Na: Dk. Reubeni Lumbagala

Maji ni miongoni mwa huduma muhimu ya kijamii. Maji ni huduma ambayo kila mtu anahitaji tena kila siku. Utahitaji maji kwa kuoga, kupikia, kufulia, kupigia mswaki, kunyweshea mifugo, kumwagilia maua au bustani. Mambo yanayohitaji maji ni mengi. Maji haya yanapaswa kusambazwa kutoka katika vyanzo vyake mathalani mito, maziwa na mabwawa hadi katika makazi ya watu ili yaweze kutumiwa. Wananchi wanataka maji yawafikie katika makazi yao, hiyo ndiyo kiu na hitaji lao.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso anatoa ushuhuda wa hali ya maji iliyokuwa hapo nyuma. “Kitendo cha wananchi wa maeneo mbalimbali nchini kukosa maji kuliifanya Wizara ya Maji kuwa ni Wizara ya kero na lawama, lakini kwa kazi kubwa alizofanya Rais Dk. Samia, leo Wizara imekuwa faraja kwa wananchi,” anasema Aweso. Maneno ya Waziri Aweso yanatokana na ukweli kuwa katika maeneo mengi nchini, wananchi walikabiliwa na shida ya maji, hivyo walikuwa na lawama nyingi kwa Wizara ya Maji kwani ndiyo yenye dhamana ya kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi kule walipo, hivyo Wizara ya Maji haikuwa na namna ya kukwepa lawama hizo.

Kutokana na utashi wa kisiasa uliopo wa serikali wa kutatua kero za wananchi ikiwemo kero ya ukosefu wa maji, serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imechukua hatua stahili na madhubuti kuhakikisha Wizara ya Maji inakuwa faraja kwa wananchi kwa kuwafikishia huduma ya maji na hivyo maji kuchangia maendeleo ya sekta nyingine ili kwa pamoja kasi ya maendeleo iweze kuongezeka.

Waziri Aweso anakiri Rais Dk. Samia ameleta mageuzi makubwa ya kimaendeleo kwani miradi ya maji iliyokuwa imekwama sasa inafanya kazi na maji yanatoka. Ni ukweli mtupu kuwa Rais Dk. Samia anaumizwa na shida ya wananchi kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji ambayo wakati mwingine hayana uhakika wa kuyapata. Muda wa kufanya shughuli za kijamii na kiuchumi wananchi inabidi wautumie kutafuta maji kwa matumizi mbalimbali kama ya kupikia, kufulia na kuogea.

Ndoa zilikuwa zipo njia panda. Wanandoa wanagombana kwa sababu mke amechelewa kurudi nyumbani kutoka kisimani, bombani au mtoni kuchota maji. Watoto wanachelewa kwenda shule kutokana na kutafuta maji. Rais Dk. Samia amefanya kazi kubwa kwa kuongeza bajeti ya Wizara ya Maji kutoka shilingi bilioni 680.3 mwaka wa fedha 2021/2022 hadi shilingi trilioni 1.01 mwaka wa fedha 2025/2026. Mapinduzi haya makubwa yamefanikisha kuongezeka kasi ya usambazaji maji kwa wananchi hali inayoleta faraja badala ya lawama.

Rais Dk. Samia amefanikisha uzinduzi wa miradi ya maji kuwa endelevu badala ya miradi hiyo kutoa maji pale tu wanapokuja viongozi kukagua na kuzindua. Uendelevu wa miradi ya maji inatoa uhakika wa wananchi kupata maji safi, salama na yenye kutosheleza. Waziri Aweso anasisitiza Rais Dk. Samia kuwa kinara wa maji kwani miradi iliyokuwa imekwama tangu miaka ya 1970, sasa imekamilika na inatoa maji. Wizara ya Maji imekuwa faraja kwa wananchi kutokana na fedha za miradi kutolewa kwa wakati kugharamia miradi hiyo. Jambo la kufurahisha hapa ni kwamba, fedha nyingi za miradi ya maji ni mapato ya ndani (own sources) badala ya kutegemea misaada ya wahisani.

Kwa mujibu wa Waziri Aweso, katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Samia, zaidi ya shilingi trilioni tatu zimetolewa kugharamia miradi ya maji, jambo linaloongeza kasi ya usambazaji maji kwa wananchi. Katika kuendeleza tabasamu kwa wananchi, Wizara ya Maji inatekeleza mpango mkakati wa ujenzi wa Gridi ya Taifa ya Maji ili kuhakikisha maji yanakuwa ya kuhakika kwa matumizi mbalimbali ya kimaendeleo.

Katika Wiki ya Maji iliyozinduliwa Machi 16 hadi 22, 2026, Wizara ya Maji ina kila sababu ya kutembea kifuambele kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana likiwemo suala la upatikanaji wa maji kufikia asilimia 92.5 maeneo ya mijini na asilimia 85.2 maeneo ya vijijini. Kazi nzuri zimefanyika. Kwa maeneo ambayo maji hayajafika, dhamira ya serikali ni ile ile kuwafikishia wananchi wake wote maji safi, hivyo kazi ya kufikisha maji kwa wananchi wote inaendelea tena kwa kasi na viwango vikubwa.

Maoni: 0620 800 462.