Tanzania na Mauritius zimekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kwa lengo la kukuza biashara, uchumi wa buluu na maendeleo ya pamoja.

Hayo yamejitokeza wakati wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Mahmoud Thabit Kombo na alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kikanda na Biashara ya Kimataifa wa Mauritius, Mhe. Dhananjay Ramful Aprili 10,2026 pembezoni mwa Mkutano wa Tisa wa Bahari ya Hindi unaofanyika jijini Port Louis Mauritius Aprili 10 hadi 12, 2026.

Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Kombo amesisitiza uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Mauritius umejengwa juu ya msingi wa kuheshimiana, historia ya pamoja, na maslahi ya kimkakati yanayofanana, hali inayozidi kuimarisha mshikamano kati ya mataifa hayo mawili.

Aidha, alibainisha kuwa biashara kati ya nchi hizo imekua kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha mwaka 2017 hadi 2023 ambapo Uwekezaji wa Mauritius nchini umeendelea kuongezeka na kutoa ajira kwa Watanzania.

Pia alishukuru kwa fursa za masomo zinazotolewa na Mauritius kwa Watanzania na kuomba kuongezwa katika nyanja za mawasiliano, sayansi, akili unde na sayansi za afya.

Balozi Kombo alisisitiza umuhimu wa kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi, hususan katika sekta za biashara na Uwekezaji na kuwaita wawekezaji wa Mauritius kutumia fursa zilizopo nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, madini, nishati, utalii, TEHAMA na uchumi wa buluu, ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa pande zote mbili.

Alihimiza ushirikiano katika maeneo ya uvuvi wa kina kirefu, ufugaji wa samaki, usafirishaji wa baharini pamoja na usalama wa majini. Pia alieleza umuhimu wa kuimarisha utalii na usafiri wa anga kupitia ushirikiano kati ya mashirika ya ndege ya Tanzania na Mauritius.

Kwa upande wake, Mhe. Dhananjay Ramful alisisitiza haja ya kuongeza biashara kati ya nchi hizo na kuhimiza ushiriki mkubwa wa sekta binafsi. Viongozi hao pia walijadili masuala ya ushirikiano wa kikanda na kimataifa, wakisisitiza kulinda rasilimali za bahari, kuimarisha usalama wa Bahari ya Hindi, na kushughulikia changamoto za kimataifa kama mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, walikubaliana kuendeleza ushirikiano katika utalii, utamaduni na mahusiano ya watu kwa watu ili kuimarisha zaidi uhusiano kati ya nchi hizo.