Geneva, 27 Februari 2026
Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization – WMO) Prof. Celeste Saulo ameahidi kuendelea kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika kuboresha huduma za hali ya hewa kwa matumizi katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Ameyasema hayo wakati wa kikao cha pembezoni mwa kikao cha 70 cha Kamati Kuu Tendaji ya Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (Seventieth Session of the Intergovernmental Panel on Climate Change-IPCC (70th IPCC Bureau), alipokutana na Dkt. Ladislaus Chang’a, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania (TMA), ambaye pia ni Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika WMO na Makamu wa Mwenyekiti wa Jopo la IPCC kwa lengo la kujadiliana kuhusu maendeleo ya utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini Tanzania na mipango ya kuendeleza ushirikiano na WMO tarehe 27 Februari 2026 Jijini Geneva, Uswisi.
Prof. Celeste Saulo amempongeza Dkt. Chang’a na kufurahishwa na namna TMA wanavyoendelea kusimamia vyema utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini Tanzania. Aidha, Prof. Celeste Saulo ameahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha huduma za hali ya hewa kupitia programu mbalimbali za WMO ikiwa ni pamoja na eneo la matumizi ya akili mnemba (AI) katika mnyororo mzima wa utoaji wa huduma za hali ya hewa.
“Nimefurahishwa na maendeleo ya utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini kwenu. Sisi kama WMO tuko tayari kuendelea kushirikiana ili kuboresha zaidi huduma huduma za hali ya hewa nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha na taasisi nyingine zilizopiga hatua zaidi ili kubadilishana ujuzi zaidi” Alisema Prof. Celeste Saulo.
Katika Kikao hicho, Dkt. Ladislaus Chang’a amemshukuru Katibu Mkuu wa WMO kwa usaidizi kwa TMA kupitia programu zake mbalimbali za uboreshaji wa huduma za hali ya hewa kikanda na kitaifa zikiwemo za “Climate Risk and Early Warning Systems (CREWS-EA), “Systematic Observations Financing Facility (SOFF)” na “Weather and Climate Information Services for Africa (WISER)” ambazo zinatekelezwa kwa ushirikiano na Wadau wa Maendeleo na Nchi Wanachama wa WMO ambapo utekelezaji wake unaendelea vizuri.
“Nashukuru sana kwa usaidizi wa WMO kupitia programu zake mbalimbali zikiwemo za CREWS, SOFF na WISER ambazo zinachangia pakubwa katika kuboresha utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini na kuongeza nguvu katika uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususan katika uboreshaji wa miundombinu ya hali ya hewa nchini na kuwajengea uwezo wataalamu. Programu hizi sio tu zimechagiza katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa bali zinawajengea uwezo wataalamu wa TMA wa kusaidia nchi nyingine kuboresha huduma zao za hali ya hewa” Alisema Dkt. Chang’a.
Dkt. Chang’a alimjulisha Katibu Mkuu wa WMO kuwa, Taasisi za Hali ya Hewa za Nchi wanachama wa WMO ambazo wataalamu wa TMA wametoa msaada wa kiufundi Barani Afrika hivi karibuni ni pamoja na Burundi, Sudan Kusini na Zimbabwe ambapo nchi nyingine ikiwa ni pamoja na Zambia, Sierra Leone na Uganda wataalamu wanaendelea na majadiliano ya namna wanavyoweza kusaidiwa na TMA katika maeneo ambayo TMA tumepiga hatua zaidi.
Maeneo ambayo TMA imezisaidia nchi nyingine katika tasnia hii ya hali ya hewa ni pamoja na uboreshaji wa “Mfumo wa Usimamizi wa Ubora wa huduma (Quality Management System-QMS and Competency Assessment )”, “Utabiri wa Hali Mbaya ya Hewa (Severe Weather Forecasting)”, “Utabiri wa Hali ya Hewa kwa Kutumia Modeli za Kompyuta (Numerical Weather Prediction-NWP)”, “Mchakato wa kisheria katika sekta ya hali ya hewa (Legal Matters)” na Usambazaji wa Huduma za Hali ya Hewa kwa Umma (Public Weather Services-PWS).
Katika kuhitimisha mazungumzo yao, Dkt. Chang’a alimshukuru Katibu Mkuu wa WMO kwa fursa ya kuleta mikutano mikubwa ya kitaalamu nchini ikiwa ni pamoja na mkutano wa nne (4) wa Wataalamu bingwa wa utabiri wa hali ya hewa Duniani utakaojadili maendeleo ya utabiri wa hali ya hewa kwa kuzingatia ukuaji wa teknolojia na matumizi ya huduma hizi kwa sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi “The Fourth WMO Operational Climate Prediction (OCP-4)” unaotarajiwa kufanyika Arusha mwishoni mwa mwezi Juni hadi mwanzo wa Julai 2026 kwa mara ya kwanza barani Afrika na kwa Tanzania.



