Na Cresensia Kapinga ,JamhuriMedia, Songea

Wafanyabiashara 13 wamefariki na wengine wawili wamejuruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutumbukia mto Njoka wakati wakitoka Ndongosi mnadani kuelekea kijiji cha Namatuhi wilayani Songea mkoani Ruvuma.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 10, 2023, kwenye eneo la chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo Hospitali ya Serikali ya Mkoa Songea (HOMSO), Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Marco Chily,a amesema kuwa ajali hiyo imetokea majira ya saa 3, usiku katika eneo la daraja la Mto Njoka Namatuhi katika barabara ya Ndongosi iendayo Namatuhi Songea vijijini.

Mganga Mfawidhi wa Hospital ya Mkoa wa Songea (HOMSO), Dkt Magafu Majur , akizungumza na waandishi wa habari kwenye chumba cha kuhifadhia maiti .

Amesema kuwa gari hilo lenye namba za usajili T 800 BXB, Mistubish Fusso, lililokuwa likiendeshwa na dereva Thobias Njovu, lilipofika kwenye eneo la daraja hilo na wakati linapanda mlima ghafla liliacha njia na kutumbukia mtoni .

Amewataja wafanyabiashara walifaofariki kwenye ajali hiyo kuwa ni Happy Msemwa, Jafari Ngalimus, Hidaya Salum,Biesha Yahaya ,Mustafa Ally, wengine wamefahamika kwa jina moja moja ambao ni Mwaisha, Hamad, Juma Said ,Boniface, Christofa Msuya.

Wengine ni Deograsia Mapunda, Simba na mama Faraja ambapo majeruhi ni Hamis Mbawala na Christofa Banda ambao wamelazwa katika kituo cha afya cha Mpitimbi.

Kamanda amesema kuwa maiti zimehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Serikali ya Mkoa wa Songea.

Aidha Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma linaendelea kusisitiza wananchi kuacha kupanda magari ya mizigo wanapokuwa wanakwenda kwenye minada hivyo Polisi hawatosita kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayekiuka agizo hilo.

Baadhi ya wananchi waliofika kutambua miili ya ndugu zao kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika hospital ya serikali ya Mkoa wa Songea (HOMSO)

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Serikali ya Mkoa wa Songea (HOMSO), Dkt.Magafu Majura amesema kuwa amepata taarifa ya ajali majira ya saa 8, usiku ya kuamkia leo Aprili 10.

Amesema kuwa kwa kushirikiana na timu ya madaktari pamoja na wauguzi walijipanga na kufika kwenye chumba cha kuhifadhia maiti ambako walipokea miili ya watu 13 kati yao wanawake saba na wanaume sita.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akiwa ameongozana na kamati za ulinzi na usalama za mkoa na wilaya walifika kwenye eneo la kuhifadhia maiti ambako umati mkubwa wa wananchi walifika kwa nia ya kutambua ndugu zao.

RC huyo amesikitishwa na tukio hilo ambalo baada ya kupata taarifa ilimlazimu kufika Hospitali ya Mkoa Songea usiku wa majira ya saa 8 na kushirikiana na madaktari pamoja na wauguzi.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma Marco Chilya, akitoa taarifa ya vifo vya watu 13 na majeruhi wawili katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Amesema Serikali ilishatoa katazo muda mrefu la wafanyabiashara wanaokwenda kwenye minada kuacha kupanda gari zenye mizigo kwani imekuwa ikichangia kupoteza nguvu kazi ya taifa.

Mmoja wa ndugu wa marehemu wa ajali hiyo Nestory Nyanguru,mkazi wa Subira kati, Manispaa ya Songea akiongea na waandishi wa habari nje ya chumba cha kuhifadhia maiti amesema kuwa taarifa ya tukio hilo aliipata jana majira ya saa 5 usiku kuwa mdogo wake amepata ajali amepelekwa katika Hospitali ya Serikali ya Songea ambako aliutambua mwili wa mdogo wake.

Please follow and like us:
Pin Share