Na Muhidin Amri, JamhuriMedia, Songea

MPANGO wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,kuongeza program maaalum za mafunzo ya ufundi stadi kupitia vyuo vya ufundi ni hatua nzuri ya kujenga rasilimali imara kwa vijana hapa nchini.

Mpango huu unatajwa kuwa mwanzo wa mapinduzi makubwa katika mfumo wa utoaji elimu ya ufundi hapa nchini kwani utasaidia sana kutengeneza nguvu kazi inayoendana na uhalisia na kupunguza tatizo la ajira kwa kundi kubwa la kijamii hususani vijana.

Changamoto ya ajira hapa nchini ni pengo kubwa kwa sababu,elimu inayofundishwa shuleni na ujuzi ni kama vitu viwili tofauti kwani baadhi ya vijana wanahitimu kwenye shule na vyuo vya elimu ya juu bila kuwa na uwezo kwa vitendo.

Hali hiyo imekuwa chanzo cha kukatisha tamaa na inachangia sana hata baadhi ya vijana hapa nchini, kujitumbukiza katika shughuli zisizo rasmi baada ya kukosa kipato cha uhakika.

Baada ya kutambua changamoto hiyo Wizara ya elimu kupitia vyuo vya ufundi stadi hapa nchini(VETA)imeanza kutoa mafunzo ya fani mbalimbali kwa vijana ili kuwapa ujuzi kwa vitendo ambao utawasaidia kujiajiri badala ya kusubiri ajira za Serikali.

Miongoni mwa vyuo hivyo ni Chuo cha VETA Songea, ambacho kimeanzisha kuwajengea uwezo wahitimu wake ili wanapomaliza masomo yao waweze kukabiliana na changamoto ya ajira kwa kuanzisha shughuli mbalimbali ikiwemo viwanda vidogo na vya kati badala ya kukaa nyumbani kwa muda mrefu wakisubiri kuajiriwa.

Mkuu wa Chuo cha Veta Songea Rahabu Mwakatundu, akizungumzia juu ya kozi mbalimbali zinazofundishwa kwenye chuo hicho

Chuo cha VETA Songea,kilianzishwa kama sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha sekta ya elimu na kuongeza ujuzi wa kiufundi kwa vijana wa Tanzania na kutoa mafunzo ya ufundi kwa kiwango cha kitaaluma ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira ndani nan je ya nchi.

Awali chuo hiki kilianza kutoa mafunzo mwaka 1984 kwa fani tatu za ufundi ambazo ni ufundi wa magari,ujenzi,uashi na useremala na kilikuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 60.

Kwa sasa,chuo hiki kimepiga hatua kubwa ya kimaendeleo kwa kuingiza teknolojia mpya na mbinu za kisasa za ufundushaji,hatua iliyosaidia kuzalisha wahitimu wengi wenye uwezo wa kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta mbalimbali za kiufundi ambazo ni pamoja na ujenzi,umeme wa majumbani na magari.

PROGRAMU NA MAFUNZO YANAYOPATIKANA KWENYE CHUO CHA Ufundi VETA SONGEA.

Kwa mujibu wa Mkuu wa chuo hicho Rahabu Mwakatundu,kwa sasa chuo kimepata mafanikio makubwa kwani kinatoa mafunzo ya kozi ndefu 13 za ufundi wa magari,ushonaji,umeme wa majumbani na magari,uashi,useremala,Uhazili na kompyuta.

Mwakatundu anataja kozi nyingine zinazotolewa na VETA Songea ni uungaji vyuma,Tehama(ICT)Upakaji rangi ufundi wa vifaa vya Electroniki na upishi na uwezo wa chuo kupokea wanafunzi umeongezeka kutoka 60 mwaka 1984 hadi 760 mwaka 2026 kwa kozi za muda mrefu(Level 1-3)ambazo ni miaka miwili hadi mitatu na kozi za muda mfupi wiki hadi miezi sita kulingana na mahitaji ya mwombaji.

FURSA MBALIMBALI

Mwakatundu anasema,kusoma katika chuo hiki kuna faida nyingi zinazowafanya vijana na wazazi kuamua kuwekeza kwenye elimu ya ufundi hususani wahitimu kuwa na ujuzi wa kiufundi unaohitajika sana kwenye soko la ajira,hivyo kuwa na nafasi kbwa ya kupata ajira au kuanzisha biashara.

Anataja kozi zinazotolewa ni matengenzo ya magari,huduma ya ujenzi na ukarabati wa nyumba,ushonaji mavazi ya viwandani,kutengeneza samani mbalimbali,kutengeneza mashine za kilimo na bidhaa mbalimbali.

“Katika chuo chetu tunatoa kozi maalum ya mapambo kwenye kumbi za mikutano,harusi,huduma ya chakula,kurasimamisha ujuzi,mafunzo kwa wenye mahitaji maalumu,mafunzo kwa wajasiriamali na mashine za kuteneneza chakula cha mifugo kama kuku, Samaki nk”alisema Rahabu.

Mwalimu wa fani ya ushonaji katika Chuo cha Ufundi Veta Songea Riziki Ndomba akiwa kazini, Ndomba ni miongoni mwa walimu waliosoma katika chuo hicho kabla ya kuajiriwa kwa kazi ya Ualimu wa fani hiyo

MIRADI YA MAFUNZO INAYOTEKELEZWA NA CHUO CHA VETA SONGEA.

