Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ametangaza kuanza rasmi kwa kliniki maalum ya kutatua kero za wananchi, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya viongozi wa juu wa Serikali.
Akizungumza leo Machi 2,2026 Jijini hapa kuhusu mpango huo, amesema Ofisi yake imetenga siku tatu za kusikiliza kero za wananchi kuanzia Machi 4 hadi 6 mwaka huu, ambapo Taasisi zote za umma zitashiriki moja kwa moja katika kupokea na kushughulikia malalamiko hayo.
“Lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kuwasilisha changamoto zao na kupata majibu na ufumbuzi ndani ya muda mfupi, kliniki hiyo itasaidia wananchi kupatiwa huduma mbalimbali bila malipo, ikiwemo huduma za afya kwa kupima afya kwa hiari na kutoa damu, sambamba na huduma nyingine zitakazotolewa na Taasisi shiriki, ” ameeleza.
Amebainisha kuwa kero za wananchi hazimaliziki, kwani huibuka mpya kila siku, hivyo uwepo wa Taasisi zote ni muhimu ili kuongeza ufanisi wa mpango huo.
Kutokana na hayo amehimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika siku hizo tatu ili kutumia fursa hiyo kuwasilisha kero zao ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu.
“Natoa wito pia kwa Taasisi zote za umma kuwajibika ipasavyo na kuonesha weledi, ukarimu na uwajibikaji kwa wananchi, na kaulimbiu ya awali ya “Kero yako, wajibu wangu” tumeiboresha na sasa kwenye mpango huu tutaenda na “Kero yako, wajibu wangu – Tabasamu na Samia”, ikilenga kuimarisha uhusiano chanya kati ya Serikali na wananchi.

Kuhusu wananchi wa pembezoni , Senyamule amesema mpango huo utakuwa endelevu, na hivyo kuwafikia wananchi wote wa wilayani kwa mujibu wa taratibu na miongozo ya Serikali hali itakayowarahisishia na kuwapunguzia gharama za kuifuata huduma hiyo mbali.
“Kwa watakaoshindwa kuhudhuria moja kwa moja Pia, wa naweza kuitumia namba 0736 520 025 kwa kutuma ujumbe mfupi wa kero zao ili zipokelewe na kushughulikiwa na mamlaka husika,mpango huu unatarajiwa kuimarisha uwajibikaji wa Taasisi za umma, ” amesema


