Na Mwandishi wetu,JamhuriMedia
Dar es Salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametangaza kuanzishwa kwa tuzo maalum zitakazotolewa kwa shule zitakazofanya vizuri katika matokeo ya jumla ya kitaifa, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuinua kiwango cha elimu na kuondoa ziro pamoja na matokeo duni mashuleni.
Chalamila ametoa kauli hiyo leo Februari , 2026, jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa PTA, wakati wa mkutano wake Mkuu na wadau wa sekta ya elimu uliohusisha Maafisa Elimu, Wakuu wa Shule, Waratibu wa Elimu pamoja na Wadhibiti Ubora wa Shule wa mkoa huo.
Amesema utoaji wa tuzo hizo unatarajiwa kuanza mwezi Aprili mwaka huu, na lengo ni kuchochea ushindani chanya baina ya shule, hali itakahamasisha Waalimu kubuni mikakati madhubuti ya kuboresha ufaulu wa wanafunzi.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha kuwa Serikali inaendelea kufanya tathmini ya kina kubaini sababu za matokeo yasiyoridhisha, akisisitiza kuwa si sahihi kuwalaumu wanafunzi pekee, bali ni muhimu kuchunguza mifumo ya ufundishaji, mazingira ya kujifunzia pamoja na usimamizi wa elimu kwa ujumla.
Nilileta mfumo mwingine kwamba hawa wanaofeli tuwaangalie upya kwamba na wao tunafanyaje, kufeli kwa wanafunzi katika Shule kwani kuna sababu nyingi za kimazingira, taasisi, au masuala ya kifamilia”amesisitiza RC
Katika mkutano huo, Chalamila pia amewataka walimu kuhakikisha kunakuwepo na matumizi bora na muunganiko sahihi wa lugha, hatua itakayowawezesha wanafunzi kumudu lugha za kimataifa na lugha za biashara, hivyo kuongeza ushindani wao katika soko la ajira.

RC amesema matarajio na maono ya Serikali kwenye sekta ya elimu ni makubwa na ndio maana imekuwa ikitumia fedha nyingi kuelekeza katika maeneo mbalimbali, hivyo ni muhimu kwa walimu na wadau wengine wa elimu kutafsiri maono hayo kwa vitendo.
Pia amewataka wakurugenzi, maafisa elimu na wakuu wa idara ya elimu kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zimazowakabili walimu ili kuweza kutimiza malendo na maono ya Rais Dkt Samia kwenye sekta ya elimu
Kwa upande wake, Mratibu wa Tume ya Walimu, Subira Mwakibete, amesema tume hiyo inaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na nidhamu kwa watumishi wa elimu, kwa lengo la kuimarisha haki, uadilifu, uzalendo kazini pamoja na heshima kwa uongozi uliopo.
Ameongeza kuwa katika mwaka 2025, Tume ya Walimu ilipandisha vyeo walimu 3,612 na kuajiri walimu wapya 978, wakiwemo walimu 26 waliopangiwa kufanya kazi katika ngazi za maabara licha ya kutokuwa na taaluma ya ualimu.
Aidha Wito umetolewa kwa walimu na wadau wengine wa elimu kutafsiri vema maono ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri kwenye masomo yao na baadae wanapohitimu masomo ili kuwa na kizazi chenye tija.

