Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kagera

Serikali imesema itaendelea kuwaunga mkono na kuwatia moyo wawekezaji wa viwanda vya kuzalisha mifuko mbadala na vifungashio vyenye viwango, hatua inayosaidia jamii kuachana na mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.Dkt. Festo Dugange wakati wa ziara ya kukagua shughuli za uzalishaji wa vifungashio katika kiwabnda cha L & N Standard PackagingSolutions Ltd kilichopo Bunazi Wilaya ya Missenyi moani Kagera Februari 27, 2026.

Akizungumza mara baada ya kujionea shughuli za uzalishaji alionesha kuridhishwa na kulieleza kuwa wawekezaji wa viwanda vya mifuko mbadala wana nafasi katika utunzaji wa mazingira kwani wanazalisha mifuko ambayo inaoza na haichafui mazingira hivyo waungwe mkono.

Dkt. Dugange alisema kuwa Serikali ilipiga marufuku uzalishaji wa mifuko ya plastiki na vifungashio vya plastiki visivyo na viwango ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kulinda afya za wananchi endapo itachomwa au chembechembe zake zitaingia kwenye vyanzo vya maji.

“Mifuko ya plastiki inapotupwa na kuzagaa ovyo mitaani huweza kusabaisha maradhi yakiwemo saratani na vifo kwa mifugo endapo wataimeza hivyo viwanda kama hivi Serikali inaviunga mkono, niwapongeze sana kwani wanafanya kazi nzuri,“ alisema.

Aidha, Dkt. Dugange alisema kuwa mifuko mbadala ina soko kubwa na kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na wizara zenye dhamana ya Uwekezaji na Viwanda itahakikisha wawekezaji hawa wanapata ushirikiano ili uzalishaji uwe endelevu.

Halikadhalika, alielekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuendelea kuwasaidia wanapokidhi vigezo vya kupata cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM).

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo alitembelea mradi wa kitalu cha miche kilichopo Kashaba, Missenyi kwa ajili ya kuona namna mradi huo unavyotekelezwa.

Akiwaa katika mradi huo aliwaasa wananchi kupanda miti na kuitunza ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yana athari kubwa ikiwemo mafuriko kutokana na mvua zisizo na mpangilio pamoja na ukame unaosababisha hali ya jangwa.

Ili kukabiliana na changamoto hizo, Dkt. Dugange alieleza kuwa Serikali imekuja na mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa ya kijani kwa kupanda miti kwenye maeneo mbalimbalki ncnini

Kwa upande wake Mkurugenzi wa L&N Bw. Leonard Faustine alisema kiwanda hicho kimeajiri zaidi ya wafanyakazi 40 na katika kipindi kijacho kinatarajia kuajiri wafanyakazi 200 wa kudumu pamoja na wa msimu kulingana na mahitaji, hatua itakayoleta ufanisi zaidi katika uzalisha wa vifungashio.

Aliishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia NEMC kwa ushirikiano wanaopata hususan katika kupata vyeti vya mazingira na hivyo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika uchumi wa viwanda.

Pia, Bw. Faustine aliishukuru Serikali kwa ujumla kwa kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwemo katika uingiza nchini mitambo kwa ajili ya matumizi ya viwandani.

Akizungumzia kitalu hicho, alisema kuwa ulianzishwa mradi wa biashara ya kaboni kwa wakulima wadogo ambapo hadi hadi sasa wakulima zaidi ya 136,000 wamesajiliwa.

Pamoja na hatua hiyo, alisema ni theluthi moja ya wakulima hao ndio wana uwezo wa kuvuna hewa ya ukaa zaidi ya tani moja huku theluthi mbili hawakukidhi vigezo hivyo mradi huon umeanzishwa ili kuwawezesha.

Kitalu hicho cha miche zaidi ya milioni moja kilianzishwa mwaka 2022 kwa lengo la kuzalisha miche ya zao la biashara ya miti ya kivuli, viungo na matunda ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na wakati huo wakulima wanapata matunda.