Na Mwandishi Wetu -Jeshi la Polisi

Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa wa Songwe (TPF Net) kwa kushirikiana na wanawake wa majeshi mengine mkoani humo, wamemtembelea Bi. Enita Sinyinza, mkazi wa Kitongoji cha Hezya Kati, Kijiji cha Hezya, Kata ya Hezya, Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, kwa lengo la kumpa faraja na msaada wa magodoro pamoja na mahitaji mbalimbali ya matumizi ya nyumbani.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo nyumbani kwa Bibi Enita tarehe 04 Machi 2026, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Maria Kway alisema Bi. Enita Sinyinza ni mfano wa kuigwa katika jamii kwa namna anavyowalea na kuwahudumia watoto wake licha ya changamoto kubwa ya kiafya wanayokabiliana nayo, huku akieleza kuwa moyo wake wa uvumilivu, upendo na kujitoa unaakisi nguvu ya mwanamke katika jamii, huku akisisitiza umuhimu wa taasisi na wananchi kushirikiana kuwasaidia wenye uhitaji ili kuimarisha ustawi wa jamii.

Kwa upande wake, Bi. Enita Sinyinza alishukuru Jeshi la Polisi kwa umoja na mshikamano walionao ikiwa ni.pamoja kati ya wengi kumkumbuka na kumpa faraja, akieleza kuwa ujio wao umempa moyo na matumaini mapya ya kuendelea kuwalea watoto wake.

Kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Hezya, Bw. Adamu Nzunda alishukuru ujio wa ugeni huo na kupongeza ushirikiano mzuri uliodhihirishwa kati ya Majeshi na jamii, akibainisha kuwa mshikamano huo hauimarishi tu masuala ya usalama bali pia unajenga utamaduni wa kusaidiana na kuwajali.

Ikumbukwe kuwa Bi. Enita ana watoto 04 wenye changamoto ya akili ambao ni Tito, Lomanusi, Michael na Marita Mwangwale, ikiwa Jeshi la Polisi na Majeshi mengine wakionesha upendo, mshikamano na kujitoa kwa jamii na kwa familia zinazokabiliwa na changamoto mbalimbali kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayotarajiwa kufanyika Machi 08, 2026.