Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Songwe
Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, inayoadhimishwa kote ulimwenguni kila ifikapo Machi 08, 2026, Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa wa Songwe (TPF NET) kwa kushirikiana na wanawake wa majeshi mengine mkoani humo, wametembelea Kituo cha Afya Tunduma kilichopo Wilaya ya Momba, Mkoa wa Songwe, kwa lengo la kuwafariji wagonjwa waliolazwa katika wodi ya wanawake na watoto.
Akizungumza Machi 02, 2026 mara baada ya kukabidhi mahitaji ya kila siku ya binadamu kwa wagonjwa hao, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Maria Kway alisema lengo la ziara hiyo ni kuonesha mshikamano, upendo na moyo wa kujitoa kwa jamii, hususan kwa wanawake na watoto wanaohitaji msaada na faraja katika wakati huu wa kuelekea maadhimisho hayo muhimu duniani.

Kwa niaba ya uongozi wa kituo hicho cha afya, Katibu wa Afya wa Kituo cha Afya Tunduma, Bi. Manselina Kivamba, aliushukuru Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa wa Songwe pamoja na wanawake wa majeshi mengine kwa moyo wao wa kujitolea, huku akiziomba taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali pamoja na mashirika mengine kuiga mfano huo kwa kuendelea kusaidia makundi yenye uhitaji katika jamii.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linaendelea kuthibitisha kuwa lipo karibu na jamii, si tu katika masuala ya ulinzi na usalama, bali pia katika kuungana na wananchi kuwasaidia wenye uhitaji, hatua inayochangia kujenga taswira chanya na kuimarisha imani ya jamii kwa Jeshi la Polisi.






