Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu watu 11 ambao ni wakazi wa Ifakara, mkoani Morogoro kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh. Milioni 6 kwa kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutoa taarifa za uongo mtandaoni.

Washtakiwa hao ni Fredrick Kanepela, Julius Mwabula, Amiry Luwiso, Tareeq Sadrudin, Ashraf Awadhi, Frank Kifyoga, Samson Tandike, Michael Haule, Mussa Maganga, Helman Lwambano na Kelvin Mkapila.

Hukumu hiyo ilitolewa Machi 26, Mwaka huu Mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Mwandamizi Annah Magutu baada ya washtakiwa hao kusomewa na kukiri mashtaka yanayowakabili.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mwandamizi Magutu amesema hukumu hiyo imetolewa kwa washtakiwa 11 kati ya washtakiwa 23 wanaokabiliwa na kesi hiyo.

Amesema washtakiwa hao 11 waliohukumiwa waliomba kuingia makubaliano ya kumaliza kesi kwa kukiri makosa yao yaani ‘pre bargain’.

Awali washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao na jopo la mawakili wa serikali ambao ni Neema Moshi, Royda Mwakamele, Titus Aron, Cathbert Mbilingi na Winniwa Kassala.

Moshi amedai kuwa washtakiwa hao wakiwa na nia ovu walitoa taarifa za uongo mtandaoni na kufanikiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Amedai kuwa washtakiwa hao ambao maarufu kama ‘Halo halo’ walitoa taarifa za uongo wakitumia ujumbe usemao “Nitumie hiyo hela kwenye namba hii”.

Amedai kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti tofauti Ifakara, Mkoani Morogoro ambapo washtakiwa hao walikula njama na kutuma jumbe za kitapeli kwa nia ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutoa taarifa za uongo mitandaoni.

Inadaiwa kuwa washtakiwa hao wamekuwa wakiwatumia wananchi mbalimbali jumbe za simu za kitapeli pamoja na kupiga simu huku wakidai wao ni wafanyakazi wa makampuni ya simu na kuwatapeli wananchi fedha zao.

Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka yanayowakabili walikiri kutenda makosa hayo ndipo Hakimu Maguta alitoa adhabu hiyo.

Washtakiwa watano ambao ni Fredrick Kanepela, Julius Mwabula, Amiry Luwiso, Tareeq Sadrudin na Ashraf Awadhi waliridhia kulipa faini ya Tsh milioni 6 kwa kila mmoja.

Washtakiwa wengine sita akiwemo Frank Kifyoga, Samson Tandike, Michael Haule, Mussa Maganga, Helman Lwambano na Kelvin Mkapila walipewa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela kila mmoja baada ya kushindwa kulipa faini hiyo.

Hata hivyo shauri hilo bado linaendelea mahakamani kwa washtakiwa wengine 13 waliosalia ambao hawakukiri makosa yao.

By Jamhuri