Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Mohammed Ali Kawaida amezindua rasmi Mfumo wa Kijani Ilani Chatbot ambao utawarahisishia vijana kupata taarifa kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 na ahadi za mwaka 2025-2030 kupitia simu zao mahali popote walipo.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo, Kawaida alisema mfumo huo ni nyenzo muhimu ya kidigitali inayowawezesha vijana na wananchi kwa ujumla kufahamu kwa urahisi namna Chama na Serikali yake ya Awamu ya Sita zinavyotekeleza ahadi zilizotolewa kwa Watanzania.

“Kijani Ilani Chatbot itawaonyesha vijana wa Kitanzania na Watanzania wote utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa 2020-2025 na pia kueleza mambo yaliyoahidiwa katika Ilani ya mwaka 2025-2030, hususan kwa upande wa vijana,” alisema Kawaida.

Aidha aliwasihi vijana kutumia kikamilifu mfumo huo ili kupata majibu ya moja kwa moja kuhusu Ilani ya CCM, miradi ya maendeleo na hatua za utekelezaji wake, badala ya kutegemea taarifa zisizo sahihi kutoka kwa watu wenye nia ya kupotosha umma.

“Twendeni tukautumie mfumo huu kuondoa upotoshaji unaofanywa na watu wasiokuwa na mapenzi mema na taifa letu kwa kuwaambia Watanzania ukweli,” aliongeza.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Halid Mwinyi, alisema mfumo huo wa kidigitali ni wa kisasa na unatoa fursa ya mawasiliano ya moja kwa moja baina ya mtumiaji na mfumo, ambapo kila kijana ataweza kuuliza swali na kupata majibu kwa haraka na kwa urahisi.

“Mfumo huo unalenga kutoa taarifa sahihi, kwa wakati na kwa njia ya kidigitali kuhusu Ilani ya CCM na miradi ya maendeleo, kuwezesha vijana kuuliza maswali na kupata majibu ya papo kwa papo, kuongeza uelewa wa vijana kuhusu nafasi yao katika maendeleo ya taifa na ushiriki wa kisiasa pamoja na kukuza matumizi ya teknolojia ya akili mnemba (AI) katika elimu ya siasa na utawala bora,” alisema Mwinyi.

Alisisitiza kuwa kupitia Kijani Ilani Chatbot, vijana watapata maarifa mapya kuhusu siasa, maendeleo na wajibu wao katika kujenga taifa imara na lenye mshikamano.