Desemba 15, 2016 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya ziara katika Wilaya ya Ngorongoro. Safari hii ililenga, pamoja na mambo mengine, kupata suluhu ya migogoro ya ardhi inayoendelea kwa miaka mingi sasa.

Migogoro katika Tarafa ya Loliondo hailengi kitu kingine, isipokuwa ni masuala ya uchumi. Kuna kundi la watu walioamua kwa makusudi kuona haikomi, wakitambua kuwa kukoma kwake ni mwisho wa maslahi yao manono wanayovuna katika eneo hilo.

Ni kwa sababu hiyo, Waziri Mkuu alionesha kushangazwa kwake na utitiri wa mashirika yasiyo ya serikali (NGOs) zaidi ya 30 katika eneo hilo pekee!

Pamoja na dhamira njema ya Waziri Mkuu ya kuona Loliondo na Ngorongoro kwa jumla inatulia, kuna dalili zote kuwa mgogoro wa ardhi katika eneo hilo hautakoma.

Bahati mbaya viongozi wa Serikali waliopaswa kumweleza Waziri Mkuu ukweli wa mambo na kumwonesha uharibifu wa mazingira uliovuka kiwango, wao ndiyo walioongoza kumpotosha.

Ili Loliondo itulie, sharti wajitokeze watu wa kuthubutu kueleza ukweli bayana ili kuwasaidia viongozi wakuu wa Serikali kutambua kinachoendelea na kuleta suluhu ya kudumu.

Endapo tutaendelea kuoneana haya kwenye suala hili la Loliondo na mengine ya aina yake nchini, kamwe hatutamaliza migogoro. Ni kwa sababu hiyo, naomba niwataje baadhi ya viongozi na wahusika wengine walioshiriki kumdanganya Waziri Mkuu. Hapa kuna Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo; Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Rashid Mfaume; na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, Michael Lekule.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, kinadharia anaonekana mwenye nia njema katika kuumaliza mgogoro huu, lakini ukweli wa mambo sivyo. Gambo ameshakuwa rafiki mkuu wa NGOs, na hasiti kulisema hilo hadharani. Hoja hapa si yeye kujenga uadui na NGOs, la hasha, bali kinachotakiwa ni yeye, kama alivyo Waziri Mkuu, kutambua kuwa kuna NGOs zinazoendeshwa kihuni kwa maslahi ya kudumisha migogoro ili wahusika waendelee kuvuna fedha kutoka kwa wafadhili. Kigezo kikuu kinachotumiwa hapa ni kuwa NGOs zinawatetea wananchi, jambo ambalo si la kweli.

Gambo ameshakuwa rafiki mkuu wa kampuni ya AndBeyond, na katika ziara yake aliyoifanya Loliondo Agosti 2016 hakusita kuposti kwenye mtandao wake maneno haya: “Kampuni ya AndBeyond peke yake mwezi uliopita wamelipa kodi bilioni 3 (akimaanisha Sh bilioni 3)”. Taarifa hii si ya kweli na bila shaka alimpa Waziri Mkuu. Kiasi hicho cha kodi ni kikubwa mno kulipwa na Klen’s Camp pekee kwa mwezi! Pengine kinajumuisha maeneo yote matano ya AndBeyond. Mengine ni Ngorongoro Crater Lodge, Under Canvas Serengeti, Mnemba Lodge na Manyara Trees Lodge. 

 

Ukweli wa mambo 

Kijiji cha Ololosokwan kimeingia mkataba na Kampuni ya AndBeyond Limited kwa ajili ya kuendesha shughuli za utalii wa picha katika eneo lenye ekari 25,000. Kampuni ya AndBeyond Limited imekuwa ikifanya shughuli za utalii wa picha katika eneo hilo tangu mwaka 1996 hadi sasa. 

Kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori Na.5 ya mwaka 2009, eneo lote la Tarafa ya Loliondo na sehemu ya Tarafa ya Sale linatambulika kama Pori Tengefu la Loliondo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 4,000. Eneo hili ni kitalu cha uwindaji cha daraja la kwanza (ingawa sasa kinastahili kuwa daraja la tatu) ambayo kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC) kimepewa dhamana ya kuwinda. 

Pamoja na eneo hilo kutambulika kama kitalu cha uwindaji, bado kumekuwapo vijiji vilivyoingia mikataba na kampuni nyingine za utalii wa picha. Miongoni mwa vijiji hivyo ni Ololosokwan ambacho kimeingia mkataba na AndBeyond Klein’s Camp.

Kampuni ya OBC walipewa kitalu hiki kwa ajili ya shughuli za uwindaji wa kitalii. Pamoja na kwamba OBC ndiyo inayomiliki eneo hilo, kumekuwapo mkanganyiko mkubwa katika matumizi ya pori hili, jambo ambalo limesababisha vijiji kuingia mikataba na kampuni nyingine zinazofanya shughuli za utalii wa picha.

