Na. Asia Singano na Jordan Mbwambo, WF – Dodoma.
Serikali kupitia Wizara ya Fedha, inaendelea kutekeleza mageuzi yanayolenga kuimarisha sekta ya fedha, kuboresha upatikanaji wa fedha, na kuendeleza jukumu la ushirikishaji wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), alipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Kikundi cha Benki ya ECOBANK, ulipomtembelea ofisini kwake Wizara ya Fedha, Treasury Square jijini Dodoma.
Alisema kuwa Serikali inatambua nafasi muhimu ya taasisi za kifedha katika kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia uwezeshaji kwa njia mbalimbali ikiwemo kutoa mitaji kwa sekta mbalimbali za uzalishaji na uwekezaji.
‘’Haya ni pamoja na ukusanyaji wa mitaji ya muda mrefu kwa ajili ya miundombinu na sekta za kimkakati, upanuzi wa ufadhili wa biashara kuongeza huduma za kifedha za kidijitali ili kukuza ujumuishaji, na kutoa suluhisho za kifedha’’ alisema Mhe. Mhandisi Munde.
Alieleza kuwa kufikiwa kwa adhima ya uchumi imara kunahitaji ushiriki madhubuti wa sekta ya fedha, hususan katika kuwezesha miradi ya kimkakati inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
“Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili taasisi za kifedha ziweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi, sambamba na kuhakikisha kuwa huduma za kifedha zinawafikia wadau wengi zaidi,” alieleza Mhe. Munde.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Ecobank, Bw. Michael Larbie, alieleza dhamira ya taasisi hiyo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuendeleza miradi ya maendeleo kupitia utoaji wa huduma za kifedha zenye tija.
Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kifedha na kuongeza ubunifu katika utoaji wa mikopo na huduma nyingine za kifedha, ili kusaidia kukuza uwekezaji na shughuli za kiuchumi nchini.
Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Fedha, akiwemo Kaimu Kamishna, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema pamoja na Maafisa wengine wa Wizara ya Fedha pamoja na Maafisa kutoka Kikundi cha benki ya ECOBANK.








