Na Byarugaba Innocent, OR-MV
Tanzania nchi yangu, nakupenda kwa moyo wangu wote. Ni nchi yenye utajiri mwingi kuanzia amani iliyopo. Aidha, rasilimali watu, ardhi yenye rutuba, madini, mbuga za Wanyama, vyanzo vya kudumu vya maji ikiwemo bahari, maziwa, mito na mabwawa, Milima na mabonde yenye maajabu mengi yanayowavutia hata wenzetu wa ng’ambo!
Sijutii kamwe, bali ni fahari kwangu kuzaliwa bongo land. Katika hili tunaongozwa na usemi wa baba wa Taifa aliyepata kusema ili tuendelee tunahitaji vitu vinne; Watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.
Si Kusini wala Magharibi ama Kaskazini na Mashariki kote ngoma droo. Utajiri mtupu. Asiyelima basi atafuga, asiyefuga atachimba madini ya Vito vya thamani. Aidha, asiye na madini, atavua viumbe maji ama atawekeza kwenye utalii na mwingine anaweza kufanya yote kadri anavyowiwa.
Baada ya karne nyingi kupita, 2025 Rais wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan amekuja na maono ya kumfikisha kijana kwenye ndoto yake anayoitamani. Ameunda Wizara mahususi kwa ajili ya kusikiliza hoja za vijana, kuwaongoza na kuwawezesha kufikia nchi ya ahadi ya asali na Maziwa. Inawezekana kabisa kila mmoja akiitumia kama fursa.

Aidha, amemteua Waziri Kijana mwenye karma ya kutoa semina lukuki kwa vijana akiwafundisha ujasiliamali na nidhamu ya fedha. Dkt. Joel Arthur Nanauka. Ameapa kuwatumikia vijana usiku na mchana kama sehemu ya kuhakikisha maono ya mwajiri wake yanatimia bila tashwishwi na tashititi. Tayari amaeanza kazi kwa kishindo. Ee Mungu msaidie!
Wizara inaongozwa na mtendaji mahiri Bi.Jenifa Christian Omolo, mchumi mbobezi akisaidiwa na Dkt.Kedmon Mapana Mzee wa vibe kuhakikisha mambo ya vijana yanakwenda sawia.
Viongozi hawa hawataki na hawapendi kuona vijana wana ndoto za kuwafikisha wanapopataka lakini wanakwama kwa kisingizio cha kukosa mitaji tena wakati huu ambao Dkt.Samia Suluhu Hassan amemwaga Bilioni 200 kwa ajili yao.
Tayari Mhe.Nanauka amekabidhiwa tangu tarehe 5Februari,2026 na Waziri Mkuu Dkt.Mwigula Lameck Nchemba kwenye hafla iliyofanyika Mlimwa ukumbi wa Waziri Mkuu kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali, ikiwemo vijana. Nami nilihudhuria aiseeee.
Tarehe 10 Januari,2026 Nanauka alizindua rasmi jukwaa la Vijana jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa JNICC na baadaye kulitambulisha mikoa ya Singida, Mwanza, Shinyanga,Tabora na Mtwara likiwahusisha vijana wa makundi mbalimbali wakiwemo Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati, Bodaboda, Wajasiriamali, wavuvi, Mama Lishe, Machinga na wengineo wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi, hususan katika sekta za usafirishaji, ufugaji, biashara, uvuvi, huduma, na ubunifu na kuwapa changamoto chanya kufikia maendeleo
Nanauka ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imewaweka vijana katikati ya ajenda ya maendeleo ya Taifa. Ndiyo maana tarehe 10 Januari 2026 jijini Dar es Salaam, Vijana Platform ilizinduliwa rasmi kama mfumo wa kitaifa wa kuwasikiliza, kuwahusisha na kuwawezesha vijana katika masuala ya ajira, ujasiriamali, ubunifu, teknolojia na uongozi.

Vijana Platform ni jukwaa linalowaunganisha vijana kutoka makundi mbalimbali wanafunzi wa vyuo, vijana wajasiriamali, vijana wa sekta isiyo rasmi, na vijana waliopo katika jamii ili waweze kushiriki mijadala ya maendeleo, kupata taarifa za fursa, na kushirikiana moja kwa moja na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo.
Malengo makuu ya jukwa hii ni kupanua ushiriki wa vijana katika mipango ya maendeleo, Kuweka daraja la mawasiliano kati ya Serikali na vijana, kuwaunganisha vijana na fursa za ajira, mitaji na ubunifu. Kujenga kizazi cha vijana wenye uongozi, uzalendo na maadili, Kubadili changamoto za vijana kuwa fursa za maendeleo.
”Napenda kutoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa maono yake makubwa kuhusu maendeleo ya vijana. Hii ni dhamira ya Serikali ya kuweka masuala ya vijana katika kipaumbele cha juu” ameongeza Mhe. Nanauka
Mhe. Nanauka amewasihi vijana kuachana na tabia za kukaa vijiweni na kupiga soga na badala yake watumie kikamilifu fursa zinazotolewa na Serikali na wadau mbalimbali katika kujiletea maendeleo kwani fursa ukizisogelea zinafunguka lakini ukiwa mbali haziwezi kufunguka.
“Bajaji za mabosi zinaumiza sana, kupoteza muda na kuwachosha vijana bila faida na tija yoyote anasema Wilbert Malale mwenyekiti wa Waendesha Bodaboda Buswelu Jijini Mwanza huku akitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwa kuwajali na kuwathamini vijana na kuamua kuwapa mikopo ya riba nafuu ya milioni 103 ili waweze kumiliki vyombo vyao usafiri.

Ipyana Job mmoja wa wanufaikaji kwenye kikundi cha “KITWIMA Youth Group” kinachoundwa na vijana 7 waliohitimu vyuo vikuu ngazi ya shahada wanaojishughulisha na ufugaji wa Samaki kwenye ziwa Victoria kwa njia ya vizimba anasema uanzishwaji wa Vijana Platform na utoaji wa mikopo ya riba na nafuu ni mpango wa Mungu uliopitishiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan. Mpango huu umekuja kuwakomboa vijana kutoka kwenye wimbi la umasikini. Kupitia Milioni 100 tuzokabidhiwa tunakwenda kujiajiri na kuajiri wengine
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 ni takribani milioni 20.6, sawa na zaidi ya theluthi moja ya Watanzania wote. Takwimu hizi zinaonesha wazi kuwa mustakabali wa Taifa hili unategemea nguvu, maarifa na ubunifu wa vijana.

