Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. Jim Yonazi ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Mradi wa DART amesema Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha inamaliza changamoto ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam, ili wananchi waweze kupata huduma bora, ya haraka na yenye uhakika.

Akizungumza hii leo 27 Februari, 2026 mara baada ya Kamati hiyo kufanya ziara ya kukagua miundombinu ya usafirishaji jijini humo, Dkt. Yonazi amesema Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika kuboresha sekta ya usafiri wa umma.

Alisema katika ziara hiyo, kamati ilitembelea Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) pamoja na Kampuni ya Uendeshaji wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) na kujionea maendeleo ya uwekezaji uliofanywa.

“Ni dhamira ya Serikali kuhakikisha usafiri wa Dar es Salaam unakuwa bora, wa kisasa na unaokidhi mahitaji ya wananchi. Tumejionea miundombinu iliyowekwa na jitihada zinazoendelea kuboresha huduma,” alisema.

Dkt. Yonazi alibainisha kuwa tayari kampuni zimeanza kuleta mabasi mapya, hatua itakayoliwezesha jiji hilo kuwa miongoni mwa majiji yenye usafiri wa kisasa barani Afrika. Aliongeza kuwa mabasi mengi yatatumia gesi asilia, huku Serikali ikiwa imejenga miundombinu ya vituo vya gesi ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa urahisi.

Aidha, alisema Serikali imewekeza katika mifumo ya TEHAMA itakayomwezesha mwananchi kutumia kadi maalumu kulipia nauli bila kulazimika kupanga foleni, jambo litakaloongeza ufanisi na kupunguza usumbufu.

Katika hatua nyingine, aliwahakikishia wananchi kuwa mabasi yote yaliyoharibika yatafanyiwa ukarabati na kurejea barabarani ili kuimarisha upatikanaji wa huduma.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Bw. Said Tunda alisema lengo kuu ni kurejesha furaha kwa wananchi wa Dar es Salaam kwa kuwapatia usafiri wa uhakika.

Pia aliwataka waendesha daladala kuendelea kutoa huduma huku Serikali ikiendelea kufanya mazungumzo nao ili kupata utaratibu bora wa ushirikiano, hususan kwa zile zilizopewa kibali cha kutumia barabara ya mwendokasi.

Hatua hizo zinaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia miundombinu imara na huduma bora za kijamii.