Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Kibiti

Ndugu zangu Watanzania, leo nimeona niwaandikie kwa uwazi, kwa uchungu na kwa upendo wa dhati juu ya kinachoendelea hapa nchini.

Jumapili iliyopita nimefuatilia kwa karibu mahubiri ya viongozi wengi wa dini makanisani. Wamehubiri siku mbili kabla ya leo siku ya Uhuru Desemba 9, 2025. Wamehimiza amani, upendo na mshikamano. Ujumbe huu ulikuwa muhimu mno katika kipindi hiki.

Nafahamu tumepitia misukosuko. Nikiri nami kama wengi ilivyokuwa, ni mmoja wa tuliowaza kuwa Oktoba 29, 2025 yasingetokea maandamano.

Maandamano yale kwa sura yoyote ile yanayoitwa, wengine wanayaita maandamano, wengine wanayaita vurugu. Mimi nasema kwa lugha au sura yoyote ile yanayoitwa, bado madhara yake yamekuwa makubwa kwa taifa letu. Hasara iliyopatikana ni kubwa kuliko tulivyotarajia.

Sitanii, mimi nazungumza na watu wengi. Kuanzia wazee hadi vijana na watoto. Jamii naitumikia mitaani hadi kanisani. Napata fursa ya kusikia. Nimewasikia vijana. Naendesha mijadala mbalimbali. Nafuatilia lugha ya serikali na watendaji wake. Nafuatilia lugha za vijana, ‘memes’. Hizi za hoyaaaaaa, niyaje? Na nyingine zaidi ya hizo zinazotumika mtandaoni kutambulisha sikukuu za kidini na nyingine.

Nimeguswa na taarifa ya Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, kuwa vituo vya mafuta 672 vimechomwa moto. Sitaji orodha ya vitu vingine vingi vilivyoharibiwa. Nimejiuliza, kama vituo idadi hiyo vimechomwa moto, ina maana kama kila kituo kinaajiri vijana 10, ambayo ndiyo namba ya chini kabisa.

Vituo vya mafuta mara nyingi kwa sababu ya ‘shift’ vina waajiriwa 10 kila kimoja. Sote ni mashahidi. Wauzaji katika vituo vya mafuta ni vijana. Kwa vituo 672 kuchomwa moto, ina maana vijana 6,720 waliokuwa wameajiriwa na vituo hivyo, kwa sasa wapo nyumbani. Ajira zao zimechomwa moto. Natamani tuwaze kwa utulivu. Ajira ni tatizo si kwa Tanzania tu, bali dunia nzima. Vijana ndio wahanga wakubwa wa tatizo hili. Je, tunalimaliza kwa kuharibu hata hizo chache zilizopatikana au kwa kuweka pamoja juhudi kupata ufumbuzi?

Sitanii, tumekuwa tukisikia miito ya maandamano mara kwa mara. Wapo wanaochochea, wapo wanaopotosha, na wapo wanaotumia hamasa za ujana kama daraja la kufanikisha malengo yao.

Lakini msione giza la mbali mkasahau mwanga wa nyumbani. Maisha yetu, nchi yetu na mustakabali wetu ni vitu vya thamani kuliko hisia za muda mfupi.

Vijana, maandamano si mchezo. Kwenye maandamano, hakuna anayekuhakikishia usalama. Historia imeonyesha mara nyingi kuwa maandamano huishia na machozi, majeraha, vifungo, uharibifu wa mali, na wakati mwingine vifo. Hivi unadhani wale wanaokupa hamasa watakuwa mstari wa mbele wakati risasi za tahadhari zikipigwa? Hapana. Mara nyingi wanaosukumwa ndio wanaoanguka, lakini wachochezi wao huwa salama wakiwa majumbani wakifuatilia habari.

Sitanii, Tanzania imebarikiwa. Tunaishi kwenye nchi ambayo dunia inaitazama kama kisiwa cha amani. Huu ni urithi uliolindwa kwa miaka zaidi ya 60. Amani haikujitokeza tu; imejengwa kwa hekima za wazee, busara za viongozi na ustahimilivu wa wananchi. Amani ndiyo inafanya Watanzania wapate habari, wakulima wakalime, wafanyabiashara wafanye biashara, na vijana kama ninyi kuwa na ndoto za kuendelea mbele. Bila amani, hakuna shule, hakuna ajira, hakuna biashara, hakuna maisha.

Wapo watakaowaambia maandamano ni haki. Ni kweli, lakini haki hii inakuja na wajibu mkubwa. Katika nchi nyingi, maandamano yamegeuka kuwa uwanja wa vijana kupoteza maisha, kukamatwa bila sababu za msingi. Je, unataka kesho ukifika kwenye usaili wa kazi uhojiwe kuhusu kushiriki vurugu? Je, unataka wazazi wako waishi kwa hofu kwa sababu mtoto wao yuko barabarani akipambana na askari? Fikiria hilo kwa makini.

Kama kuna jambo hamlikubali, Tanzania ina njia nyingi za kulitatua tatizo hili bila kuumiza mtu. Kuna majadiliano, mijadala, mikutano halali, malalamiko rasmi, na vyombo vya kisheria. Hakuna haja ya kuweka maisha rehani. Hakuna haja ya kugeuza barabara kuwa uwanja wa vita. Mabadiliko ya kweli yanakuja kupitia hoja, elimu, uvumilivu, na nguvu ya uvumilivu – si kwa mawe, si kwa fujo.

Sitanii, vijana, naomba mfahamu kuwa dunia ya leo inawahitaji muwe wabunifu, wajasiriamali, wanasayansi, walimu, wahandisi, na viongozi wa kesho. Msisahau kuwa nasi tulipata kuwa vijana. Nchi haiwezi kufika mbali ikiwa nguvu zenu zote zitaishia kwenye maandamano. Tanzania inawahitaji muweke nguvu zenu kwenye kushika kalamu, kujenga biashara, kuongoza mijadala yenye tija, na kutengeneza suluhu za changamoto zinazolikabili taifa.

Ndiyo maana nasema hivi, kila anayeona jambo haliendi vizuri, atusaidie kueleza nini kifanyike. Dhana kwamba namchukia fulani, haiwezi kututoa hapa. Tujenge hoja ya kipi kibadilishwe na kipi kiweje, hapo tutasonga mbele pamoja kama taifa. Nikiulizwa, nitakwambia tuchague amani. Tuchague busara. Tuchague kujenga badala ya kubomoa. Amani ya Tanzania ni urithi, lakini pia ni jukumu. Tuilinde amani na tuitunze.

Mwisho, nawaomba. Nimeona serikali imeunda hadi Wizara ya Vijana. Nimeziona juhudi za kuzungumza na vijana na watu na taasisi mbalimbali. Naamini tukichagua mkondo wa mazungumzo, kwa hapa tulipofikia na kusikilizwa ninakokuona, ufumbuzi utapatikana. Tusichague kuchoma kila tulichonacho tukidhani tutaanza upya. Geuka nyuma uangalie. Wanaotuhamasisha, wako salama. Je, sisi? Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827