Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

WAKATI dunia ikijiandaa kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ifikapo Machi 8, 2026 , wanawake nchini Tanzania wameendelea kuandika historia mpya katika sekta ya madini wakivunja vikwazo vilivyodumu kwa miaka mingi.

Hayo, yamejidhihirisha kwa Asha Jama ambaye ni mmoja wa wamiliki wa mgodi wa MCC MAHADEO Tanzania unaochimba madini ujenzi aina ya kokoto katika kijiji cha Ntyuka jijini Dodoma.

Akizungumza na Madini Diary Asha Jama amesema kuwa, uwezeshaji wa wanawake katika sekta ya madini si tu suala la usawa wa jinsia , bali ni mkakati muhimu wa kukuza uchumi jumuishi.

Asha ameeleza kuwa, Wanawake wanaendelea kuwa sehemu ya uchumi na fursa za usawa zinaongeza juhudi katika uzalishaji sehemu mbalimbali pamoja na kuimarisha ustawi wa familia na jamii kwa ujumla.

Kwasasa wanawake tupo katika mnyororo mzima wa thaman madini tunajishughulisha katika kuleta na kuchangia Pata la Taifa kwa kufanya uzalishaji na uuzaji wa bidhaa mbalimbali zilizopo katika mnyororo wote wa thaman madini nchini.

Kwa upande Bi. Ellah Christopher ambaye anamiliki leseni ya madini ujenzi aina ya mchanga katika korongo la Ihumwa anasema kuwa , wanawake wana uwezo mkubwa katika kumiliki sekta ambazo zamani zilionekana kuwa za wanaume ikiwemo sekta ya madini na sekta za ujenzi hii ni kutokana na mabadiliko ya kifikra na ushirikishwaji wa wanawake katika shuguli za maendeleo kumefungua mawazo chanya ambayo yanaleta maendeleo makubwa kuanzia ngazi ya familia, jamii inayotuzunguka na taifa kwa ujumla.

Ellah anaeleza kuwa, wanawake wengi ujifunza kupitia mifano ambapo mwanamke anayefanikiwa kwenye biashara kubwa anawatia moyo wanawake wengine lakini pia anaonyesha kuwa mwanamke anaweza kuwa kiongozi na mfanyabiashara mkubwa.

Akifafanua kuhusu ushiriki wa mwanamke katika sekta za kiuchumi, amesema kuwa, Mwanamke anayemiliki biashara kama mgodi wa mchanga ana jukumu kubwa la kuonyesha uwezo wa wanawake katika uchumi , kusaidia jamii pamoja na kulinda mazingira.