Na Sixmund Begashe, JamhuriMedia, Arusha
Waongoza watalii wote nchini wametakiwa kuchukuwa hatua zote za taadhari wakati wanapowatembeza watalii katika maeneo ya Hifadhi hususani Hifadhi ya Taifa Serengeti hasa kipindi hiki cha mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) kwenye Mkutano wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameki Nchemba (Mb), Wilayani za Karatu, Monduli Mkoani Arusha.

Dkt. Kijaji amesema kuwa, Wizara hiyo inahitaji kuona watalii, waongoza watalii na watanzania wote ndani ya Hifadhi za Taifa wanakuwa Salama, hivyo ni vyema waongoza watalii na madereva wote wanaigia Hifadhi za Taifa kuzingatia kanuni na taratibu zilizopo za taaluma zao.
Katika zoezi la kulipa kifuta jasho na kifuta machozi, Dkt. Kijaji amebainisha kuwa, Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imelipa jumla ya shilingi 59,337,500.00 kwa wananchi 167 walioathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu katika Wilaya ya Karatu kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24 na 2024/25.
‘Kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24 na 2024/25 jumla ya shilingi 553,499,375.00 zimelipwa kwa wananchi 2,176 walioathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu katika Wilaya ya Monduli”. Alisema Dkt. Kijaji
Aidha katika mapambano dhidi ya Wanyamapori wakali na waharibifu, pamoja na Matumizi ya teknolojia ya kisasa, Dkt. Kijaji amesema kuwa Wizara hiyo inajenga vituo viwili vya askari kimoja kinajengwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) katika kijiji cha Chemchem kitongoji cha Mbulumbulu na cha pili kinajengwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) katika kijiji cha Endara kata ya Endara Wilayani Karatu.







