Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

Mkoa wa Pwani umejiwekea mpango mkakati kuandaa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 hadi 2030/2031 kwa kuzingatia Dira ya Taifa 2050, Ilani ya CCM 2025/2030 na Malengo Endelevu ya Milenia, itakayobeba masuala yote muhimu ili kuinua mkoa kupitia uwekezaji na viwanda.

Aidha Mkoa huo unatarajia kutumia Tsh bil497,184,263,311 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ambapo matumizi ya kawaida ni Tsh 293,578,022,000 miradi ya maendeleo Tsh 92,321,580,000 na mapato ya ndani ya halmashauri Tsh 111,284,681,311.

Akizungumza katika kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC) kilichofanya tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2025/2026 na bajeti ya mkoa wa Pwani mwaka wa fedha 2026/2027, Romwald Mwendi ,Katibu Tawala Msaidizi -Sehemu ya Mipango na Uratibu alieleza wanaendelea kuhakikisha fedha za ruzuku, mapato ya ndani ya halmashauri na michango ya wahisani zinatumika katika shughuli zilizokusudiwa wananchi.

Aliongeza kuwa mwaka wa fedha 2026/2027 mkoa unakisia kutumia Tsh 385,899,500,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo.

“Kati ya fedha hizo mishahara ni Tsh 270,800,000,000 matumizi mengine Tsh 22,777,900,000 na miradi ya maendeleo Tsh 23,327,000,000, “

“Halmashauri zinakisia kukusanya Tsh 111,284,600,000 katika vyanzo vya ndani vya mapato ambapo makisio yameongezeka Tsh 23,327,081,311 sawa na asilimia 26.52 ukilinganisha na makisio ya mwaka 2025/2026”

Alitaja changamoto zinazokuwa zikiwakabili ni ufinyu na ukomo wa bajeti usiotosheleza mahitaji ukilinganisha na jiografia na ukubwa wa mkoa, kupanda kwa bei ya bidhaa na vifaa, uchache na uchakavu wa magari katika mamlaka za serikali za mitaa na kuwepo kwa visiwa wilaya ya Mafia na Mkuranga pamoja na Delta ya Mto Rufiji hali inayosababisha gharama kubwa za uendeshaji na utekelezaji wa miradi.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Abubakar Kunenge aliishukuru serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuupatia mkoa fedha kwa ajili ya kutekeleza program mbalimbali na miradi ya maendeleo na ya kimkakati.

Kunenge alisema mkoa umejipanga kuendelea kuwa kinara kwa kila jambo nchini ikiwemo ongezeko la viwanda, elimu, afya na uwekezaji.

Aliwataka kuwajibika, kushirikiana kupiga hatua ya kiuchumi na kusisitiza Halmashauri ziendelee kuongeza fursa, kubuni vyanzo vya mapato ili kujiimarisha pamoja na kuvutia wawekezaji kwenye maeneo yao.

Katika kikao hicho kuliwasilishwa ombi la Halmashauri ya Kibaha kupandishwa hadhi kuwa Halmashauri ya Mji baada ya kukidhi vigezo na Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kuwa Manispaa baada ya kutimiza vigezo viwili vilivyosalia ili iweze kupitishwa na mkoa kisha ipelekwe TAMISEMI kwa hatua zaidi.