*Ataka fedha zitafutwe kujenga barabara ya Katesh – Babati
*Akataza watendaji kuchukua bidhaa za wajasiriamali wadogo
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amezindua Stendi ya Mabasi ya Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyopo Katesh, wilayani Hanang, mkoani Manyara ambayo imejengwa kwa gharama ya sh. bilioni 5.69.
Stendi hiyo ambayo ujenzi wake umekamilika na imeanza kutumika, imelenga kuboresha utoaji huduma za usafiri na usafirishaji. Miundombinu iliyopo ni pamoja na jengo kuu la kituo cha mabasi, maduka 116, maeneo ya wauza vyakula, vyoo matundu 21, vituo saba vya kukusanyia taka na vituo viwili vya ukaguzi na ulinzi. Hakuna kituo cha polisi.
Akizungumza na wakazi wa Hanang waliofika kushuhudia uzinduzi huo leo (Jumapili, Machi Mosi, 2026), Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na ujenzi wa stendi hiyo ambao ni sehemu ya miradi ya kimkakati ya kuboresha miundombinu ya usafiri na kuongeza mapato ya ndani.
Dkt. Mwigulu ametumia fursa hiyo kumwagiza Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya awasiliane na Waziri wa Ujenzi na Mtendaji Mkuu wa TANROADS ili watafute fedha za kuitengeneza barabara ya Katesh – Babati kutokana na uchakavu ilionao.
Amesema barabara za wilayani za mkoa wa Manyara ziangaliwe na kujengwa haraka kwani mkoa wa Manyara ni miongoni mwa mikoa ambayo haina barabara za lami za wilaya. “Ukiondoa barabara kuu ya Arusha – Dodoma na hii ya Babati – Singida kupitia Katesh, hawana barabara nyingine.”
Kuhusu tabia ya kuwanyang’anya wajasiriamali zana zao za kazi, Waziri Mkuu amekemea tabia hiyo na kuwataka watendaji wanaofanya hivyo waache mara moja. “Acheni watu wafanye kazi, bakuli, sahani, bajaji au pikipiki ni vitendea kazi vyao. Msikamate vitendea kazi vyao,” amesisitiza.
“Tusichukue bidhaa za watu, tusitupe bidhaa za watu hiyo ni mitaji yao. Tuna kazi kubwa ya kutekeleza Dira 2050, tunahitaji fedha nyingi kutekeleza miradi iliyopo. Msichukue bidhaa zao, kama kuna jambo tuongee nao, tuwaeleweshe,” amesisitiza.
Kuhusu kesi zilizoko mahakamani au zilizotolewa maamuzi na mahakama, Waziri Mkuu amewataka wananchi wafuate taratibu za kisheria kwa vile Serikali ni mhimili mwingine na unaheshimu maamuzi yanayotolewa na na mhimili wa mahakama. Amesema maamuzi ya kimahakama hayabatilishwi na matamko ya viongozi kama Makamu wa Rais, Waziri Mkuu au Mkuu wa Mkoa.
“Jambo likishaenda mahakamani Mkuu wa Mkoa wala Waziri Mkuu hawawezi kuweka neno hapo. Sisi ni lazima tuheshimu utaratibu wa kisheria. Kama mwananchi hajaridhika na maamuzi ya awali, ipo njia. Ipo milango ya kufuata, lakini sisi hatuwezi kuingilia maamuzi ya mhimili wa sheria,” amesisitiza.
Waziri Mkuu ambaye amekuwa akisikiliza kero za wananchi kwenye mikutano yake ya hadhara, leo kwenye mkutano huo amepokea hoja nyingi zilizohusu kesi za madai na mirathi, migogoro ya ardhi, familia kudhulumiana na mipaka ya mashamba.






