Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Leo nimetoka kanisani. Ni Dominika ya Februari 8, 2026. Najua makala hii itachapishwa gazetini siku ya Jumanne Februari 10, 2026. Somo kuu katika Injili, imehojiwa kuwa “Chumvi ikiharibika itatiwa nini?” Baba Moses Mbilinyi wa Parokia ya Misugusugu ndiye ametulisha neno leo. Ameeleza maneno makuu. Ametutaka Watanzania tupendane, tusaidiane.

Sitanii, mimi ni mdogo katika walio wadogo. Jana (Februari 7, 2026) nilipata fursa adhimu ya kushiriki mkutano kati ya waandishi wa habari na marais wawili; Dk. Samia Suluhu Hassan na Mzee Yoweri Kaguta Museveni. Marais hawa wamezungumza mambo mawili ya msingi. Kubwa ni kuimarisha uhusiano wa Tanzania na Uganda.

Kwa mujibu wa Rais Samia, yeye na Rais Museveni wamezungumza mambo mengi, yakiwamo ya historia ya ukombozi wa taifa letu.

Wamezungumza kuhusu kuondoleana vikwazo visivyo vya kikodi na masuala mengine yanayopuguza kasi ya ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na Uganda.

Najua Tanzania na Uganda zimo katika mchakato wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi (EACOP), linalotoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga.

Bomba hili linakwenda kukuza zaidi uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Uganda. Kwa kweli naomba kukiri kwa dhati kuwa sikupata kupitia takwimu za biashara kati ya Tanzania na Uganda kabla ya ziara hii ya wiki iliyopita ya Rais Museveni nchini Tanzania. Nafahamu Watanzania wengi watakuwa kama nilivyokuwa mimi.

Katika ziara hii nimepata takwimu za kutia moyo. Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ni nchi ya kwanza kwa kuwa na mauzo makubwa nchini Uganda, ikilinganishwa na nchi zote za Afrika Mashariki.

Imebainika Kuwa Tanzania inauza wastani wa dola za Marekani bilioni 1.6 nchini Uganda kwa takwimu za mwaka 2004, ilhali Uganda ikiuza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 160 kwa Tanzania, kwa mwaka 2004 na biashara imezidi kukua baada ya hapo.

Kiwango hiki kikubwa cha biashara kina maelezo. Mwaka 2019, Tanzania ilikuwa inauza nchini Uganda bidhaa zenye thamani ya dola milioni 494. Kwa mwaka 2024 bidhaa zilizouzwa nchini Uganda ni dhahabu (Sh bilioni 1.2), mchele dola milioni 201, karanga dola milioni 20 na bidhaa nyingine zinazoingiza fedha za kigeni.

Uganda ni mfano mmoja katika mingi. Nchi yetu inayo nafasi. Ikiwa nchi ya Uganda tunaweza kuuza bidhaa zenye thamani ya hadi dola bilioni 1.6, basi tukiongeza nguvu kidogo tu, bajeti yetu yote tunaikusanya kutoka kwenye vyanzo vyetu vya mapato bila kutegemea wafadhili. Kwamba Tanzania inaongoza katika Afrika Mashariki kwa kuwa muuzaji mkubwa wa bidhaa nchini Uganda, ni jambo lenye heri.

Rais Samia amesema wamekubaliana na Rais Museveni, reli ya SGR itoke Kahama hadi Lusaunga. Kisha itokee Lusaunga hadi Mulongo. Lusaunga hadi Bukoba ni kilomita 200. Napenda kuamini uamuzi huu ni sahihi kwa asilimia 100. Reli ikiishafika Lusaunga, naamini itapia Biharamulo, Kulema, Bukoba, Kyaka hadi Mulongo. Hapa kuna umbali wa kilomia karibu 270. Huu ni uwekezaji sahihi.

Ni kutokana na mwendelezo wa uwekezaji wa pamoja kati ya Tanzania na Uganda na kwa kuangalia uwekezaji wa bomba la mafuta la Afrika Mashariki lenye gharama ya dola bilioni 5 kwa sasa, ndiyo maana nimewaomba Rais Samia na Museveni wamalize kero za vikwazo vya kikodi na visivyo vya kikodi tule maisha. Tunafahamu Tanzania na Uganda ni nchi mbili zenye historia ya vita mwaka 1972 na mwaka 1978/79.

Sitanii, ya kale yamepita. Kama Tanzania imeuza bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 1.6, kati ya bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 8 kwa manunuzi inayofanya Uganda kwa mwaka, kumbe nchi yetu Tanzania kwa Bandari tuliyonayo na mazingira ya ukanda wa biashara, tunayo nafasi ya kufanya vema na kutengeneza maisha ya Watanzania na Waganda yakawa bora zaidi leo na kesho.

Asante Rais Museveni kuitembelea Tanzania siku chache baada ya kuchaguliwa. Asante Rais Samia kwa kukubaliana na Rais Museveni kuondoa vikwazo vinavyochelewesha ukuaji wa biashara kati ya nchi zetu. Hata hivyo, kwa vyovyote iwavyo, wakuu mnastahili pongezi kwa kufungua milango ya ukuaji wa biashara katika nchi zetu kwa maendeleo ya watu wetu kati ya mwaka 2019 na sasa 2026. Mungu ibariki Uganda, Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827