Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Katika mwamko mpya wa kuipeleka Dodoma kimataifa na kuileta dunia Dodoma, Serikali imezindua Mpango Mkakati wa Kuendeleza Utalii wa Mkoa wa Dodoma huku ikipendekeza kuanzishwa kwa Kijiji cha Utalii wa Wagogo kitakachohifadhi na kuonyesha nyimbo, mavazi, mapishi na maisha ya jadi ya kabila hilo.

Akizungumza katika uzinduzi huo Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo, amesema mkakati huo ni sehemu ya majibu ya kiu ya muda mrefu ya kuitangaza Dodoma kimataifa kupitia vivutio vyake vya kipekee na kwamba huu si wakati wa maandiko ya mipango pekee, bali ni hatua ya utekelezaji unaopaswa kuibadilisha Dodoma kiuchumi na kijamii.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa,Jafo ameeleza kuwa Dodoma imebarikiwa vivutio vya asili, historia na utamaduni vinavyoweza kutumika kama nyenzo ya kukuza uchumi wa taifa kupitia utalii.

Ameeleza kuwa kuanzishwa kwa Kijiji cha Utalii wa Wagogo itakuwa ni jukwaa la kipekee la kuonesha utajiri wa mila na desturi za Wagogo, ambapo Kupitia kijiji hiki, wageni wa ndani na nje ya nchi watapata fursa ya kujifunza kuhusu maisha ya jadi ya Wagogo, ikiwa ni pamoja na nyimbo za asili, mavazi ya kitamaduni, mapishi ya kienyeji na shughuli mbalimbali za kila siku.

“Kijiji hiki kitakuwa zaidi ya kivutio cha utalii; kitakuwa pia sehemu ya elimu na urithishaji wa utamaduni kwa vizazi vijavyo ambapo maudhui yake yatalenga kulinda na kuendeleza utambulisho wa Wagogo, ambao umekuwa ukitishiwa kutoweka kutokana na mabadiliko ya kisasa, “amesema.

Amesema hatua hiyo pia inatarajiwa kuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi kwa wakazi wa maeneo ya karibu, kwani itafungua fursa za ajira, biashara ndogondogo na miradi ya kijamii.

Amesisitiza kuwa bidhaa kama mchuzi wa zabibu, mvinyo wa asili, historia ya wapigania uhuru na maeneo ya urithi wa taifa ni tunu ya kuiweka Dodoma kwenye ramani ya dunia.

“Mkakati huu si tu waraka wa maono, bali ni chombo cha mageuzi kwa mkoa huu,” amesema.

Akibainisha nafasi ya miundombinu katika kufanikisha lengo hilo, Waziri Jafo amesema Serikali inatarajia kukamilisha kwa wakati ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, ambao utakuwa lango la moja kwa moja kwa watalii wanaoingia kutoka mataifa mbalimbali.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa SGR na maeneo yanayozunguka vituo vya treni kuandaliwa kitalii ili kutoa taswira ya mkoa wenye utambulisho wa kiutamaduni na kiutalii kwa wageni wa ndani na nje.

Ameongeza kuwa mapishi ya kienyeji, mavazi ya asili, lugha na tamaduni za Wagogo, Warangi, Wasandawe na Waburunge ni hazina ambayo inapaswa kutumika kama bidhaa ya kitalii.

“Utalii unaanza na wewe,” aliongeza, akisisitiza kuwa kila mwananchi anayo nafasi ya kuwa balozi wa utalii kwa kuenzi, kutunza na kutangaza vivutio vya eneo lake.

Aidha, ameeleza kuwa mkakati huo unahitaji mshikamano wa wadau wote wakiwemo sekta binafsi, viongozi wa serikali, vijana na jamii kwa ujumla.

“Hii si kazi ya serikali peke yake,tunahitaji kila mdau kushiriki kwa vitendo katika kuijenga Dodoma mpya mji wa urithi, fursa na utalii endelevu,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amesema mkakati huo umejengwa katika msingi wa kuitumia kaulimbiu ya “Ipeleke Dodoma Kimataifa, Ilete Dunia Dodoma” kwa vitendo.

Amesema mkoa huu unazo rasilimali nyingi za asili na historia ambazo bado hazijatumika ipasavyo, ikiwemo misitu ya hifadhi ya Swagaswaga na Mkungunero, historia ya Kongwa kama makazi ya wapigania uhuru, pamoja na majengo ya kihistoria kama Ikulu ya zamani na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Senyamule amesisitiza kuwa utalii wa kilimo ni miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa kwa Dodoma, akieleza kuwa zabibu na mashamba yake yanaweza kutumika kama vivutio vya kipekee kwa watalii wa ndani na nje, wajasiriamali na watafiti.

Pamoja na mambo mengine katika kuhakikisha mafanikio ya mkakati huo, Serikali imesema itaendelea kuweka miundombinu wezeshi, kurahisisha mifumo ya uwekezaji, kutoa vibali kwa wakati na kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wote wa sekta ya utalii.