuja kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kimeelekeza kabisa tuajiri askari wa ngazi ya chini,” anasema Simbachawene.

Anasema askari hao ndio watakuwa wapiganaji, wapambanaji na anatarajia vyombo hivyo katika mchakato wake vitazingatia maelekezo ya serikali ya kuhakikisha kwamba watakaopata nafasi hizo ni wale waliopitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kupata malezi na kuhitimu, pia walishiriki kujenga nchi kupitia JKT. 

Pia anasema kama kutakuwa kuna namna yoyote tofauti na sifa hizo, zitatolewa na vyombo vyenyewe katika kutangaza nafasi hizo katika maeneo yao.

1817 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!