Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepongeza hatua ya Hungary kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi na Tanzania, hasa kupitia utekelezaji wa miradi ya maji na maendeleo ya kijamii.
Pongezi hizo zilitolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, alipokutana na kufanya mazungumzo na Kaimu Balozi wa Hungary Nchini, Mhe. David Tòth, katika Ofisi za Wizara ya Fedha, jijini Dodoma.
Dkt. Mwamba aliishukuru Serikali ya Hungary kwa mchango wake mkubwa katika kukuza uhusiano wake na Tanzania, hasa kwa hatua ya hivi karibuni ya kufungua Ofisi ya Kidiplomasia jijini Dar es Salaam ambayo ni ishara ya dhamira ya dhati ya nchi hiyo katika kuimarisha uhusiano na Tanzania.
Aliongeza kuwa Serikali ya Tanzania inaithamini sana dhamira ya Hungary katika kufadhili miradi ya maendeleo ikiwemo Mradi wa Maji wa Biharamulo katika Mkoa wa Kagera, unaoendana kikamilifu na vipaumbele vya maendeleo ya Taifa vilivyoainishwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22–2025/26) pamoja na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.
“Utekelezaji wa mradi huu utaboresha huduma za maji safi kwa wananchi wa Biharamulo na maeneo jirani, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” alisisitiza Dkt. Mwamba.
Vilevile, Dkt. Mwamba alihimiza upanuzi wa mfumo wa ushirikiano wa kifedha kati ya Tanzania na Hungary ili kuhusisha pia misaada ya ruzuku (grant) kwa miradi ya kijamii na kiuchumi.
“Tunaishukuru Hungary kwa mikopo nafuu, na mfumo wa ushirikiano wa sasa kati ya nchi zetu umejikita zaidi katika mikopo nafuu, huku ukiwa na nafasi ndogo ya ufadhili wa ruzuku tungependa kuona upanuzi wa mfumo huu ili kujumuisha pia misaada ya ruzuku katika sekta muhimu za kipaumbele, ikiwemo huduma za jamii, miundombinu, na miradi ya kukuza uchumi, ambao utaimarisha zaidi uhusiano kati ya nchi zetu na kuongeza uwezo wake wa kuleta manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili” alisema Dkt. Mwamba.
Kwa upande wake, Mhe. David Toth, alieleza dhamira ya Serikali ya Hungary ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania, akisisitiza kuwa mradi wa maji wa Biharamulo ni mfano wa ushirikiano wa kimaendeleo unaolenga kuboresha maisha ya wananchi moja kwa moja.
“Hungary inaiona Tanzania kama mshirika muhimu wa maendeleo barani Afrika, na tumejizatiti kuunga mkono miradi inayogusa maisha ya wananchi, ikiwemo mradi huu wa maji wa Biharamulo ambao utaongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Kagera,” alisema Mhe. Toth.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, Kaimu Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Dkt. Remidius Ruhinduka, Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade, Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Bw. Melkizedeck Mbise, Mtaalamu wa Miradi ya Maji, Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya Hungary, Bw. Szabolcs Nagy na Maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha, na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.