Kampuni ya AndBeyond na Kijiji cha Ololosokwan waliingia mkataba wa kukodisha eneo la ekari 25,000. Hata hivyo, eneo hilo lipo ndani ya Pori Tengefu Loliondo ambalo ni kitalu cha uwindaji cha OBC. Hii ina maana uwindaji wa picha wanaoufanya, hauratibiwi na mamlaka za Serikali moja kwa moja katika Pori Tengefu. Hali ni tofauti katika Hifadhi na Mapori ya Akiba ambako kuna mamlaka za Serikali zinazokusanya maduhuli. Kwa hali ilivyo sasa, AndBeyond na kampuni nyingine za aina yake katika Loliondo, hazilipi maduhuli kama inavyopasa kisheria. Hili sharti litazamwe na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Shughuli za utalii zinazofanywa na AndBeyond ni pamoja na matembezi ya wageni, matembezi kwa magari, utalii wa kiutamaduni na matembezi ya magari usiku.

Kampuni ya AndBeyond imekuwa ikilipa kijiji cha Ololosokwan fedha za mkataba kutokana na makubaliano yao wenyewe. Kutokana na mkataba huo, hakuna kiasi cha fedha ambazo Serikali Kuu, au Halmashauri ya Wilaya inapata kutoka na mkataba huo. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kampuni ya AndBeyond ililipa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro Sh milioni 13 tu.

Kwa miaka mitatu iliyopita kampuni hiyo, kulingana na mkataba wake na Kijiji cha Ololosokwan, imekilipa Sh 880,941,990.00. 

Kampuni ya AndBeyond imekuwa ikitamba kuwa imejenga Kituo cha Afya na Kituo cha Polisi vyenye kiwango kijijini Ololosokwan. Waziri Mkuu alidanganywa kwa kuambiwa Kituo cha Afya kina mashine nzuri na za kisasa, hata akatamani afike azione. Alionekana kufurahia taarifa hiyo, lakini hakujua anadanganywa! Hospitali Teule ya Wasso ambayo ina vifaa na inatoa huduma nzuri kwa msaada mkubwa wa OBC, viongozi wa wilaya na mkoa hawakutaka akanyage huko kabisa. Walijua kama angefika na kuona ilivyo, angeipongeza OBC ambayo tayari ni mbaya wa DC na RC!

 

Alidanganywa

Mosi, Kituo cha Afya kipo barabarani kabisa, kwa hiyo, kama kingekuwa na sifa hizo nzuri, angepitishwa hapo kujionea ‘uzuri’ huo kabla ya kupelekwa katika Kituo cha Utamaduni kilichojengwa kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). Ukweli ni kuwa kituo hicho kimejengwa chini ya kiwango. Kuta zake zina nyufa kubwa. Mashine ambazo Gambo anamdanganya Waziri Mkuu zimewekwa na AndBeyond, zilitolewa msaada na UNESCO.

Kuthibitisha hilo, Kituo cha Afya hicho kilipojengwa chini ya kiwango, uongozi na wananchi wa Ololosokwan wakagoma kukipokea. Kikafanyiwa marekebisho, na kwa mara ya pili wananchi na uongozi wa kijiji wakagoma kukipokea. Mara ya tatu marekebisho yalipofanywa, ndipo walau wananchi wakakubali kukipokea kwa shingo upande.

Wakati huo, UNESCO walishafikisha msaada wa kompyuta, vifaa vya umeme-jua na hiyo mitambo ya afya. Ikaonekana ni vema mitambo hiyo iwekwe kwenye majengo hayo ‘machovu’ ili isiendelee kuharibika ndani ya makontena. Hiki ndicho Waziri Mkuu alichoambiwa kwa mbwembwe kuwa ni kituo cha kisasa chenye mashine za kisasa!

Pili, Kituo cha Polisi kipo njiani – kando ya barabara iliyotumiwa na Waziri Mkuu. Kama kingekuwa na ubora, Gambo angesimamisha gari japo kwa dakika 5 ashuhudie ‘uzuri’ huo. Hakufanya hivyo. Kituo hiki ni kichovu mno. Askari wanalala humo humo! Hii ni aina ya misaada ya kuwadhalilisha Watanzania.

Uswahiba wa Gambo kwa AndBeyond umeenda mbali zaidi. Mara kadhaa amepewa ofa ya kulala bila malipo katika hoteli ya Klen’s Camp ambayo ni ya kifahari. Sidhani kama kuna Mzungu mwekezaji anayeweza kuwa mkarimu wa kukubali kutoa vyumba vya mamilioni ya shilingi kwa Mkuu wa Mkoa na ujumbe wake bila kuwa na matarajio ya kulipwa fadhila. Wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Gambo alilala hapo katika chumba ambacho gharama yake si chini ya Sh milioni 2 kwa usiku mmoja!