Veta Songea inatekeleza mradi wa ukuzaji ujuzi(uanangezi) na kozi hizo zinatolewa kwa ufadhili wa Ofisi ya Waziri Mkuu na wanufaika ni vijana wanaolipiwa ada na wanachagua kusoma kozi yoyote wanayoipenda na muda wa mafunzo ni miezi 8 ambapo miezi 6 wanakuwa darasani namiezi 2 wanapelekwa viwandani.

Anasema,mradi mwingine tunaotekeleza katika chuo chetu ni Timiza Malengo chini ya ufadhili wa TACAIDS,mradi huu unalenga kuwasaidia vijana wa kike kupata ujuzi ili waweze kujiajiri na kuajiriwa kwa lengo la kujipatia kipato.

Mwakatundu anafafanua kuwa,lengo kubwa ni kuwaepusha kuingia katika hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa ikiwemo ukimwi na biashara ya ngono,hapa napo mabinti hawa wanachagua fani yoyote wanayoipenda na muda wa kzo hii ni miezi mitatu na walengwa ni mabinti wanaotoka katika mazingira hatarishi na kaya maskini.

MRADI WA ZANA ZA KILIMO,UMWAGILIAJI NA UHIFADHI MAZAO.

Mwakatundu anasema,mradi huu unahusika kuwapatia vijana ujuzi wa kutumia na kutengenezaa zana za kilimo,kuwapatia ujuzi wa kuhifadhi na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na unahusisha jinsia zote.

Anasema, chuo cha Veta Songea kinatekeleza Programu maalum inayofahamika Mafunzo ya Wanawake na Samia ambayo imejikita zaidi kuwapatia wanawake wa Mkoa wa Ruvuma ujuzi wa kuweza kuwasadia kujiajiri na kupata kipato.

“Tunategea wanawake hawa kutumia ujuzi huu kupata fursa katika miradi ya kimkakati na miradi mingine ya Serikali na binafsi kupitia vyetu tunavyowatunuku mara baada ya kumaliza kazi”amesema.

JENGA UWEZO NA AJIRA-JUA

Mwakatundu anaeleza kuwa,mradi huu unafadhiliwa na Shirika la COPE lenye makao makuu yake Nchini Italia na unahusika kutoa mafunzo ya ufundi kwa vijana ili kuwajengea uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa na wanufaika wake ni makundi yenye mahitaji maalum(Vijana,Wanawake na wenye ulemavu).

Anasema,mradi upo kwenye hatua za awali za kuwabaini walengwa kutoka katika makundi hayo maalum ili mafunzo yaweze kuanza. Tunawahamasisha Wananchi wa Ruvuma kuchangamkia fursa hii.

VIJANA WENYE ULEMAVU KUSOMA BURE

Mamlaka ya Elim una Mafunzo ya Ufundi Stadi imeona ni vema kuwafadhili vijana wenye ulemavu ili waweze kupata elimu ya ufundi stadi bila malipo ili waweze kuendesha maisha yao bila kutegemea watu wengine na waweze kuingia kwenye soko la ajira.

Mmoja wa wanafunzi mwenye ulemavu aliyesoma chuo cha Veta Songea na sasa ni fundi wa ushonaji Riziki Ndomba anasema,chuo hicho kimemsaidia sana kupata ujuzi ambao leo umemwezesha kujitegemea kimaisha kwani bila kwenda Veta hasingeweza kuisha maisha aliyonayo sasa.

Anasema,alipofika Veta alipokelewa vizuri na uongozi wa chuo na kutokana na hali yake ya ulemavu wa miguu na mikono alichaguliwa fani ya ushonaji na kutokana na chuo hicho kuwa na walimu wenye ujuzi na weledi mkubwa alimaliza kazi yake na kufaulu vizuri.

“Kutokana na ulemavu wangu walimu niliowakuta walinichagulia fani ya ushonaji na mimi niliipenda sana na kuongeza juhudi ili niweze kufanya vizuri kwenye mafunzo yangu na hatimaye niliweza kuhitimu kazi yangu ya muda mrefu ya miaka miwili nikiwa fundi na leo jamii inaniamini”alisema Ndomba.

Amewataka jamii ya watu wenye ulemavu, kuacha kukata tamaa ya maisha na kuomba omba badala yake wajikite kutafuta fursa zilizopo ikiwemo kujiunga na vyuo vya ufundi kupata ujuzi na kuanzisha shughuli za kujipatia kipato hivyo kujikwamua na umaskini.

Mwanafunzi wa mwaka wa pili anayesoma fani ya umeme Agrey Komba amesema,ameshawishika kujiunga na Veta ili kupata maarifa ambayo kama kijana yatamsaidia kupata ujuzi kwa ajili ya kujiajiri.

Komba anasema,kitu kingine kilichomshawishi ni fursa zilizopo kwenye ufundi na amejiunga na Chuo cha Veta Songea uwepo wa walimu wenye weledi, kuwa na vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kinatoza gharama ndogo ikilinganisha na vyuo binafsi.