GENEVA – Wakati mwenendo wa hali ya haki za binadamu katika baadhi ya mataifa duniani ukitajwa kuwa mbaya, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imemwagiwa sifa kuwa na mwenendo mzuri wa kushughulikia haki za binadamu.
Sifa hizo zilitolewa na Kamishna Mkuu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC), Volker Turk katika hotuba yake ya ufunguzi kuhusu Hali ya Haki za Binadamu Duniani, wakati wa Kikao cha 61 cha baraza hilo kilichofanyika Geneva, Uswisi.
Katika hotuba hiyo iliyosheheni rekodi ya matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu duniani, ikiwemo Marekani, Kamishna Turk alisema baraza hilo linatambua na kuthamini hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania za kuanzisha Tume ya Uchunguzi kufuatia vurugu zilizojitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025.
Hatua hiyo ya Tanzania kutajwa kwa sifa hizo nzuri na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Duniani inaendeleza rekodi na taswira ya nchi kuwa kisiwa cha amani na utulivu. Tayari wafuatiliaji wa masuala ya haki za binadamu duniani wameshauri matokeo ya ripoti ya Tume yazingatie misingi na juhudi za kutekeleza haki za binadamu, mambo yanayotarajiwa kuzingatiwa kutokana na uhuru na weledi wa wajumbe wake wakiongozwa na Mwenyekiti, Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman.
HALI ILIVYO DUNIANI
Tanzania ikisifiwa, mwenendo wa haki za binadamu umetajwa kuwa mbaya nchini Marekani, ambako operesheni dhidi ya wahamiaji haramu imetajwa kuendeshwa kwa kukiuka misingi ya haki za binadamu.
Pia, Iran imechomoza kuwa na hali mbaya ya haki za binadamu huku ikituhumiwa kukandamiza waandamanaji na kuwahukumu kifo, wakiwemo watoto.