Pale Ololosokwan kwenye mkutano wa hadhara, Gambo alimshangaa Naibu Waziri wa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi, ole Nasha, ambaye ni Mbunge wa Ngorongoro, kwa kushindwa japo kuwataja na kuwasifu AndBeyond.

“Nilidhani atazungumzia AndBeyond na changamoto ya ardhi, nilidhani mbunge atalisemea hilo, lakini itifaki imembana,” alichomekea Gambo.

AndBeyond wanajua wanachokifanya na wanajua wanachokitafuta kutoka kwa Gambo. Tayari wameshampa maombi mazito na yeye amewaahidi kushughulikia ombi lao la kufunguliwa kwa uwanja wa ndege waliokuwa wakiutumia kabla ya kufungwa na mamlaka za Serikali kwa sababu za kiusalama.

Uwanja huo upo kilometa chache kutoka mpaka wa Tanzania na Kenya. Ulifungwa baada ya kuwapo taarifa zisizotiliwa shaka kuwa hapakuwapo uratibu wowote, hali iliyotia shaka uingiaji na utokaji wa wageni waliopitia Kenya na mataifa mengine.

Sasa, baada ya kumpata rafiki Gambo, AndBeyond wanahaha uwanja huo ufunguliwe haraka. Wanatoa sababu zao. Wanasema uwanja ulio karibu ni ule wa Lobo wageni hutumia saa moja na dakika 50 kwa magari kufika Klens Camp. Wanalalamika kuwa TANAPA hawafanyi matengenezo ya barabara, kwa hiyo wageni wao huchoka mno, na kwamba endapo uwanja wao utafunguliwa, watasafiri kwa magari kwa dakika 15 tu.

Wanasema kuwapo uwanja eneo hilo kutasaidia kutangaza utalii na kuongeza wageni watakaozuru huko, wanasema kufunguliwa kwake ‘kutainua’ uchumi Wilaya nzima ya Ngorongoro; eti wataongeza ulinzi katika eneo la Ngorongoro na kadhalika.

“We see NO down side to opening the Klen’s Camp airstrip for your investors, community and the district,” wanasisitiza.

Taarifa kutoka mamlaka mbalimbali zinaonesha kuwa Gambo ameshaanza kazi ya kuhakikisha uwanja huo unafunguliwa, licha ya sababu za kuufunga kuwa bado ziko palepale.

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mfaume, awali alionekana kutambua thamani ya uhifadhi katika Loliondo, lakini kwa mambo yalivyo sasa ni kwamba wameamua kutekeleza maagizo ya Mkuu wa Mkoa.

Mfaume akitambua kwa asilimia 100 namna mazingira yalivyoharibiwa, hakutaka Waziri Mkuu apite katika vijiji vya Karkamoru, Oloipir au Kirtalo. Kama Waziri Mkuu angepita katika vijiji hivyo wakati akitoka uwanja wa ndege, angeona matrekta zaidi ya 50 kutoka Kenya yanavyolima katika eneo la hifadhi ya Karkamoru. Angejionea maelfu kwa maelfu ya ng’ombe na ukataji miti unavyofanywa. Angeona kanisa lililojengwa katikati ya pori mbali na wananchi – yote ikiwa kujihalalishia makazi katika eneo la uhifadhi.

DC Mfaume hata nafsi yake inatambua kuwa walimdanganya Waziri Mkuu kuhusu kile kilichoitwa ‘Taarifa ya Kamati Teule kwa ajili ya kuratibu maoni na mapendekezo ya wananchi namna ya kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi na kuboresha uhifadhi katika kata saba zinazopakana na Hifadhi ya Serengeti.’

Mfaume anatambua fika namna taarifa hiyo alivyoshiriki kuiandaa yeye kwa maelekezo ya RC Gambo, kisha akapewa Diwani wa Ololosokwan, Yanik Ndoinyo, amsomee Waziri Mkuu pale Ololosokwan katika Kituo cha Utamaduni kilichojengwa na UNESCO.

Hata Waziri Mkuu alipomwuliza Ndoinyo; “Taarifa hii ni ya wananchi?” naye akajibu; “ndiyo”; alikuwa akimdanganya kiongozi huyo wa shughuli za Serikali. Mfaume anajua hata wakati Ndoinyo akiisoma taarifa ile alikuwa akisitasita kwa sababu yaliyomo si yeye Diwani wala wananchi walioyaandaa. Na zaidi ya yote, Ndoinyo si mmoja wa wajumbe kwenye Kamati Teule. 

