Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

BONDIA Abdul Zugo wa Tabora ameahidi kumpiga kwa KO bondia kutoka India, Sameer Kumar katika pambano lao la Ubingwa wa Dunia la uzito wa kati litakalofanyika kesho katika ukumbi wa Orion Hotel Mjini Tabora.

Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kupima uzito wao leo asubuhi mjini hapa, Zugo amesema kuwa amejiandaa vizuri kwa pambano hilo na ameahidi kumchapa mpinzani wake kwa KO katika raundi ya pili au ya tatu.

Zugo amebainisha kuwa hadi sasa ameshacheza mapambano 18 ndani na nje ya nchi na ameshinda jumla ya mapambano 15, ameshinda kwa KO mapambano 13, sare 2 na kupoteza 1.

‘Naushukuru Uongozi wa Mkoa chini ya Mkuu wa Mkoa Paul Chacha na Mkuu wa Wilaya Upendo Wella, kwa sapoti kubwa wanayonipa, katika pambano hili nawaahidi kuwa nitamwadabisha mpinzani wangu, nimejiandaa vizuri ’, amesema.

Ameeleza kuwa mpinzani wake Sameer Kumar kutoka India ni bondia mzuri lakini atamwonesha kuwa yeye ni bora zaidi, hivyo wapenzi wake watarajie pambano la ubingwa wa dunia lenye msisimko wa hali ya juu.

Pambano hilo linaloandaliwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Duniani (WPBF), litapigwa kesho katika ukumbi wa Orion Hotel Mjini hapa na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa huo Paul Chacha.

Pambano hilo litatanguliwa na mapambano 15 ya utangulizi likiwemo pambano la Karim Mandonga (mtu kazi) dhidi ya Juma Farahani wa Tabora yakiwemo mapamabno 2 ya wanawake.

Akizungumzia pambano hilo, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Upendo wella amewataka wakazi wa Manispaa ya Tabora na Wilaya zote kujitokeza kwa wingi kushuhudia pambano hilo na kumpa sapoti kijana wao.

Ili kuhakikisha Zugo anafanya vizuri katika pambano hilo DC amemkabidhi kitita cha sh milioni 10 zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa kama motisha ya kufanya vizuri na kushinda mkanda huo unaotambuliwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Duniani (WPBF).