Na Mwandishi wetu, JamhuriMedia, Dar es salaam
Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Chama cha ACT Wazalendo kupitia ngome yake ya wanawake kimezindua mnara wa kumbukumbu kwa ajili ya watu waliopoteza maisha kufuatia matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29, 2025.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Machi 3, 2026, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, amesema hatua hiyo inalenga kuenzi kumbukumbu ya waliopoteza maisha na kuonesha mshikamano na familia zilizoathirika na matukio hayo.
Dorothy amesema maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ni wakati muhimu wa kutafakari nafasi ya wanawake katika jamii pamoja na changamoto wanazokutana nazo, ikiwemo maumivu wanayopitia mama waliopoteza watoto wao katika matukio hayo.
“Machozi ya mama anayesubiri kurejeshewa mwili wa mwanae ni kilio kisicho na sauti, lakini chenye uzito mkubwa kwa taifa. Machozi ya mama ni deni la taifa,” amesema Dorothy.
Amesisitiza kuwa taifa linahitaji uponyaji wa kweli kufuatia matukio ya Oktoba 29, akieleza kuwa uponyaji huo unaweza kupatikana kwa kukabiliana na ukweli wa yaliyotokea pamoja na kuhakikisha haki inapatikana kwa waathirika.
Dorothy pia ametoa wito wa kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi iliyo nje ya Serikali ili kuchunguza kwa kina matukio hayo, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha haki, uwajibikaji na maridhiano ya kweli kwa taifa.