Mfaume anajua fika kuwa taarifa ile ya Kamati Teule haikuandaliwa na wawakilishi wa vijiji 15 ndani ya kata saba. Walioshiriki mkutano wa Novemba 9, 2016 katika Ukumbi wa Domell, Wasso wanajulikana.

Kamati Teule inatajwa kuwa na wajumbe 16 ambao ni Raphael Long’oi (Mwenyekiti/Losoito), Kashanga Pusalet (Oloirien), Ikayo Mbalala (Oloipir), Kinyanjui Kimirial (Soitsambu), Mshao Naing’isa (Ololosokwan), Maanda Ngoitiko (PWC), Gabriel Kilel (KIDUPO), Pirias Kilel, Tina Timan, Lanoi Munge (Arash), Justin Nakoren (Piyaya), Fredy Ledidi (Katibu/Halmashauri), Samwel Naing’iria (NGONET), Nganana Mothi (Halmashauri), Teresia Irafay (Halmashauri) na Elibariki Bajuta (Halmashauri).

Wiki iliyopita, waliongezwa wajumbe wengine wanne wakiwamo Ole Tiamasi (Diwani Katete), Parisiana, Philipo na mwingine ambaye sikupata jina lake.

RC Gambo na DC Mfaume wamweleze Waziri Mkuu, wasifu wa kila mjumbe katika hii kamati halafu tupime kama kweli hiyo kamati itatoa jibu la kudumu la uhifadhi Loliondo!

Lakini waeleze pia namna wajumbe hao walivyopatikana. Wasipomweleza, mimi nitakuwa na wajibu huo!

 

Hitimisho:

 Nimewataja Gambo na Mfaume kama viongozi ambao hawakumweleza ukweli Waziri Mkuu. Makala zitakazofuata nitaeleza nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Lekule, na Nasha kwenye mgogoro huu wa Loliondo.

Mgogoro wa Loliondo hauwezi kumalizwa kama viongozi wa Serikali wanakuwa kinyume cha matakwa ya kisheria na uhifadhi.

Ilivyo sasa, RC Gambo ameshashikana urafiki na NGOs ambazo lengo lake kuu si uhifadhi, bali kuchuma mapato kutokana na migogoro inayopikwa na kuendelea Loliondo. 

Wakitambua kuwa NGOs hizi miongoni mwazo zitafutwa kutokana na kuendesha mambo yake kinyume cha yale waliyoomba wakati wa usajili, sasa zinahimiza wananchi walime kwa kasi kabisa katika Kijiji cha Karkamoru. Tena kasi hiyo imeongezeka baada ya Waziri Mkuu kuhitimisha ziara yake Ngorongoro.

Endapo Serikali itathubutu kuwaondoa, NGOs zitakuwa na ajenda mpya ya kuuhadaa ulimwengu kuwa Wamaasai wanaondolewa kwa nguvu katika ardhi yao. Hawatasema wanaondolewa ili kulinda mazingira na roho ya Serengeti kiikolojia! Kelele hizo zitawasaidia kuendelea kuvuna mabilioni ya shilingi kutoka kwa wafadhili. 

Hivi sasa kuna baadhi ya wenye NGOs wanaosomesha watoto katika shule ambayo ada kwa mwaka ni Sh milioni 52! Yupo mmoja ana watoto watatu. Anawalipia shilingi zaidi ya milioni 150 kwa mwaka. Katika hali ya kawaida, kiasi hicho cha fedha ni kikubwa mno! Wanatoa wapi hizo fedha kama si kwa migogoro hii ya Loliondo? Je, nani yuko tayari kukosa fedha hizo, na hivyo wanawe wasome shule za kata? Hakuna.

Tumewasikia viongozi wakuu wakikemea urukaji na utuaji ndege holela katika migodi. Hifadhi ni migodi mingine yenye manufaa makubwa kuliko hata ile ya dhahabu! Utalii na uhifadhi kwa jumla ndilo eneo linaloongoza kwa kuliingizia Taifa letu mapato ya fedha za kigeni kuliko dhahabu na madini mengine. 

Tunaweza kuwafurahisha wananchi kwa kuruhusu wavuruge na hatimaye waue kabisa uhifadhi, lakini tuwe tayari kukubiliana na matokeo ya uamuzi huo.

Hata kama Loliondo yote watakabidhiwa wananchi, haitawatosha. Hata wakipewa Serengeti yote, bado itakuwa haitoshi! Kilichopo, kama alivyosema Waziri Mkuu, ni kusimamia matumizi bora ya ardhi kwa kutenga maeneo ya misitu, maeneo ya hifadhi na maeneo ya kilimo. Siasa nyepesi nyepesi hizi za kuruhusu kuua mahali ambako asilimia 48 ya maji yote ya Serengeti yanapatikana, ni kukaribisha janga na hatimaye kuua uhifadhi.

 

>>ITAENDELEA

By Jamhuri