Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

Maafisa Elimu nchini wametakiwa kushirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali wakiwemo sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na jamii ili kuwekeza na kuimarisha miundombinu ya nishati safi ya kupikia katika shule.

Wito huo umetolewa Machi 4, 2026 jijini Arusha na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Ngereja Mgejwa, wakati akiwasilisha mada kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia shuleni katika Mkutano Mkuu wa 12 wa Umoja wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri Tanzania (REDEOA) wenye kaulimbiu isemayo “Matumizi ya TEHAMA ni nguzo muhimu ya uboreshaji wa elimu Tanzania.”

Mgejwa amesema pamoja na jitihada za Serikali kutekeleza Mradi wa Nishati Safi ya Kupikia shuleni na kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100, zikiwemo shule, bado kuna umuhimu mkubwa wa kushirikiana na wadau ili kufanikisha utekelezaji wa ajenda hiyo.

Amesema wadau wana nafasi kubwa katika kuharakisha uwekezaji na utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia kupitia ubia na ushirikiano wa kimkakati.

Kupitia ushirikiano huo, amesema shule zinaweza kupata majiko ya kisasa, mifumo ya gesi pamoja na nishati mbadala itakayosaidia kupunguza gharama za uendeshaji, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za chakula na kulinda afya za wanafunzi pamoja na watumishi.

Ameongeza kuwa baadhi ya shule tayari zimeanza kutumia nishati safi ya kupikia kwa kushirikiana na wadau, zikiwemo Shule ya Sekondari Masoka mkoani Kilimanjaro, St. Monica Primary School jijini Arusha na Shule ya Sekondari Moringe mkoani Arusha.

Mgejwa amesema hatua hiyo inaenda sambamba na juhudi za Serikali za kulinda mazingira na kuboresha afya ya jamii kwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Aidha, amewahimiza Maafisa Elimu kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi hiyo na kuhakikisha miundombinu inayowekwa inakuwa endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Amesema hadi kufikia mwaka 2025, takribani asilimia 23.2 ya Watanzania walikuwa wamehamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia na kutokana na juhudi zinazoendelea, inatarajiwa ifikapo mwaka 2034 zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania watakuwa wanatumia nishati safi ya kupikia.

Kwa upande wake, Afisa Elimu Mkoa wa Ruvuma, Mwl. Edith Mpinzile, amesema mkoa huo unaendelea kufanya vizuri katika utekelezaji wa agizo la Serikali kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100.

Amesema Mkoa wa Ruvuma una jumla ya shule za sekondari 153, ambapo kati ya hizo shule 43 tayari zinatumia nishati safi ya kupikia.

Ameongeza kuwa viongozi wa baadhi ya shule wamekuwa wakishirikiana na wadau pamoja na wazazi katika ujenzi wa majiko ya kisasa yanayokidhi matumizi ya nishati safi ili taasisi hizo zinahamie katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ambayo ni nafuu na rafiki kwa mazingira.