Na Maelezo, Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mkazo maalum katika kuimarisha ukuaji wa Sekta ya Viwanda kwa kuvutia uwekezaji katika maeneo tengefu ya viwanda kwa kuweka miundombinu wezeshi ya maedeleo ya viwanda Unguja na Pemba.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo Kaimu Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Mhe. Shariff Ali Shariff kuhusiana na siku 100 za Mafanikio ya uongozi wa awamu ya pili ya Dkt. Mwinyi amesema maeneo yaliyotengwa ni pamoja na Dunga, Chamanangwe na Pangatupu.

Amesema kuwa eneo la Viwanda Dunga Zuze tayari miradi mikubwa mitatu (3) ya viwanda yenye thamani ya TZS bilioni 203.906 inaendelea kujengwa ikiwemo kiwanda cha kuzalisha dawa za magonjwa ya binaadamu, kiwanda cha nguo, kiwanda cha kuzalisha bidhaa za chuma pamoja na kiwanda cha kuchakata mwani Chamanangwe ambapo ujenzi wake unaendelea.

“Kukamilika kwa miradi hiyo kutazidi kuimarisha mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa kutoka asilimia 20.8 ya sasa na kufikia asilimia 25 mwaka 2030, pamoja na kuchangia upatikanaji wa ajira, kupunguza uagizishaji bidhaa kutoka nje na kuchochea kuimarika biashara nchini” ameeleza Mhe. Shariff.

Waziri huyo ameeleza kuwa mradi huo utasaidia kukuza ajira kwa vijana na wanawake, kuongeza thamani ya zao la mwani pamoja na kipato cha wakulima vile vile kuimarisha mapato ya Serikali kupitia bidhaa za viwandani zenye ushindani wa kimataifa.

Aidha Waziri Shariff amefahamisha kuwa Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC) limeuza jumla ya tani 3,702 za karafuu nje ya nchi kwa thamani ya Shilingi Bilioni, 59.88 kwa kipindi cha siku 100 ambapo matarajio ya awali ilikuwa ni kuuza tani 2,827.

“Katika jitihada za kuongeza thamani ya ufanyaji biashara Wizara kupitia Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) limeweza kuzalisha jumla ya tani 3,423.65 za karafuu  zenye thamani ya Shilingi Bilioni, 55.45, ambapo matarajio ya awali ilikuwa ni kununua tani za karafuu 2,870” amefahamisha Waziri huyo.

Akizungumzia kuhusu bei elekezi ya bidhaa amesema Wizara kupitia Tume ya Ushindani Halali wa Biashara (ZFCC) inaendelea kudhibiti bei elekezi kwa bidhaa za mchele, unga wa ngano, sukari, mafuta ya kula na saruji ambapo Taasisi hiyo imefanya ukaguzi wa maduka 375, maghala 18, na Supermarket nne (4) na wafanyabiashara tisa (9) kubainika na makosa ya kutoweka utambulisho wa bei katika bidhaa zao.

Amefahamisha kuwa katika kuimarisha ukuaji na utafutaji masoko nchini, Wizara imefanya maonyesho ya 12 kwa lengo la kuitangaza Zanzibar kibiashara hivyo Wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango imeandaa mpango wa kujenga kituo cha kimataifa cha maonyesho ya biashara huko Fumba.

“Kituo hicho kinalenga kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa kuunganisha biashara za sekta muhimu za utalii, fedha, mawasiliano, miundombinu, elimu, afya na kilimo pamoja na kukuza biashara za ndani na za Kimataifa” ameeleza.

Kaimu Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Shariff Ali Shariff akizungumza na Vyombo vya Habari kuhusiana na Maendeleo na Mafanikio yaliopatikana katika Wizara kwa kipindi cha Siku Mia Moja za Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi kwa kipindi chake cha Pili hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Habari Maelezo Rahaleo Zanzibar